TANGAZO
WASIFU Umri: Miaka 43 Elimu: Msingi
katika shule ya Msingi Mkomaindo Halmashauri ya Mji wa Masasi na baadae shule
ya msingi Kiwalala Halmashauri ya wilaya ya Lindi Vijijini. Kazi: Msanii
Mchekeshaji anayetumia Lafudhi ya Lugha ya Kimakonde katika kusema mambo ambayo
wananchi hawayajui.
Historia yake
Msanii Ismail Issa Makombe maarufu “Baba Kundambanda”ni msanii
mwenye kipaji cha uchekeshaji ambaye kwa siku za hivi karibuni amejizolea
umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake wa kuzungumza masuala mbalimbali
ambayo yamekuwa yakileta mabadiliko kwa wananchi. Makombe amekuwa akitumia
lafudhi ya kimakonde katika kuimba lakini yeye sio mmakonde bali ni mmakua wa
wilaya ya Masasi. Alizaliwa Februari 05, 1972 katika Hospitali ya Mkomaindo wilayani
Masasi mkoani Mtwara. Baba yake mzazi mzee Issa Makombe ambaye kwa sasa ni
marehemu aliwahi kuwa mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wa kata ya
Migongo,dereva wa idara ya ujenzi halmashauri ya wilaya ya Masasi na makamu mwenyekiti
wa chama cha msingi Mkuti.
Mama yake mzazi ni Bi.Maimuna Kavinga ambaye bado yuko hai na
kwa sasa anaishi mtaa wa Migongo Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara
akiendelea na shughuli zake za kilimo.
Alianza elimu ya Chekechea mwaka 1979 eneo ambalo lilikuwa
linaitwa Mzambarauni karibu na kanisa la Anglikana mtaa wa Mkomaindo Masasi na
alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi
Mkomaindo wilayani Masasi ambako alisoma darasa la kwanza hadi la tatu
kati ya mwaka 1980 – 1982, lakini baadae alihamia huko katika shule ya msingi
Kiwalala ambako alihitimu elimu ya msingi mwaka 1987.
Sababu za kuhamia huko katika kijiji cha Kiwalala ni kumfuata
baba yake mkubwa Mzee Makombe aliyekuwa anaishi huko kwa wakati huo.
Bwana Ismail Makombe hakubahatika kuchaguliwa kuendelea na
masomo ya kidato cha kwanza ambapo baada ya kumaliza elimu ya msingi huko
kiwalala aliamua kurudi wilayani Masasi katika mwaka wa 1988.
Mwaka 1989 aliamua kujifunza kazi ya uashi (ujenzi wa majumba)
kwa mafundi wa kawaida wa mitaani ambapo alihitimu mafunzo hayo na akaanza
kufanya kazi hiyo ya ujenzi iliyomwezesha kuishi na kusaidia wazazi wake na
alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1990.
Katika Mwaka 1991 aliamua kuondoka Masasi na kwenda wilayani
Songea katika mkoa wa Ruvuma na alikaa huko kati ya mwaka 1991-1994 akiendelea
na shughuli zake za ufundi wa majumba ambapo Juni, 1994 aliamua kurudi Masasi.
Kundambanda alikaa mjini Masasi kwa muda wa miezi mitano tu na
baadae Novemba 1994 aliamua kuondoka na kuelekea jijini Dar es salaam kwenda
kutafuta maisha kwani katika kipindi hiko chote bado mambo yalikuwa hayaendi
sawia katika upatikanaji wa kipato.
Mwanaharakati huyo kuwahi kutokea katika historia ya mikoa ya
kusini mwa Tanzania alipofika Dar aliendelea na kazi yake ya ujenzi wa majumba
lakini uzito wa matofali ya saruji ndio kitu ambacho kilimfanya aachane na kazi
hiyo na kuanza shughuli ya kusukuma mkokoteni huko katika Mtaa wa Tegeta
Kibaoni mkoani Dar es salaam.
Kazi ya kusukuma mkokoteni aliifanya kati ya mwaka 1995-1998 iliyomwezesha
kuishi mjini na kuweza kulipa kodi ya chumba ya shilingi 2500 kwa mwezi lakini
bado maisha yalikuwa magumu kwake ambapo aliamua kuachana na kazi hiyo na
kuingia kwenye kazi ya kupakia kwenye gari viroba vya ngano huko kariakoo na
kuvileta Tegeta kazi ambayo alikuwa analipwa shilingi 3500 kwa siku.
Baada ya kuona bado maisha yanazidi kuwa magumu aliamua kuachana
na kazi hiyo ya mkokoteni na aliamua kujifunza udereva na ufundi wa magari na
hiyo ni kati ya mwaka 1999-2000 na baada ya kuhitimu mafunzo hayo alifanikiwa
kupata leseni na alianza rasmi kazi ya udereva wa daladala kati ya
Tegeta-Mwenge jijini Dar es salaam.
Bwana Kundambanda alifanya kazi ya udereva wa Daladala kwa
kipindi cha Miaka sita kati ya mwaka 2001-2006 kwa daladala ya Tegeta-Mwenge
lakini mwishoni mwa mwaka 2006 alianza kuendesha magari makubwa(Malori) ambapo
kwa bahati mbaya alipata ajali aliyosababisha avunjike mikono yake yote miwili.
Kutokana na kupata ajali hiyo aliamua kurudi kijijini Kiwalala Lindi
vijijini kwa lengo la kujiuguza na baada ya kupona Novemba 2007 alirudi tena
Dar lakini wakati huu sasa aliingia rasmi kwenye sanaa ya uchekeshaji na
alifanya sanaa akiwa chini ya kampuni yake ya Karem Video Production iliyokuwa huko Tegeta
na alifanikiwa kutoa filamu iliyoitwa “TRAFIKI” pamoja na kazi zingine nyingi na
alifanya kazi na kampuni yake kati mwaka 2008-2010.
Mwaka 2011-2014 alianza kufanya kazi na kampuni ya Ally Riyami
Video Production na kufanikiwa kufanya kazi zaidi ya 300 na kampuni hiyo lakini
ilipofika mwaka 2013 alipata ugonjwa wa ngozi akiwa Mkoani Tanga.
SIASA:
Bwana Ismail Makombe “Baba Kundambanda” alianza kupenda na
kufuatilia masuala ya kisiasa tangu mwaka 1999 pale alipoanza kusoma taarifa na
makala mbalimbali kupitia magazeti ya Raia mwema,Rai,Dira na Mwanahalisi ambapo
alisema magazeti hayo ndiyo hadi sasa yemempa uwezo wa kujiamini na kutetea
hoja zake.
Alianza kufanya kazi za siasa kama mwanaharakati na wakati huo
hakuwa na kadi ya chama chochote cha siasa nchini huku mapenzi yake makubwa
yakiwa kwa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lakini alitumia usanii
wake katika kufikisha ujumbe kwa jamii ambapo alishauriwa na watu kuwa ni vyema
awe na kadi ya chama cha siasa aweze kufanya kazi zake kwa uhakika zaidi.
Baada ya kuona anaweza kufanya kazi za kisiasa mnamo Desemba 27,
2012 alijiunga rasmi na chama cha Wananchi CUF kama mwanachama wa chama hicho
na alifanikiwa kupewa kadi ya uanachama yenye namba-0980635 iliyotolewa katika
tawi la Migongo Halmashauri ya mji wa Masasi.
Mwaka 2014 alianza kufanya mikutano mbalimbali ya kisiasa akiwa
mwanachama wa CUF na kwamba katika mwaka 2015 pekee tayari ameshafanya mikutano
32 kwenye jimbo la Masasi huku akitumia kiasi cha shilingi 52,000/= pekee kwani
mikutano yake yote inaandaliwa na wananchi wenyewe.
Aidha katika kipindi chote cha maisha
yake Bwana Ismail Makombe amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo katibu mtendaji wa chama
cha usafirishaji wa abiria kwa daladala za Dar es salaam –Bagamoyo kati ya
mwaka 2008-2010.
MAFANIKIO KATIKA SANAA:
Baba kundambanda hadi sasa katika sanaa amefanikiwa kuimba
nyimbo zaidi ya 32 lakini kati ya hizo anasema kuwa nyimbo maarufu ni pamoja na
Mwalimu,Gesi,Wabunge wa Kusini,Usalama wa Raia pamoja na dua ya kuliombea Taifa
ni nyimbo ambazo zimempa umaarufu mkubwa nchini.
HALI YA NDOA:
Kundambanda ameoa na amefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume
anayeitwa Makombe Ismail Makombe mwenye umri wa miaka mitano (05) ambaye kwa
sasa anaishi mkoani Mtwara huku mkewe akiitwa Shamsa Ismail na kwa sasa
Kundambanda anaishi Chiumbati wilayani Nachingwea ambako anaendelea kupata
matibabu ya ugonjwa wake wa Ngozi.
Msanii
Ismail Makombe kama ilivyo kwa baadhi ya watia nia wengine ni mara yake ya
kwanza katika historia ya maisha yake kutangaza nia yake ya kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Masasi kwa tiketi
ya UKAWA.(Akitokea chama cha Wananchi CUF).
Kundambanda
amesisitiza kuwa huu ni mwaka wa mabadiliko:
“Sisi
ni watu na si vitu…na sifa ya mwanadamu yeyote aliyeumbwa na mwenyezi mungu ni
kufikiri,kubadilika pamoja na kuangalia ni wapi alikotoka,alipo na anakokwenda.
Akizungumzia
kuhusu watu wanaombeza kuwa hana elimu alisema wana Masasi wanahitaji mtu
mwenye uzalendo,mwenye dhamira ya kweli ya kuwaondoa wananchi pale waliponasa
kwenye matope na kuwapeleka mbele kwenye maendeleo.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD