Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

61,267 WAANDIKISHWA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA HALMASHAURI YA MJI WA MASASI

TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Ruangwa.
HALMASHAURI ya mji wa Masasi mkoani Mtwara imefanikiwa kuvuka lengo la uandikishaji kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuandikisha jumla ya watu 61,267 sawa na asilimia 111.38 ambapo lengo lilikuwa ni kuandikisha watu 55,007.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Masasi Fortunatus Kagoro wakati wa kikao cha kamati ya fedha ya Halmashauri hiyo na kwamba lengo limevuka kwa asilimia 11.38 ya makadirio kwa kata zote 14.
Alisema zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lilianza Aprili 24 mwaka huu na kumalizika mei 24 huku likidumu kwa  muda wa siku 28 ndani ya siku saba kwa  kila kanda kama ilivyoelekezwa na tume ya Taifa ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Kagoro alisema kutokana na takwimu hizo ni dhahiri kuwa zoezi hilo la uandikishaji wilayani humo limevuka lengo ambapo hakusita kuwapongeza maofisa waandikishaji pamoja na  wataalamu wa mashine za BVR kwa moyo waliouonesha katika kipindi chote cha zoezi hilo.
Akizungumzia kuhusu changamoto zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo alisema kulikuwa na baadhi ya changamoto ikiwemo baadhi ya wananchi kujiandikisha kwenye kanda ambazo tayari zilishaanza zoezi hilo kwa mujibu wa ratiba.
Alisema changamoto zingine ni pamoja na kuharibika kwa BVR kits pamoja na upungufu wa fedha za mafuta kwa ajili ya kutatua matatizo ya hitilafu za mashine zilizokuwa zinatokea wakati wa zoezi zima la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
 Alisema kwa ujumla zoezi hilo lilienda vizuri licha ya kuwepo kwa changamoto hizo ambazo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka tume ya Taifa ya uchaguzi walifanikiwa kufanikisha mchakato huo muhimu kwa watanzania hasa katika kipindi hiki kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais,wabunge na madiwani.
Mwisho.


TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top