TANGAZO
HABARI LEO.
WABUNGE wameishauri Serikali isifanye haraka kwa kuwasilisha
bungeni miswada ya sheria kuhusiana na masuala ya mafuta na gesi kwa sababu
mawazo yao hivi sasa yapo katika Uchaguzi Mkuu na wana mgogoro wa utulivu wa
mawazo na fikra.
Pia wamesema hakuna uharaka wa miswada hiyo kuwasilishwa kwa
hati ya dharura kwa sababu nchi haipo vitani, badala yake suala hilo liachwe
mpaka Bunge lijalo ili kuwe na umakini zaidi katika kuijadili.
Wakichangia hoja mbalimbali kwa nyakati tofauti wakati wa semina
ya wabunge hao kuhusiana na masuala ya mafuta na gesi iliyofanyika ukumbi wa
Msekwa bungeni mjini hapa jana, walisema mawazo ya wabunge wengi hivi sasa yapo
kwenye uchaguzi na si wakati mwafaka kujadili jambo zito na nyeti linalohusu
mafuta na gesi.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bunge juzi, kuanzia kesho
hadi Jumatatu wiki ijayo kutawasilishwa miswada mitatu inayohusu mafuta na gesi
ambayo ni Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya
Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Uwazi
na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015.
Mbunge Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema kuna
haja ya kujifunza kutokana na makosa na historia ya nyuma kwani walipitisha
sheria mbalimbali kuhusiana na madini, ambazo zimewaumiza Watanzania na zote
zilipitishwa siku moja kwa haraka kama inavyofanyika hivi sasa.
Alisema miswada hiyo ina vifungu vingi jambo ambalo kwa haraka
haraka kulijadili itakuwa si kuwatendea haki Watanzania, hasa wakati huu ambao
idadi ya wabunge ni ndogo bungeni ikiwa ni pamoja na wanaopitisha miswada
hawafiki 40 bungeni.
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), akichangia
hoja alisema haoni uharaka juu ya miswada hiyo na kuna haja kwa serikali
kuongeza umakini badala ya kukimbilia bila kufanya umakini na kwamba wanahitaji
mjadala mpana zaidi.
“Napenda mabadiliko lakini chanya, sijaridhika na miswada hii
mitatu. Haraka ya nini? Alihoji Chenge.
Kwa upande wake Mbunge wa Maswa, John Shibuda (Chadema), alisema
wabunge hivi sasa wana mgogoro wa utulivu wa fikra kuhusu Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, hivyo si vyema wakawa na jukumu la
kujadili jambo nyeti kama hilo.
Katika uchangiaji huo, kuliibuka tafrani alipokuwa akichangia
Mbunge wa Igunga, Dk Dalali Kafumu (CCM), ambapo wakati akiendelea kutoa hoja
ghafla Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage alisimama na kuanza
kujibishana naye kwa hasira bila ruhusa ya Mwenyekiti.
Naibu Waziri alionekana kukerwa na uchangiaji wa Kafumu, hasa
alipodai sehemu kubwa ya sheria za miswada hiyo wamechukua katika sheria za
Uganda.
“Tusiharakishe katika hili, tupate muda wa kutosha. Sheria
nyingi humu ni kama za Uganda yaani ni ‘copy na kupaste’, pengine walichoondoa
humu ni jina la Uganda,” alisema na kusababisha Mwijage kupanda hasira, ingawa
kwa waliokuwa nje ya ukumbi ilikuwa ngumu kujua alikuwa anasema nini, lakini
ishara ya mikono yake ilionesha alikuwa na hasira na pengine umbali baina yao
ulisaidia kuzuia mengine zaidi.
Tukio hilo la Mwijage lilisababisha Mwenyekiti wa semina hiyo,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, ambaye pia ni Mbunge
wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) kumuonya kwamba halikuwa la kiungwana. “Mimi
ndiye Mwenyekiti wa kikao hiki, si vizuri kuanza kumnyooshea kidole mbunge mwenzako.
Si jambo zuri,” alisema na kumruhusu Kafumu kuendelea, ambapo Mbunge huyo wa
Igunga alimuomba radhi Mwijage kama kauli hiyo ilimkwaza, lakini akisisitiza
wajipe muda wasije wakajilaumu.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema wanasiasa
wakatae miswada hiyo na itaenda kuibua mgogoro mkubwa kuhusiana na masuala ya
mafuta kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kwani suala la mafuta ni kati ya mambo
yenye mgogoro katika Muungano na kusema hivi sasa mawazo ya wabunge kwa suala
nyeti kama hilo itakuwa ngumu.
Wabunge wengine waliochangia na pia kuzungumzia usiharakishwe
huku wakigusia uharaka na suala la mahudhurio ni Mbunge wa Viti Maalum, Mary
Mwanjelwa (CCM), Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangwala, Mbunge wa Kasulu Mjini,
Mosses Machali (NCCR Mageuzi), Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP).
Mbunge Mwanjelwa alisema kuna haja jambo hilo wasiliharakishe,
maana mawazo yao yapo katika uchaguzi na pia kuna haja ya elimu zaidi kwa umma
ikatolewa kuhusiana na miswada hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP),
alisema suala la mahudhurio ya wabunge ni mtihani mkubwa kwa jambo nyeti kama
hilo na kwamba hata Kamati ya Bajeti ambayo yeye ni Makamu Mwenyekiti wakati
mwingine inakuwa na wajumbe wachache.
“Si wakati wa kutunga sheria, tutajiaibisha mbele ya umma,”
alisema na kuungwa mkono na Kigwangwala aliyesema yeye ni miongoni mwa wabunge
ambao karibu mwezi mzima hawajahudhuria vikao na macho ya wengi yapo katika
uchaguzi.
Mbunge wa Muheza, Herbert Mtangi (CCM) ndiye pekee jana mchango
wake ulionekana kuitaka miswada hiyo, akisema kuna haja ya sheria kupitishwa
haraka ili ianze kutumika.
Akizungumza awali wakati wa semina hiyo kabla ya michango ya
wabunge, Waziri Simbachawene, alisena Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji
katika Tasnia ya Uchimbaji ikipitishwa itafanya mikataba yote ya madini na gesi
iwe wazi na halitakuwa jambo la siri kama ilivyo sasa. Pia alisema sheria hiyo
itaweka uwazi katika leseni na mikataba ya madini, gesi na hata mafuta
yakipatikana.
Alisema Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia
ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015 ukipitishwa na kuwa sheria pamoja na mambo
mengine italazimisha uwepo wa uwazi katika mikataba ya gesi, madini na mafuta
tofauti na sasa, ambapo ni jambo la siri.
Waziri Simbachawene alisema Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa
Gesi na Mafuta ya mwaka 1980 inasema lazima kuwe na usiri kwenye mikataba,
lakini katika muswada unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni unafuta jambo hilo na
unasema kunatakiwa kuwe na uwazi juu ya mikataba ya aina hiyo.
Pia alisema ushiriki wa Watanzania lazima uwe wazi ijulikane
wameshiriki kwa kiasi gani tofauti na sasa na kwamba pia gharama za uwekezaji
na uzalishaji nazo zinatakiwa kuwa wazi.
Alisema sheria italazima kujua taarifa kuhusu uwekezaji kama ni
halisi na sahihi na kwamba hilo ni jambo muhimu na ndiyo sababu wanataka uwazi
uwe katika sheria.
Baadaye jana baada ya michango ya wabunge, alisema kama miswada
hiyo isipopelekwa nchi itaathirika kwa mambo hayo na pia itasababisha matarajio
kuhusu masuala ya uzalishaji wa gesi kwa sheria kuanzia mwaka 2018/2019 isubiri
hadi mwaka 2023/2024.
Pia alisema itakuwa maumivu kwa Watanzania wanaotaka kuwekeza
katika sekta hiyo na wawekezaji wengine na itaathiri uwekezaji kwa ujumla.
Alisema miswada yote ilishapitia hatua muhimu na alitarajia jana
ingekuwa wabunge waboreshe na kusema serikali inaliachia Bunge ili liwape
muongozo kwani wao walishamaliza ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau na
kupata maoni yao.
Naye Ndassa akifunga semina hiyo aliwashauri wabunge kwamba
miswada hiyo ipelekwe kwa sasa kutokana na umuhimu wake na kama kutakuwa na
mabadiliko basi serikali itakuja kuifanyia, lakini kwa mazingira ya sasa
wasiiondoe, lakini akisisitiza atamjulisha Spika, Anne Makinda kuhusu maoni ya
wabunge kwenye semina hiyo.
MWANANCHI.
Hiki ni kivumbi.
Kati ya wagombea 42 waliojitokeza kuwania urais kupitia CCM, anatakiwa kubaki
mmoja tu na mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu unafungwa kesho.
Kuimarisha uchumi
kwa kutumia mbinu mbalimbali, kupambana na rushwa na ufisadi, kuboresha elimu,
kukuza ajira kwa vijana na kuboresha uwajibikaji ni baadhi ya ahadi
zilizotawala na makada 42 waliochukua fomu.
Hadi sasa ni kada
mmoja tu, Hellen Elinawinga ametangaza kutoendelea na mchakato huo.
Gazeti la
Mwananchi linapitia ahadi hizo kwa kifupi.
Samweli Sitta
Waziri huyo wa
Uchukuzi ameahidi kupambana na rushwa, kutenganisha uongozi na biashara na kila
mara amekuwa akisisitiza kuwa: “Nitahakikisha inaandaliwa sheria maalumu ambayo
itawalazimisha watu kuchagua kati ya biashara na uongozi.”
Dk Titus Kamani
Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ameahidi kupambana na changamoto za afya, ajira na
uchumi. Jingine ni kuangalia makundi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake
na wastaafu.
Profesa Sospeter Muhongo
Mbunge wa
Kuteuliwa na Rais ameahidi kukuza uchumi kwa kusimamia mafuta, gesi, umeme na
elimu ili kuwakwamua wananchi katika lindi la umaskini. Pia kukuza uchumi wa
nchi kwa asilimia 7.5 hadi asilimia 10 mpaka 15 kwa kipindi cha miaka mitano au
10.
Edward Lowassa
Mbunge wa Monduli
amepania kuinua vijana katika ajira, kusimamia Muungano, kuinua elimu na uchumi
wa nchi kupita rasilimali za ndani. Pia, kutatua migogoro ya ardhi ya wakulima
na wafugaji. Katika michezo ameahidi, kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri
katika ramani ya dunia na kwamba ataweka mkazo zaidi katika mchezo wa riadha.
Mwigulu Nchemba
Naibu Waziri wa
Fedha amejitosa kupambana na umaskini, kusimamia ulipaji kodi ili kulipa Taifa
mafanikio ya kiuchumi. Pia, kupinga utitiri wa kodi bila huduma husika na
muhimu kutolewa na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma.
Balozi Amina Salum
Ameahidi
kusimamia uchumi na maendeleo, kitu ambacho kitakuwa na jukumu la kutoa ushauri
wa haraka kuhusu maeneo na aina ya uwekezaji unaohitajika.
Pia ameahidi
kuondoa kasoro za mfumo dume ambao unachangia kudumaza huduma za msingi kwa
wanawake.
Profesa Mark Mwandosya
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Kazi Maalum) ataanzisha kilimo cha kisasa na kisayansi
kinachozingatia sifa zote za kilimo cha kisasa kwa kuboresha pembejeo na
miundombinu.
Pia atapambana na
rushwa kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia mapapa wa rushwa wasishughulikiwe na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Frederick Sumaye
Ameahidi kukuza
uchumi kwa kuweka msukumo katika kilimo, kuboresha mbegu, kutafuta masoko na
kusimamia viwanda vya ndani.
Pia ataunda
mahakama maalumu ya kushughulikia rushwa, ufisadi, uhujumu uchumi na biashara
ya dawa za kulevya.
Mizengo Pinda
Waziri Mkuu,
ameahidi kuanzia pale Serikali ya Awamu ya Nne itakapoishia akisema
yanayoonekana sasa ni matunda ya CCM.
“Nikiingia
nimepanga kuongeza ukuaji wa uchumi wa pamoja ili kuondoa wigo kati ya mwenye
nacho na asiyekuwa nacho.”
William Ngeleja
Mbunge wa Sengerema
amesema atapambana na maadui sita ambao ni maradhi, umaskini, ujinga, maradhi,
rushwa, ufisadi na kukuza maadili.
Benard Membe
Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ameahidi kusimamia utawala bora kwa
kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika nafasi yake kwa uadilifu na
kuzingatia sheria za nchi. Pia atasimamia utawala bora, elimu na maendeleo ya
jamii.
Peter Nyalali
Ameahidi kukuza
demokrasia, kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali zikiwamo za uchumi,
jamii, michezo, nishati, utawala bora na kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa
vijana na kusimamia usalama wa Taifa.
January Makamba
Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ameahidi kuinadi Ilani ya CCM na kuunda
baraza dogo la watu 18, waadilifu na wachapakazi.
Dk Khamis Kigwangalla
Mbunge wa Nzega
atapambana na rushwa ikiwa ni pamoja na kuichukia, kukuza ajira, kubana
matumizi kuwezesha wajasiriamali kupambana na umasikini.
Luhaga Mpina
Mbunge huyo wa
Kisesa ameahidi kukuza uchumi kwa kuongeza misingi ya upatikanaji wa fedha. Kuongeza
mapato ya nchi na kuyasimamia kwa manufaa ya nchi na wananchi kwa ujumla.
Lazaro Nyalandu
Waziri wa
Maliasili na Utalii ameahidi kujenga uchumi imara utakaosaidia kupunguza ukali
wa umaskini kwa wananchi na kuwawezesha wananchi mmojammoja kupata kipato
kulingana na shughuli anazofanya.
Dk Augustine Mahiga
Balozi huyo
mkongwe ameahidi kuongeza kipato cha kati cha wananchi, kukuza uchumi kwa
kupambana na umaskini kwa kutoa msukumo katika kilimo, viwanda, uchukuzi na
utalii.
Dk Mwele Malecela
Mtaalamu huyo wa
masuala ya tiba ameahidi kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa watu wote,
kutoa elimu ya ufundi ili kuongeza ajira kwa vijana, msukumo mkubwa ukiwa
kukuza uchumi.
Elidephonce Bihole
Ameahidi
kuwapeleka Watanzania katika nchi ya ahadi, kuinua uchumi wa nchi kwa kutumia
rasilimali zilizopo.
Dk Hassy Kitine
Amepania
kuirudisha Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere, kuwa na sera sahihi za maendeleo
ya nchi, kuinua kilimo, viwanda, uchukuzi, afya, elimu na kuinua maisha ya kila
mwananchi.
Dk Asha-Rose Migiro
Waziri huyo wa
Katiba na Sheria ameahidi kutekeleza Ilani ya CCM kuendelea kukuza uchumi
utakaowafikia wananchi walio wengi zaidi.
Joseph Chagama
Ameahidi
kupambana na tatizo la ajira kwa vijana. Kusimamia utekelezaji wa Sheria ,
uadilifu na elimu.
Balozi Ali Karume
Mwanadiplomasia
huyo ameahidi kuwapo kwa uhuru bila kujali dini, itikadi za vyama, elimu wala
vyeo, kupambana kukuza kilimo kwanza na elimu baadaye anasema ni ngumu kusoma
kama una njaa.
Makongoro Nyerere
Mbunge wa Afrika
Mashariki anasema vipaumbele vyake vitatokana na ilani ya CCM.
Maliki Malupu
Ataboresha elimu,
kilimo kwa kuwa na mbegu bora kuongeza msukumo katika kilimo chenye tija na
kumwezesha mkulima mdogo kujikimu.
Dk Ghalib Bilal
Makamu wa Rais atasimamia uwajibikaji katika sekta ya umma,
kulinda haki za binadamu na kuongoza kwa misingi ya sheria. Pia, kusimamia
matumizi mazuri ya rasilimali za Taifa na kuboresha usimamizi wa mapato. Amos Siyantemi
Atadumisha amani,
kurudisha mfumo wa mabalozi wa nyumba 10, kuwafilisi mali wote watakaokamatwa
na rushwa.
Dk John Magufuli
Waziri wa Ujenzi
ameahidi kutekeleza kwa nguvu zote ilani ya CCM.
Jaji Augustino
Ramadhani
Ameahidi
kuyaangalia mapendekezo ya wananchi yaliyoachwa kwenye Katiba Inayopendekezwa
na kuyatafutia dawa mapema matatizo yakiwamo ya rushwa, ufisadi na tatizo la
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Dk Mussa Kalokola
Amesema
atakomesha unyanyasaji wanaofanyiwa Watanzania na kurejesha mfumo utakaoleta
mchangamko wa uchumi, ambao unadorora kwa kukosekana uongozi bora.
Ritta Ngowi
Atakuza uchumi,
kujenga kituo cha kulea kuwahudumia wastaafu, walemavu na wasiojiweza.
Monica Mbega
Atatekeleza ilani
ya CCM na kuendeleza mazuri yaliyofanywa na waliotangulia.
Nicholas Mulenda
Atahakikisha CCM
inakuwa imara zaidi.
Banda Sonoko
Ameahidi kuvaa
viatu vya Mwalimu Nyerere kwa kusimamia nchi kujiendesha kwa kodi za nchi na
kufufua uchumi wa viwanda.
Helen Elinawinga
Atapambana na
adhabu za vifo kwa viongozi.
Dk Harrison Mwakyembe
Atatekeleza ilani
ya CCM, kupambana na rushwa kwa nguvu zote.
Mathias Chikawe
Ataendeleza
mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini na kupiga vita ufisadi.
Antony Chalamila
Ameguswa
kuwatumikia wananchi.
Veronica Kazimoto
Ameahidi kuinua
uchumi na kumfikia kila Mtanzania
Peter Nyalali
Ameahidi kukuza
demokrasia pamoja na kuleta mabadiliko chanya katika nyanja mbalimbali.
Stephen Wasira
Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushiriki ameahidi kuleta mageuzi katika kilimo akisema jembe la
mkono litapelekwa makumbusho kuwa historia.
HABARI LEO
SERIKALI imeanza msako wa mtu au watu waliohusika na hujuma ya
mafuta, kwa kutouzia wateja wa reja reja, pamoja na wanaosambaza ujumbe mfupi
wa maandishi, kutisha kuwa mafuta hayatapatikana hadi leo.
Aidha, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imetakiwa
ibadilike na kuendana na wakati kwa kutangaza bei mpya za mafuta kila
inapobidi, badala ya kusubiri kupitishwa kwa bajeti za Serikali.
Akizungumzia msako huo bungeni mjini hapa jana, Naibu Waziri wa Nishati
na Madini, Charles Mwijage alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa za kuwepo
kwa vituo vya mafuta vinavyo ficha petroli na dizeli, kusubiri bei inayoanza
leo, alimwagiza Inspekta Mkuu wa mamlaka hiyo, ampe orodha ya majina ya watu
hao.
Mwaijage alisema, kwa Dar es Salaam pekee maofisa ukaguzi wa
EWURA walivikagua vituo nane vilivyotajwa kuacha ghafla kuuza mafuta, lakini,
baada ya ukaguzi, iligundulika kuwa havikuwa na mafuta katika hifadhi zake.
“Kwa sababu hiyo, ninapenda kuwaambia wananchi kuwa, hawana
sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu mafuta. Tunayo ya kutosha na hata kama
inatokea kuwepo kwa anaye yaficha, hatua zitachukuliwa dhidi yake, ikiwa ni
pamoja na kutozwa faini ya Sh milioni 20,” alisema.
Kwa mujibu wake, Waziri wa Nishati anayo mamlaka ya kuamuru meli
ilete mafuta ikiwa kuna tatizo, na kwamba, kwa hilo la kutengenezwa na
wachache, wanalimaliza kwa kuamuru walioyaficha wayatoe, vinginevyo watafutiwa
leseni pia.
“Ninapenda kuwaambia Watanzania kuwa, nchi hatuna shida ya
mafuta katika hifadhi. Tunachokifanya sasa ni kuendelea kuwasaka waliohusika
kufanya hujuma hiyo, pamoja na wanao sambaza ujumbe mfupi wa maandishi kutisha
watu kuhusu suala hilo,” alisema.
Wakati huo huo, Naibu Spika, Job Ndugai alisema jana kuwa hujuma
hiyo ya mafuta isingetokea endapo EWURA ingewahi kutangaza bei ya mafuta,
badala ya kusubiri bajeti ya Serikali.
“Ni vizuri mamlaka hiyo ikaweka utaratibu mzuri wa kutangaza bei
zake mapema inapobidi kuepusha wafanyabiashara ya mafuta wasiyafiche kusubiri
bei mpya. Kwa mambo kama EWURA haina jinsi bali kuchangamka na kutangaza bei”.
Awali, akimjibu Mbunge wa Ubungo, John Mnyika aliyeomba mwongozo
wa Spika akitaka mgogoro huo wa mafuta ujadiliwe, Ndugai alisema: “Ninaomba
suala hili lisijadiliwe, kwa sababu ni la kuisha kesho (leo) tu bei mpya za
mafuta zikitangazwa.
WASTANI wa ufaulu kwa shule za sekondari za Serikali za kata
umezidi kuimarika na kukaribia shule za Serikali ambazo ni kongwe.
Hayo yalibainishwa katika tathmini ya Baraza la Mitihani
Tanzania (Necta) iliyofanywa kwenye matokeo ya Kidato cha Nne na cha Pili kwa
mwaka 2014.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk
Charles Msonde ameelezea tathmini hiyo wakati wa uzinduzi wa vitabu vya
uchambuzi wa matokeo kwa Kidato cha Pili na Nne sambamba na uzinduzi wa mfumo
kompyuta wa upatikanaji wa matokeo ya mitihani kwa njia ya simu kupitia ujumbe
mfupi (SMS PORTAL).
Alisema wakati mwaka 2012 wastani wa ufaulu wa shule za kata
ulikuwa ni asilimia 35.40, ufaulu katika shule za Serikali kongwe ulikuwa ni
asilimia 15.81 na kwa mwaka 2014 ufaulu huo umepanda hadi kufikia asilimia
64.49 kwa shule za Serikali kongwe na asilimia 63.56 za wananchi hiyo kuwa na
tofauti ya asilimia 0.93.
Aidha, ufaulu wa shule za umma katika mtihani wa kidato cha nne
umepanda kwa asilimia 13.30 kutoka asilimia 50.48 kwa mwaka 2013 hadi kufikia
asilimia 63.78 mwaka 2014 wakati ongezeko la ufualu kwa shule zisizo za
serikali ni asilimia 1.21 kwa mwaka 2014.
“ Tathmini ya kina ya matokeo imebaini kuwa ufaulu wa shule za
Serikali unazidi kuimarika mwaka hadi mwaka. Hata ufaulu katika shule za
Serikali za wananchi dhidi ya shule za Serikali Kongwe unadizi kuimarika,
pamoja na mafanikio hayo, jitihada za pamoja zinahitajika katika kuboresha
ufundishaji na ujifunzaji,” alisema.
Aidha, Msonde alisema takwimu za ufaulu wa mwaka 2014 kimasomo
zinaonesha kuwa ufaulu kwa baadhi ya masomo katika mitihani ya darasa la saba,
kidato cha pili na nne siyo wa kuridhisha hivyo kuhitajika juhudi za kuboresha
ufundishaji na ujifunzaji utoaji wa elimu nchini.
Kuhusu mfumo wa utoaji matokeo kwa njia ya simu, Msonde alisema
Baraza limezindua mfumo huo ili matokeo ya taifa yanapatikana kwa urahisi na
kuondoa usumbufu kwa watahiniwa na wadau wa elimu bila kujali mahali walipo.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
alisema Serikali ya Awamu ya Nne imepanua elimu ya sekondari kwa kujenga shule
za wananchi kwa kila kata ili kuongeza fursa kwa Watanzania kupata elimu hiyo.
Alisema matokeo ya juhudi hizo yameanza kuonekana kwa kuwa na
ongezeko la wanafunzi wanaohitimu masomo ya kidato cha nne na sita ambapo
kutoka mwaka 2015 idadi ya wahitimu ilikuwa ni 87,560 ukilinganisha na wahitimu
244,902 kwa mwaka 2014 kwa kidato cha nne na sita wamepanda kutoka 17,1123 hadi
35,650.
“ Kwa kipindi cha miaka 10 mafanikio ni makubwa, wahitimu wa
kidato cha nne wa waliokuwa wanazalishwa kwa miaka mitatu mwaka 2005, lakini
mwaka 2014 wanazalishwa kwa mwaka mmoja. Aliongeza: “ Pia shule ambazo baadhi
ya watu walikuwa wanazibeza, wakati umefika sasa ambapo hatutazibeza.
Watanzania wanatakiwa kuacha kuishi katika historia.”
Kuhusu vitabu vya uchambuzi wa matokeo, Kawambwa aliwataka wadau
kuhakikisha wanafikisha vitabu hiyo kwa walengwa kwa wakati ili wavitumie
katika kuboresha elimu.
Aidha, Kawambwa amelipongeza Baraza kwa kusimamia ratiba za
mitihani na kudhibiti ufujaji wa mitihani kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi (Elimu,
Majaliwa Kassimu Majaliwa, amewataka maofisa elimu wa halmashauri zote nchini wa
idara ya msingi na sekondari (ambao wote walikuwepo kwenye uzinduzi)
kuhakikisha wanavisambaza vitabu kwenye shule zote ndani ya siku 14 ili
kuhakikisha vinawafikia wadau wa watumie kujisahihisha kabla ya kufanyika kwa
mtihani wa kidato cha nne mwezi Novemba mwaka huu.
“ Nisingependa kusikia kuna Halmashauri imewataka wakuu wa shule
waje kuvifuata katika halmashauri, nasisitiza tuvisambaze wenyewe kila shule,
maofisa elimu wa mikoa na wakaguzi wa kanda mna jukumu la kufuatilia ili
kuhakikisha vimewafikia walengwa na vinatumika kama ilivyokusudiwa,” alisema.
Aidha, Majaliwa amezitaka halmashauri nchini kutumia uchambuzi
huo katika kupanga namna ya kuondoa mapungufu yaliyobainishwa katika shule za
maeneo yao.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD