Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

WARATIBU ELIMU KATA WALIOSHINDWA KUSHIRIKI UMITASHUMTA H/MJI MASASI WATANGAZIWA KIHAMA

TANGAZO
Ofisa Elimu Msingi H/Mji Masasi Mzenga Twalibu
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Ofisa elimu msingi Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara Mzenga Twalibu amewajia juu waratibu elimu kata wawili wa Halmashauri hiyo huku akionesha wazi kuchukizwa na kitendo cha wanafunzi wa shule za msingi kutoka kwenye kata hizo kushindwa kushiriki kwenye kambi ya michezo ya Umitashumta kwa ngazi ya halmashauri hiyo.
Waratibu elimu kata ambao kata zao zimeshindwa kushiriki kwenye michezo hiyo iliyokuwa na lengo la kutafuta timu ya Halmashauri ya mji wa Masasi itakayoenda kushindana na Halmashauri zingine mkoani Mtwara ili kupata timu ya mkoa ni kutoka kwenye kata ya Sululu inayoongozwa na mwalimu Hussein Bwanali pamoja na kata ya Mwenge Mtapika iliyo chini ya mwalimu Alli Chipotela.
Pia ameweka wazi msimamo wake kwa viongozi hao wa elimu  kuwa atakayeshindwa kutoa maelezo ya kina ni kwa nini kata zao hazikushiriki mashindano hayo muhimu kwa wanafunzi basi atosita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu  ikiwa ni pamoja na kuwaondoa kwenye nafasi zao za uratibu.
Alitoa kauli hiyo jana mjini humo wakati anafunga mashindano ya umoja wa michezo na taaluma kwa shule za msingi Tanzania (Umitashumta) kwa ngazi ya Halmashauri hiyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule za msingi Masasi ambapo alisema kitendo kilichofanywa na waratibu hao ni utovu wa nidhamu kwa uongozi wa idara ya elimu msingi na kwamba hawapaswi kuachwa hivi hivi.
Alisema moja ya majukumu yao ni kuhakikisha suala la michezo kwenye kata zao linatekelezwa kikamilifu na kwamba kwa kushindwa kwao kutekeleza sera ya serikali kuhusu michezo ni dhahiri kuwa hawatoshi kuendelea kushika nyadhifa hizo za uongozi wa elimu kwa ngazi ya kata na kwamba wanapaswa kuwajibika kabla ya hatua kali zingine kufuata dhidi yao.
Kwa mujibu wa Mzenga alisema kuwa waratibu hao wameshindwa kuwajibika huku akionesha wazi kukerwa na majibu yao waliodai kuwa wameshindwa kuleta wanafunzi hao kwa kuwa hawana fedha za kumudu gharama za mashindano kitu ambacho amekiri kuwa hakina ukweli wowote kwa kuwa ofisi yake ilitoa agizo kuwa watumie fedha za ruzuku (Capitation) na pesa za elimu ya kujitegemea (EK).
“Haiingii akilini kwa viongozi wakubwa wa elimu kama hawa eti washindwe kuleta timu kutoka kwenye kata zao kwa madai eti hawana fedha…wakati ofisi yangu ilishatoa maagizo kuwa wawaambie walimu wakuu wa shule zote kwenye kata zao watumie fedha ya ruzuku inayoletwa na serikali pamoja na michango mingine mbona hawa wenzao wameweza? Huu ni uzembe na kamwe siwezi kuvumilia”.alisema Mzenga.
Alisema tayari ofisi yake imeshaandaa barua za wito kwa waratibu hao wanaotakiwa kuripoti ofisini kwake kwa ajili ya kutoa maelezo ya awali ni sababu gani hasa za msingi zilizowafanya washindwe kuleta timu za michezo kutoka kwenye kata zao huku wakijua wazi kuwa kila siku serikali imekuwa ikihimiza michezo mashuleni ili kupata timu bora za michezo ikiwemo timu ya Taifa.
Alisema sera ya elimu nchini inasisitiza michezo na kwamba kupitia michezo wanafunzi wanapata stadi mbalimbali za maisha ikiwemo upendo na umoja miongoni mwao hivyo kwa kitendo cha wanafunzi wa kata hizo mbili kutoshiriki michezo hiyo ni kuwakosesha moja ya haki yao ya msingi ya kucheza.
Aidha alisisitiza kuwa msimamo wake ni kuchukua hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wa elimu ya msingi ndani ya Halmashauri hiyo watakaoshindwa kuwajibika kwa yale maagizo yote muhimu yanayotolewa na idara yake huku akiwatangazia kihama kwa lengo la kuwafanya wafanye kazi iliyowaleta ya kuwahudumia wananchi.
Mwisho.

 MWANAFUNZI mwenye ulemavu wa ngozi Samson Charles (JAJA)  anayesoma shule ya msingi mchanganyiko Masasi Halmashauri ya Mji wa Masasi akisoma Ngonjera iliyoandaliwa na wanafunzi hao ikiwa ni moja ya burudani wakati wa kufunga mashindano ya Umitashumta hii leo shuleni hapo.
 MRATIBU elimu kata wa kata ya Marika Mwalimu Shabani Mkieti akipokea cheti cha ushindi kutoka kwa ofisa elimu msingi wa Halmashauri ya mji wa Masasi Twalibu Mzenga.
 MWALIMU mkuu wa shule ya Msingi Chipole Halmashauri ya Mji wa Masasi Haji Ligalawa akionesha cheti cha ushindi baada ya kukabidhiwa na mgeni rasmi wakati wa kufunga mashindano ya UMISHUMTA.
MRATIBU wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kwa ngazi ya Halmashauri ya mji wa Masasi kwa mwaka 2015 Mwalimu Jerry Idrissa Njilinji wa shule ya msingi Masasi akisoma majina ya wanafunzi waliochaguliwa kuunda timu ya Halmashauri ya mji wa Masasi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top