TANGAZO
Waziri Hawa Ghasia |
Na Mwandishi wetu,Mtwara.
BAADHI ya Halmashauri zimeonywa
kuacha mara moja tabia ya kuitegemea
serikali kuu na badala yake iwe na vyanzo vya mapato vya ndani kwa ajili ya
shughuli za kimaendeleo katika halmashauri zake.
Hayo yamesemwa leo na Waziri Wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Hawa
Ghasia wakati wa kufungua kongamano la utekelezaji wa ajenda ya maendeleo baada
ya mwaka 2015 lililofanyika mkoani Mtwara.
Kongamano hilo lilikuwa na kauli
mbiu isemayo, “Mwananchi pigia kura katiba pendekezwa na chagua viongozi bora
kwa maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.
Ghasia alisema kuwa halmashauri
nyingi zimekuwa tegemezi na hivyo pale pesa zinapochelewa kufika katika
maeneo yao zimekuwa zikishindwa kusonga mbele zaidi katika miradi na hali hiyo
inasababishwa na kukosa vyanzo vya mapato ndani ya halmashauri.
“Kazi ya serikali kuu ni kutunga
sera na kusimamia pamoja na kuweka viwango, lakini ikumbukwe serikali za mitaa
kazi yake ni kutekeleza kwani zipo karibu na wananchi kwa hiyo mwananchi wa
kawaida akilalamika moja kwa moja analalamikia mamlaka za serikali za mitaa’“.alisema
Ghasia.
Akizungumza Mwenyekiti wa ALAT Taifa,
Didas Masaburi alisema asilimia kubwa
halmashauri nyingi zinakumbwa na madeni kutokana na kukosa vyanzo vya mapato
ndani ya halmashauri hizo kutokana na kuitegemea serikali kuu.
Alisema hakuna halmashauri hata
moja ambayo haina deni chini ya miaka miwili ama mitatu kutokana na mapato
wanayopata kutoka serikali kuu kuweza kuchelewa ama kuwa madogo na hivyo
kushindwa kujiendeleza.
“Tatizo la halmashauri kutegemea
serikali kuu bado ni changamoto kubwa sana kwani wengi wao hawana vyanzo vya
mapato ndani ya halmashauri na ukiangalia halmashauri zote hakuna hata moja
ambayo haina deni si la chini ya miaka miwili ama mitatu,”alisema Masaburi na
kuongeza
“Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi
wameshafungua jicho wanaona halmashauri zinaweza kujiendesha na sisi tunaona
hivyo kwa hiyo halmashauri zisipoweza kujikwamua na serikali kuu itakaleta pesa
itafikia mahali halmashauri zikashindwa kujiendeleza ama zikafa ni lazima
ifikie wakati tujirekebishe kwasababu madeni ni makubwa na pesa hazitoshi kwani
halmashauri nyingi zinaanza kufanya mambo mapya na kuacha yale ya
zamani,”alisema Masaburi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilwa Ally Mtopa
alisema makusanyo katika halmashauri kama yakisimamiwa vizuri yanaweza kusaidia
kupunguza utegemezi toka serikali kuu na kuiacha miradi mikubwa kuungwa mkono
na serikali kuu.
Hata hivyo alisema kuwa endapo
serikali kuu itachelewa kupeleka fedha ama kutopeleka kabisa kuna hatari ya
kuzipelekea halmashauri za miji na manispaa nchini kufa.
“Makusanyo yakiwa vizuri ndani ya
halmashauri yanaweza kusaidia kupunguza kutegemea bajeti toka serikali kuu na
hivyo ile miradi mikubwa itabidi serikali kuu ituunge mkono tofauti na hapo
itabidi tusubiri kila kitu toka makao makuu na kama wakichelewesha ama kutoleta
kabisa halmashauri za miji na manispaa zinaweza kufa,”alisema Mtopa
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD