Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

TAKUKURU MASASI YAMBURUZA MAHAKAMANI MTENDAJI WA KIJIJI KWA MATUMIZI MABAYA YA NYARAKA ZA SERIKALI

TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Masasi imewafikisha mahakamani watuhumiwa wawili akiwemo ofisa mtendaji wa kijiji cha Mbuyuni na wakala wa usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa tuhuma za wizi wa pembejeo hizo.
Watuhumiwa waliofikishwa katika mahakama ya wilaya ya Masasi kujibu mashitaka 204 yanayowakabili ni Hamza Idd ambaye ni ofisa mtendaji wa kijiji cha Mbuyuni Halmashauri ya wilaya ya Masasi pamoja na Rais Mahenge aliyekuwa wakala wa usambazaji wa pembejeo hizo ingawa wakati mashtaka hayo yanasomwa hakuwepo mahakami hapo.
Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Masasi Halfani Ulaya,mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Cecilia Nshiku alisema watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti mnamo mwaka 2011 walitenda makosa 204 yakiwemo ya udanganyifu na matumizi mabaya ya nyaraka za serikali kwa lengo la kujipatia fedha kinyume na taratibu za nchi.
Nshiku aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa namba moja ambaye ni ofisa mtendaji wa kijiji cha Mbuyuni Hamza Idd alitumia nyaraka za serikali kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake kinyume na kifungu cha 22 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema mshtakiwa kwa nyakati tofauti kati ya tarehe 11,12,13,14,15 na 16 mwaka 2011 alitumia vocha mbalimbali za pembejeo za kilimo zenye maelezo ya uongo zikiwa na namba tofauti ambazo zilionesha kuwa wakulima wa kijiji hicho cha Mbuyuni kupokea pembejeo hizo za kilimo.
Alidai kuwa mshtakiwa alimdanganya mwajiri wake ambaye ni Halmashauri ya wilaya ya Masasi kwa kuandika namba hewa za vocha zilizokuwa na maelezo ya uongo huku wakulima hao wakishindwa kupata pembejeo hizo kutokana na ofisa huyo wa serikali kwa ushirikiano na wakala wa pembejeo hizo wakidaiwa kuuza kwa wafanyabiashara.
Pembejeo zinazodaiwa kuuzwa na ofisa mtendaji huyo akishirikiana na wakala wa pembejeo hizo ambaye bado anatafutwa na jeshi la polisi nchini ni pamoja na mbegu za mahindi,mbolea aina za urea na dup huku baadhi ya wakulima waliotajwa kwenye shitaka hilo kuhusishwa kupewa pembejeo hizo ni pamoja na Mussa Likonde,Hassan Mkito,Allen Mtwelo na Jemsi Jumapili.
Hata hivyo mshtakiwa alikana mashtaka yote 204 na kwamba kwa kuwa kesi hiyo inatajwa kwa mara ya kwanza hakutakiwa kujibu chochote.
Baada ya hakimu mkazi  wa mahakama ya wilaya ya Masasi Halfani Ulaya kusikiliza upande wa mashtaka alisema dhamana iko wazi kwa mtuhumiwa kwa masharti ya kudhaminiwa na watu wawili mmoja kati yao ni lazima awe mtumishi wa serikali mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri wake na kivuli cha kitambulisho cha kazi.
Alidai kuwa mdhamini wa pili ni mtu yeyote mwenye mali isiyohamishika ikiwa ni pamoja nna shamba au nyumba vyote vikiwa na  thamani ya shilingi milioni 50 na kwamba anapaswa kuwasilisha hati ya nyumba au shamba akiwa na barua kutoka kwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji.
Mshtakiwa alifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana na yuko nje kwa dhamana ambapo kesi hiyo itatajwa tena juni 29, mwaka huu.
Mwisho.


TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top