TANGAZO
Na
Clarence Chilumba, Masasi.
MWENYEKITI wa Halmashauri ya
mji wa Masasi Andrew Mtumusha amewataka wazazi pamoja na jamii kwa ujumla kutambua
kuwa suala la ulinzi na usalama kwa watoto si la serikali
pekee na kwamba vitendo vya kikatili na unyanyasaji wanavyofanyiwa watoto hapa
nchini na baadhi
ya watu havipaswi kuachwa vikiendelea
Kwenye jamii.
Pia ametoa onyo kali kwa baadhi
ya watu wanaowapa ujauzito wanafunzi wanaosoma shule za sekondari ndani ya
Halmashauri hiyo ambayo kwa mujibu wa takwimu za wataalamu wa elimu wa
halmashauri hiyo zinaeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2014/2015 jumla ya
wanafunzi 10 wa kike waliacha masomo kutokana na ujauzito.
Aliyasema hayo leo wakati wa
kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambapo kwa Halmashauri ya mji
wa Masasi yalifanyika katika kijiji cha Moroko, kata ta Temeke ambapo alisema
jamii inapaswa kukemea vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa watoto ikiwemo mimba
za utotoni, udhalilishaji wa kijinsia na ndoa za utotoni.
Alisema serikali pia iweke
msingi utakaolinda haki za watoto nchini katika kufikia na kufaidi huduma za
jamii ikiwa ni pamoja na elimu yenye kuwawezesha kudai, kutetea, kulinda haki
zao pamoja na uwezo wa kuwafichua baadhi ya watu wanaowafanyia vitendo vya ukatili
wa kijinsia ili sheria ichukue mkondo wake.
Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa
kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu , na umuhimu wa mtoto duniani ambapo maadhimisho hayo hufanyika kila juni 16 tangu
ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya umoja wa Afrika huku
suala la elimu kwa watoto ndio imekuwa mada kuu kwa nchi nyingi katika kumuinua
mtoto wa Afrika.
Maadhimisho hayo hufanyika kwa lengo la
kukumbuka mauaji ya maelfu ya watoto wanafunzi waliokuwa wakidai haki zao ikiwemo elimu kutoka kwa
utawala wa kidhalimu wa makaburu yaliyotokea katika kitongoji cha Soweto nchini
Afrika ya Kusini mnamo mwaka 1976.
Kwa upande wa Halmashauri ya mji wa Masasi
maadhimisho hayo yalianza kwa maandamano yaliyoandaliwa na shirika lisilo la
kiserikali la KIMAS kwa kushirikiana na shirika la terre des homes la nchini uholanzi pamoja na wadau wengine kwa lengo la kuhamasisha Serikali
na mashirika binafsi na yale ya kimataifa kusaidia watoto wa mitaani na wale
yatima walioachwa na wazazi wao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa
Ukimwi.
Kwa upande wake Ofisa maendeleo ya jamii wa
halmashauri ya mji wa Masasi Zuena Ungele alisema ili kupambana na vitendo vya
kikatili dhidi ya watoto idara yake kwa kushirikiana na shirika la KIMAS
limefanikiwa kuanzisha klabu kumi za watoto na kwamba kati ya hizo tano
zinaundwa na wanafunzi wa shule za sekondari huku tano zingine zikiundwa na
wanafunzi wa shule za msingi.
Alisema lengo la kuanzishwa kwa klabu hizo
mashuleni ni kufundisha watoto namna wanavyoweza kukabiliana na vitendo vyote
vya kikatili dhidi yao kwa kutoa taarifa kwa wazazi wao na kwa vyombo vya
ulinzi na usalama pale wanapokumbwa na kadhia hiyo ya unyanyasaji.
Kwa mujibu wa Ungele alisema
tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa masuala ya haki za watoto zinaonesha
kuwa sehemu kubwa ya vitendo vya kikatili hufanyika majumbani, shuleni, kwenye
nyumba za ibada pamoja na maeneo yenye migodi hali inayopelekea kuwepo kwa kundi
kubwa la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi.
Maadhimisho
hayo ya siku ya mtoto wa Afrika kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu inayosema
tokomeza mimba na ndoa za utotoni kwa pamoja tunaweza huku ripoti
ya mwaka huu ya Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, (UNICEF) inaeleza kuwa maelfu ya watoto barani Afrika wanateswa, kutumiwa vibaya pamoja na kufanyiwa
ukatili.
Mwisho
DIWANI wa Kata ya Temeke ambaye ndie mwenyeji wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika Selemani Nivako akizungumza wakati wa maadhimisho hayo hii leo.
OFISA maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya mji wa Masasi Zuena Ungele akitoa historia fupi ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya shule ya msingi Moroko kata ya Temeke.
MWANAFUNZI Vaileth Raphael wa shule ya msingi Mtakuja anayesoma darasa la saba ambaye alikuwa spika wa Bunge la watoto katika maadhimisho hayo ya siku ya mtoto wa Afrika.
WANAFUNZI wa shule ya msingi Mtakuja Halmashauri ya mji wa Masasi ambao walikuwa waheshimiwa wabunge wa Bunge la watoto ambao kwa nafasi zao walijaribu kuuliza maswali kupititia wizara mbalimbali ambazo zilikuwepo na hatimaye kupatiwa majibu ya kina.
WANAFUNZI wa shule ya Sekondari wakiigiza igizo linaloitwa HOUSE GIRL wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika lililokuwa na lengo la kutoa fundisho kwa wazazi wenye tabia ya kuwapeleka watoto wao kwenye kazi za ndani badala ya kuwapa elimu.
KIKUNDI cha Sarakasi kikifanya onesho katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya shule ya msingi Moroko kata ya Temeke halmashauri ya mji wa Masasi.
MWENYEKITI wa Halmashauri ya mji wa Masasi Andrew Mtumusha akihutubia mamia ya wakazi wa kata ya Temeke waliojitokeza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika kijiji cha Moroko.
WANAFUNZI wa shule ya msingi Mtakuja wakicheza na kuimba kwaya wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika hii leo.
BAADHI ya Mabango yaliyokuwepo kwenye maadhimisho ya kilele cha siku ya mtoto wa Afrika yakibeba ujumbe na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo Tokomeza mimba za utotoni na ndoa za utotoni kwa pamoja tunaweza.
BAADHI ya watoto waliojitokeza kwenye siku yao ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.
LICHA ya maadhimisho hayo lakini pia hii leo kumezinduliwa klabu za kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
WANAFUNZI wa shule ya sekondari wakiwa wamebeba bango lililokuwa na maneno ya kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD