TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
WANACHAMA wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kata ya Mbuyuni, jimbo la Lulindi wilayani Masasi
wamechangia fedha kiasi cha shilingi 100,000 na kumpa mbunge wao wa sasa wa
jimbo hilo Jerome Bwanausi ili akachukue fomu ya kuomba ridhaa kutoka ndani ya
chama hicho aweze kuendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka mitano ijayo.
Tukio hilo la
aina yake kuwahi kutokea kwa siku za hivi karibuni jimboni humo lilihudhuriwa
na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa madhehebu ya dini,viongozi wa kimila
(Mamwenye),viongozi wa serikali pamoja na viongozi mbalimbali wa chama cha
mapinduzi wakiwemo wajumbe wa kamati ya siasa ya kata ya Mbuyuni.
Akikabidhi
mchango huo jana kwa mbunge huyo wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika
kijiji cha Mbuyuni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa kata ya Mbuyuni Yohana
Mpondomoka alisema wameridhishwa na utendaji wa mbunge huyo na kwamba hawaoni
mwanachama mwingine kwa sasa ndani ya chama hicho ambaye anaweza kuongoza jimbo
hilo.
Alisema wakati
mbunge huyo anaingia madarakani mwaka 2010 vijiji vya kata ya Mbuyuni vikiwemo
Matogoro,Mdibwa,Mihungo,Mpulima,Majembendago pamoja na Mitonji vilikuwa havina
huduma ya maji safi na salama kwa takribani miaka kumi lakini baada ya Bwanausi
kupewa dhamana hiyo kwa sasa vijiji vinne kati ya hivyo vinapata maji safi na
salama.
Alisema lengo
lao ni kuona mbunge wao anarudi madarakani katika kipindi kingine cha miaka
mitano ili aweze kumalizia ahadi zake na miradi ya maendeleo aliyoanza
kuitekeleza ndani ya jimbo la Lulindi ambapo wameuomba uongozi wa CCM wilaya ya
Masasi kutosimamisha mgombea mwingine ndani ya chama ili mbunge huyo aweze
kupita bila kupingwa.
“Tungekuwa na
uwezo zaidi ya huu tungeweza kukuchangia fedha ya mafuta kwenye gari yako siku
utakayoenda kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge kwenye jimbo la Lulindi…na
hii yote tunafanya kwa kuwa tuna imani kubwa na wewe uendelee kutuongoza na
ikiwezekana uwe mbunge wetu wa maisha kwa kuwa umekuwa ukijali na kutekeleza
shida za wananchi wa jimbo lako”.alisema Mpondomoka.
Kwa upande wake
mbunge wa jimbo la Lulindi (CCM) Jerome Bwanausi aliwashukuru wanachama hao
huku akiwaahidi kuwa fedha waliyoitafuta kwa nguvu zao na kuamua kuchangishana
itaenda kufanya kazi iliyokusudiwa pale wakati utakapofika ili waweze kuendelea
na safari yao ya maendeleo jimboni humo kwa kasi mpya zaidi.
Alisema katika
kipindi chake cha uongozi ndani ya miaka mitano amefanikiwa kuboresha huduma
mbalimbali za jamii zikiwemo huduma za afya,maji,miundo mbinu ya barabara
pamoja na sekta ya nishati huku akiwaahidi kuwa endapo watamrudisha madarakani
atakamilisha miradi yote ya maendeleo iliyobakia jimboni humo.
Kwa muijbu wa
mbunge huyo alisema kwa sasa vijiji vingi vilivyopo kwenye jimbo hilo vinapata
huduma ya maji safi salama kutokana na kukamilika kwa mradi wa maji uliopo
kwenye chanzo cha Lulindi na kwamba kwa
vijiji vilivyobaki vitapata huduma hiyo wakati wowote kuanzia sasa kwa kuwa
wakandarasi wanaendelea na ukarabati wa miundo mbinu iliyokuwa imeharibika ya
mradi huo ili wananchi wote waweze kupata huduma hiyo muhimu.
Akizungumzia
kuhusu sekta ya afya alisema tayari fedha imeshatengwa kwa ajili ya kuboresha
zahanati ya Kijiji cha Mbuyuni kuwa kituo cha afya ili kiweze kutoa huduma kwa
wananchi wa eneo hilo huku akiahidi kutafuta fedha kwa ajili ya uwekaji wa changarawe
pamoja ujenzi wa makalavati kwa barabara
ya Mbuyuni-Mtakuja-hadi Lulindi pamoja na barabara inayotoka kijiji cha Mitonji-Umati
hadi Utimbe ili ziweze kupitika kwa wakati wote wa msimu.
Kuhusu kilimo
alisema lengo lake na nia yake ya dhati endapo wana CCM hao watampa dhamana ya
kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo atakuja na kampeni kabambe kuhusu
uanzishwaji wa kilimo cha zao la alizeti
ili liweze kuwa zao mbadala la korosho ambalo kwa siku za hivi karibuni
limekumbwa na changamoto nyingi zikiwemo za kushuka kwa bei.
Mwisho.
MBUNGE wa Jimbo la Masasi Jerome Bwanausi akitoa shukrani baada ya kukabidhiwa fedha shilingi 100,000 kutoka kwa wana CCM wa kata ya Mbuyuni Jimbo la Lulindi wilayani Masasi.
MWENYEKITI wa Viongozi wa Kimila (Mamwenye) Chimombo Bakari wakati anazungumza kwenye hafla fupi ya kutoa fedha kwa mbunge wa jimbo la Lulindi Jerome Bwanausi ili aweze kuchukua fomu za kugombea nafasi ya ubunge jimboni humo.
MKE wa Mbunge wa Jimbo la Lulindi Jerome Bwanausi akitoa shukrani kwa wanachama na viongozi wa CCM wa kata ya Mbuyuni baada ya mume wake kukabidhiwa fedha Tsh.100,000/= ili akachukue fomu ya kugombea ubunge jimbo la Lulindi.
Jerome Bwanausi Mbunge wa Jimbo la Lulindi akionesha fedha alizopewa na wanachama wa CCM wa kata ya Mbuyuni Jimbo la Lulindi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD