TANGAZO
MAJIRA
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, anatarajia kuchukua fomu leo
za kuomba kuwania urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA).
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu
Mkuu wa CHADEMA (Zanzibar), Salum Mwalimu, alisema Lowassa anatarajia kuchukua
fomu hizo makao makuu ya chama kuanzia saa tano, asubuhi.
Waziri wa JK ndani
Kwa mara ya kwanza katika historia ya siasa za Tanzania Waziri katika
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, Goodluck Ole Medeye, jana alionekana makao
makuu ya CHADEMA, akiwa amekaa meza kuu, wakati Mwalimu alipokuwa akitangaza
Lowassa kuchukua fomu.
Waandishi wa habari walipohoji kama naibu huyo waziri wa Serikali ya
Awamu ya Nne amejiunga na CHADEMA, hakukuwa na majibu yaliyotolewa rasmi zaidi
ya kuwataka waandishi wa habari wazidi kuvuta subira, kwani kambi inazidi kuongezeka.
Taarifa za mpasuko ndani ya CHADEMA
Mwalimu alipoulizwa tetesi za kuwepo kwa mpasuko ndani ya CHADEMA
kutokana na Katibu wa Chama hicho, Dkt. Wilbrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu, John
Mnyika na Mwanasheria wa chama, Tundu Lissu, kutoshiriki utambulisho wa
Lowassa, alisema viongozi hao walikuwa kwenye majukumu mengine ya kichama.
Alisema huo ni mwendelezo wa matukio ya ukomavu wa kisiasa ambao chama
hicho unapitia hasa katika wakati huu ambao nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu
na kuongeza kuwa kutakuwa na wengi ambao wanatarajia kujiunga na chama hicho.
"Haiwezekani kila tunapozungumza na waandishi wa
habari awepo kila kiongozi, viongozi wengine walikuwa kwenye majukumu
mengine," alisema na kuongeza kuwa; "Tukumbuke sasa hivi ni kipindi
cha uchaguzi hivyo viongozi wengine wanakuwa majimboni. Ndani ya chama hiki
hakuna mpasuko, kutokuwepo kwao ni mgawanyo wa madaraka."
Lissu atetea ujio wa Lowassa
Kwa upande wake, Lissu alikiri kuwa waliwahi kumtuhumu Lowassa kwa
ufisadi kutokana na mambo yaliyohusu masuala ya Richmond bungeni. Alisema
walimtaja Lowassa kwenye orodha ya mafisadi, lakini hiyo ilitokana na ripoti
iliyowekwa wazi bungeni, hivyo hakukuwa na la kuficha.
“Ni kweli tulimweka kwenye orodha ya mafisadi na hiyo
sio siri kwani suala hilo liliwekwa wazi bungeni, lakini mwenyewe amesema kuwa
alizuiwa na Rais asivunje mkataba wa Richmond,” alisema Lissu.
NIPASHE
Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai amehojiwa na Jeshi la Polisi
mkoani Dodoma kwa tuhuma za kumshambulia kwa fimbo na kumjeruhi mgombea
mwenzake katika mbio za kuwania ubunge wa Jimbo la Kongwa kwa tiketi ya CCM,
Dk. Joseph Chilongani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Dodoma, David Misime, aliiambia NIPASHE mjini Dodoma jana kuwa walilazimika
kumhoji Ndugai baada ya kupokea malalamiko kuhusiana na tukio hilo lililotokea
wilayani Kongwa juzi.
Inadaiwa kuwa Ndugai
alimpiga fimbo na kumjeruhi vibaya Chilongani wakati wagombea hao na wenzao
watano wanaowania kuteuliwa kuwa wagombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM
walipokuwa wakijinadi ili wapitishwe na wanachama wenzao jimboni humo.
"Tulipokea malalamiko,
tumemhoji Ndugai na kisha tukamuachia kwa dhamana... hivi sasa tunaendelea na
uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo," alisema Kamanda Misime na
kuongeza kuwa watatoa taarifa zaidi pindi uchunguzi ukikamilika.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Dk. Ezekiel Mpuya, alithibitisha vilevile kuwa Dk. Chilongani alipokewa
kwao juzi jioni kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na kwamba hadi kufikia
jana alikuwa bado akiendelea na matibatu.
"Anaendelea na matibabu
lakini hali yake inaendelea vizuri," alisema Dk. Mpuya.
MWANANCHI
Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza
kuhama CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema, wasomi na wachambuzi wa
masuala ya siasa wamesema pande hizo mbili zimefanya uamuzi mgumu ambao
utanufaisha kila upande.
Profesa wa Chuo Kikuu Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema
uamuzi huo wa Lowassa ambaye alitangaza kujiunga na Chadema na kufafanua kuwa
amejiunga na chama hicho kikuu cha upinzani kutekeleza azma yake ya kuwakomboa
Watanzania na kuendeleza safari ya matumaini ni uamuzi mgumu.
Alisema: “Lowassa amefanya uamuzi mgumu kutoka CCM lakini hata
wapinzani wamefanya uamuzi mgumu kumpokea.”
Alisema sababu kubwa ya Chadema
kukubali kumpokea Lowassa ambaye leo anatarajiwa kuchukua fomu kuwania urais,
wakati ilikuwa inamtuhumu kwa ufisadi inatokana na mwanasiasa huyo kuwa na watu
wengi wanaomuunga mkono, hali ambayo itaibua ushindani mpya katika siasa
nchini.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika
Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Malya alisema katika siasa kinachotazamwa
zaidi ni nafasi, na kwamba katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu.
“Ila ujio wa Lowassa Chadema lazima
utazamwe, ni lazima chama hiki (Chadema) kimtazame kiongozi huyo anakuja na
kitu gani? Pia, CCM nao hata kama hawatasema wazi, lakini kuondoka kwa Lowassa
kutawatikisa kidogo,” alisema.
HABARI LEO
WASOMI mbalimbali nchini
wamewatahadharisha wananchi kwa kusema nchi haijafikia wakati wa wanasiasa
kutaka kushinda uchaguzi kwa gharama yoyote, hata kama hawana misingi ya
utawala bora.
Wakitoa maoni yao
Dar es Salaam jana, wasomi hao kutoka taasisi za vyuo na zile za utafiti,
walisema pamoja na kwamba kuhama chama ni haki ya mtu na hakuna anayeweza
kuhoji, lakini wakahoji ni nini dhamira ya kuhama huko na kama kuna maslahi kwa
wananchi.
Akizungumzia
uamuzi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza kujiunga
rasmi na Umoja wa Vyama Vinne vya Upinzani (Ukawa) na kukihama chama tawala,
CCM, Mhadhiri Mwandamizi aliyebobea katika uchambuzi wa masuala ya siasa katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alihoji dhamira yake ni ipi.
“Kuhama chama ni haki
ya raia, hakuna anayehoji, lakini dhamira inayompeleka Ukawa ni nini, hivi mtu
aliyekuwa haramu kwao leo ni lulu, hapa ndio wasiwasi unaanza. Mwaka 2010
walimtumia Lowassa kama mtaji, mwaka 2015 wanamuona ni dhahabu, kuna uwalakini
hapa”, alisema Dk Bana.
RAIA MWEMA
Hivi Chadema
(achilia mbali CUF) inawezaje kusimama jukwaani na kumnadi urais (au hata kuwa
naye tu jukwaani) mtu ambaye yumo katika orodha yao ya mafisadi papa nchini?
Wataanzia wapi na wataficha wapi nyuso zao? Au labda ni kwa kuwa IQ ya
Watanzania ni ya kiwango cha chini, na ndiyo maana wanaamini watasahau ya jana
kuhusu mgombea urais huyo?
Hivi nani asiyejua ya kuwa Lowassa anahamia
Chadema si kwa sababu ya kukipenda chama hicho na sera zake, lakini ni kwa sababu
ya kuikomoa CCM iliyomtosa? Hivi kweli mtu anayeingia chama kulipa visasi au
kukikomoa chama chake cha zamani anaweza kuwa na faida yoyote kubwa na endelevu
kwa chama hicho alichohamia na kwa Watanzania kwa ujumla?
Tangu lini visasi
binafsi na kukomoana vikachukua nafasi ya mustakabali wa taifa? Vyovyote vile,
Chadema na Ukawa yao itabidi, kwenye kampeni ya urais waanze kwanza na
kumsafisha Lowassa (sijui kwa sabuni gani) ndipo waeleze sera zao kwa wapiga
kuwa. Itabidi kwanza wazifute hadharani kauli zote za nyuma ambazo ziko kwenye
kumbukumbu walizozitamka dhidi ya Lowassa kumhusisha na ufisadi, na ndipo
waanze kumnadi au hata kuhalalisha tu kuwa naye kwenye jukwaa wakati wa
kampeni.
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alipata kusema
ya kuwa mtu akishakuwa tu na tuhuma kubwa za ufisadi hafai kufikiriwa urais, na
naamini ni kwa hoja hiyo hiyo CCM iliamua kumtosa Lowassa hata bila ya
kufikisha jina lake kwenye vikao vya juu kabisa vya maamuzi – Kamati Kuu, NEC
na Mkutano Mkuu.
JAMBO LEO
SIKU moja baada ya Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa kutangaza rasmi kuondoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameibua mjadala mzito
kila kona ya nchi.
Lowassa alijiunga na chama hicho
kinachounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jijini Dar es Salaam juzi huku
akisema CCM siyo baba wala mama yake, hivyo alitangaza kukihama.
Vyama vingine vinavyounda umoja huo ni National League Democracy
(NLD) kinachoongozwa na, Dk. Emmanuel Makaidi, Chama cha Wananchi (CUF)
kinachoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba na NCCR-Mageuzi chini ya uongozi wa
James Mbatia.
Baadhi ya watu
wamepongeza uamuzi wa Lowassa kujiondoa CCM kwenda Chadema kwamba ni wa
kijasiri na utafungua milango kwa vigogo wa chama hicho waliokuwa na hofu
kuhama, huku wengine wakiuponda wakisema hautaweza kukiyumbisha chama hicho
tawala.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD