TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Ruangwa.
WILAYA ya Ruangwa mkoani
Lindi imepokea mgao wa mahindi ya msaada kiasi cha tani 100 kutoka ghala kuu
la kuhifadhi chakula la Taifa (NFRA) jijini Dar es salaam kwa lengo la kugawa
kwa wananchi ambao katika msimu wa mwaka 2014/2015 wameathirika na ukame
uliosababisha mazao kukauka.
Taarifa hiyo imetolewa
na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Nicholaus Kombe wakati anatoa
taarifa ya mahitaji ya chakula na mgao wa chakula uliopokelewa kwa baraza la
madiwani wa Halmashauri hiyo lilioketi kwa ajili ya kujadili na kupitisha
taarifa mbalimbali za kamati za madiwani wa Halmashauri hiyo.
Alisema katika msimu wa
mwaka 2014/2015 wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ni miongoni mwa wilaya nchini
zilizoathirika na ukame uliosababisha mazao kunyauka na kukauka kwa kiwango
kikubwa mazingira yaliyopelekea kusababisha malengo ya uzalishaji yaliyopangwa
kutofikiwa.
Alisema baada ya
tathimini ya kina iliyofanywa na kamati ya maafa ya wilaya ikiongozwa na mkuu
wa wilaya hiyo Mariamu Mtima ilibainika kuwa wilaya ya Ruangwa ina upungufu
mkubwa wa chakula cha wanga na protini ambapo wilaya ilituma maombi ya chakula
cha msaada kiasi cha tani 1179 kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi
huyo wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa alisema wilaya imeletewa mgao wa
mahindi ya msaada kiasi cha tani 100 ambapo tani 90 zitauzwa kwa bei nafuu ya
shilingi 50 kwa kilo na tani 10 zitagawiwa bure kwa kaya zisizo na uwezo.
Alisema serikali imetuma
kiasi cha shilingi milioni 4,605,000 kwa ajili ya kuwezesha zoezi la
usafirishaji na usambazaji wa mahindi hayo ya msaada kutoka ghala kuu la kuhifadhia
chakula cha Taifa (NFRA) ili kiweze kuwafikia kwa wakati wananchi husika.
Alisema kutokana na mgao
huo wa mahindi ulioletwa na serikali kushindwa kukidhi mahitaji ya chakula
yaliyopo kwa sasa kamati ya maafa ya wilaya ya Ruangwa imeagiza kugawa mahindi
hayo katika vijiji vinane ikiwemo
Nanganga,Narungombe,Chunyu,Namichiga,Matambarare,Chibula,Mandawa pamoja na
Nambilanje.
Kombe alisema kuwa
kamati ya maafa imeshauri kwa awamu hiyo ya kwanza mgao uende kwa maeneo
yaliyoathirika sana yakiwemo vijiji hivyo na kwamba tayari wametuma maombi
mengine kwa serikali ili ione namna itakavyosaidi kukabiliana na tatizo la njaa
linaloweza kutokea.
Alisema kazi ya
usafirishaji na usambazaji wa mahindi hayo ya msaada inaendelea vizuri katika
vijiji vilivyoapangwa huku akitoa onyo kali kwa maofisa watendaji wa kata na
vijiji watakaojihusisha na udanganyifu wowote katika ugawaji wa chakula hicho.
Alisema ili kuhakikisha
wananchi wote walioathirika wanapata chakula cha kukidhi mahitaji hayo ya
msingi serikali imetoa kibali kwa wafanyabiashara kwenda kununua mahindi kutoka
ghala kuu la Taifa la hifadhi ya chakula (NFRA) na kuyaleta kwa wananchi na
kuyauza kwa bei nafuu bei ambayo itaelekezwa na serikali.
Alisema maeneo ambayo
yatapewa kipaombele ni yale ambayo hayakupata chakula hicho cha msaada kwa
awamu ya kwanza na kwamba serikali ya wilaya inatarajia kutoa maelekezo kwa
wafanyabiashara waliopewa vibali na serikali ni maeneo gani yanapaswa
kupelekewa msaada huo wa chakula.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD