TANGAZO
Na Christopher Lilai,Nachingwea.
BAADHI ya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini
wilayani Nachingwea mkoani Lindi kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii
nchini Tasaf wameomba kiwango cha fedha ya ruzuku
zinazotolewa kiongezwe na kupanua wigo wa idadi ya wanufaika ili jamii zote zilizo
maskini ziweze kufikiwa.
Wakizungumza na Blog ya Mtazamo mpya jana baadhi ya wanufaika wa mpango huo
wa Tasaf katika wilaya ya Nachingwea hivi karibuni ambao miongoni wao
wameweza kujijengea nyumba,kuanzisha ufugaji wa mifugo mbalimbali kupitia kiasi
kidogo wanachopatiwa walibainisha wazi kuwa mpango huo ni ukombozi kwao.
Felista Chinguile (78) mkazi wa kijiji cha Kihuwe ambaye ni mjane
licha ya kufanikiwa kujenga nyumba yake ya matofali ya kuchoma na
kuweka saruji kwenye sakafu na kuanza kufuga nguruwe alisema kiwango cha
fedha kinachotolewa ni kidogo na kuomba kiwango hicho kiongezwe.
Alisema iwapo kiwango hicho kitaongezwa kitawafanya wanufaika kuanzisha miradi ambayo
itawaletea tija na kuboresha hali yao ya maisha hivyo kufanya lengo la
kuanzisha mpango huo kufikiwa.
Kwa upande wake Filipo Nasi
mkazi wa kijiji cha Nangoe, ambaye ni mnufaika wa mpango huo alisema kupitia
mpango huo ameweza kujenga nyumba ya matofali na kuezeka kwa nyasi ambapo kabla
ya kupatiwa kiasi hicho alikuwa anaishi kwenye nyumba mbovu ambayo ilikuwa
inahatarisha maisha yake na familia yake yenye watoto watatu.
Naye mjumbe wa kamati ya usimamizi wa mpango huo wa kijiji cha
Nangoe,Aisha Makopa alikiri wazi kuwa mpango huo ni ukombozi kwa kaya maskini
na kwamba ni vyema ukaongeza wigo kwa kuzifikia kaya nyingi zaidi ambazo
hazijafikiwa na mpango huo.
“Wanaohitaji kunufaika na mpango huu ni wengi lakini kwa
sasa wanaonufaika ni wachache hivyo ninaomba upanuliwe na kuwafikia walio
wengi”. alisema Aisha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nangoe,Rojas Mwanjise alisema katika kijiji chake kaya zipatazo 64
zinanufaika na mpango huo ambazo kwa sasa zinaweza kupata milo
mitatu,kupata matibabu kupitia mfuko wa afya ya jamii(CHF) baada ya kuchangia
kupitia kiasi kidogo cha fedha wanachokipata.
Alisema kuwa bado idadi kubwa haijafikiwa jambo ambalo
linasababisha migogoro kati ya ndugu za watu hao na uongozi wa kijiji na kuomba
utambuzi wa kaya zingine ufanyike ili kuwabaini walioachwa na kuwaingiza ili
nao wanufaike.
“Naomba utambuzi wa kaya maskini ufanyike tena kwani zipo kaya
nyingi ambazo hazikutambuliwa awali ili kuepusha migogoro ambayo sisi viongozi
tunakutana nayo”.alisema Mwanjise.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD