Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

SOKO KUU LA WAFANYABIASHARA WA SAMAKI NA MBOGAMBOGA "MKUTI-MASASI" LATEKETEA KWA MOTO.

TANGAZO
Hali ilivyokuwa katika eneo la soko la Mkuti baada ya kuteketea kwa moto.

Na Clarence Chilumba,Masasi.
SOKO kuu la Wafanyabiashara wa Samaki,dagaa na Mbogamboga maarufu Mkuti  lililopo katikati ya Mji wa Masasi limeteketea lote kwa moto  huku baadhi ya  maduka yanayolizunguka soko hilo nayo yakiteketea kwa moto huo na kwamba hadi sasa  chanzo cha moto huo  kikiwa bado hakijafahamika.
Tukio hilo la kusikitisha na lililoacha simanzi kubwa kwa wafanyabiashara wa mji wa Masasi pamoja na wananchi kwa ujumla limetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa 4:30 usiku ambapo moto mkubwa ambao chanzo chake hakifahamiki hadi sasa ulilipuka kwa nguvu katikati ya soko hilo na kuteketeza kabisa bidhaa za wafanyabiashara hao.
Aidha katika tukio hilo la usiku vijana ambao walikuja sokoni hapo kwa minajiri ya kusaidia zoezi la uokoaji walianza kuvunja na kuvamia baadhi ya maduka yaliyokuwa yamezunguka soko hilo na hatimaye kufanikiwa kupora vitu mbalimbali vikiwemo magodoro,baiskeli,cherehani pamoja na bidhaa zingine za madukani.
Kufuatia msako mkubwa uliofanywa na jeshi la polisi wilaya ya Masasi likiongozwa na mkuu wa jeshi hilo wilayani hapa Azaria Makubi tayari vijana 19 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kukutwa na baadhi ya bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara hao huku upelelezi wa nyumba kwa nyumba ukiwa bado unaendelea.

BAADHI ya Bidhaa zilizookolewa kwenye maduka ya wafanyabiashara hao wa soko kuu la Mkuti wengine wakipakia kwenye magari kupeleka majumbani mwao.
Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo la tukio mapema hii leo mkuu wa wilaya ya Masasi Bernald Nduta alisema ni pigo kubwa kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kwa kuwa soko hilo ni miongoni mwa masoko makubwa mkoani Mtwara linalotoa huduma hata kwa wanannchi wa wilaya jirani za Nanyumbu,Newala,Ruangwa,Nachingwea,Tandahimba na Liwale.
Alisema serikali ya wilaya ya Masasi iko pamoja na waathirika wote wa moto huo na kwamba tayari amewaagiza wataalamu wake wa tathimini wa Halmshauri ya mji wa Masasi kuanza kufanya tathimini za awali ili kubaini ni hasara ya kiasi gani ambayo wafanyabiashara hao wamepata kutokana na janga hilo.
Alisema kwa sasa wafanyabiashara hao waoneshe moyo wa utulivu katika kipindi hiki kigumu kwao huku serikali ya wilaya kwa kushirikiana na kitengo cha maafa kutoka ofisi ya waziri mkuu kikiangalia namna ya kukabiliana na suala hilo.
 Hali ilivyokuwa jana Usiku majira ya saa 4:30 wakati soko la Mkuti linateketea kwa moto ambao hadi sasa chanzo chake hakijafahamika.
Alisema kwa sasa wafanyabiashara hao waoneshe moyo wa utulivu katika kipindi hiki kigumu kwao huku serikali ya wilaya kwa kushirikiana na kitengo cha maafa kutoka ofisi ya waziri mkuu kikiangalia namna ya kukabiliana na suala hilo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya ya Masasi alisema ni vigumu kuamini lakini imetokea huku akiwaomba wafanyabiashara wa wilaya jirani kusaidia kuleta chakula kwa ajili ya kuuza kwa kuzingatia kwa sasa ni kipindi cha mfungo wa Ramadhani ambapo pia ametoa wito kwa wafanyabiashara hao wasitumie mwanya huo kupandisha bidhaa bei.

 DIWANI wa kata ya Mkuti Halmashauri ya mji wa Masasi Mahfoudh S. Ahmed akitoa maelezo kwa mkuu wa wilaya ya Masasi Bernald Nduta alipotembelea eneo la soko hilo kwa lengo la kujionea uharibifu wa mali uliotokea.
“Nawapa pole sana wafanyabiashara mliokusanyika hapa asubuhi hii kunisikiliza…najua ni kweli inauma kupoteza mali na fedha kwa mtindo wa aina hii nawaomba muendelee kuwa na moyo wa subira ambao tangu tukio hili lilipotokea jana usiku mmekuwa nao,serikali tuko pamoja na nyinyi katika hili”.alisema mkuu wa wilaya ya Masasi.
 MKUU wa wilaya ya Masasi Bernald Nduta akiongea na wafanyabishara kwenye eneo la soko la Mkuti lililoteketea kwa moto 
 BAADHI ya wananchi wakishuhudia uharibifu wa mali uliojitokeza kwenye soko hilo la Mkuti baada ya kuteketea kwa moto jana usiku.

"Katika hatua nyingine tayari kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Masasi ikiongozwa na mkuu wa wilaya imefanya kikao cha dharura cha kujadili namna watakavyofanya na kwamba tayari kamati zimeundwa za kufanya tathimini za awali."
 WANANCHI wakiwa kwenye eneo la soko kuu la Mkuti kushuhudia kilichokuwa kikiendelea asubuhi ya leo
 Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Masasi Fortunatus Kagoro alisema kwa sasa halmashauri inajipanga katika kuona ni namna gani wanaweza kufanya ili kunusuru wananchi ambao tegemeo lao kubwa kwa bidhaa ni soko hilo la Mkuti.
Alisema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni kukosa kwa vifaa vya kuzimia moto kutoka kwenye kitengo kinachojitegemea cha zimamoto ambao kwa siku za hivi karibuni pampu ya kurushia maji wakati wa uzimaji wa moto imeharibika na gari hilo la zimamoto kushindwa kufanya kazi zake zilizokusudiwa.
Alisema tayari wao kama Halmashauri walishawasiliana na mkuu wa jeshi la Zimamoto mkoani Mtwara ili kutatua tatzo na ni matumaini yake kuwa mapema gari hilo la zimamoto litakuwa katika hali ya ubora unaopaswa kuwepo huku akiwaomba wafanyabishara hao kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa kufanya tathimini ili kuepuka watu ambao si wafanyabiashara kujiingiza kwenye tathimini hiyo.
Nae mkuu wa jeshi la polisi wilaya ya Masasi Azaria Makubi alisema jeshi lake limejipanga katika kukabiliana na watu wote ambao wanataka kutumia mwanya huo ili kujipatia mali isivyo halali na kwamba jeshi lake litafanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kubaini bidhaa nyingi ambazo zimeibiwa jana usiku wakati wa tukio hilo.
Makubi alisema wananchi pia wana wajibu wa kutoa taarifa kwa jeshi hilo pale watakapobaini mtu yeyote katika kipindi hiki kuwa na bidhaa za madukani kinyume na utaratibu ili waweze kuwafikisha polisi na baadae kuwafikisha mahakamani.
MKUU wa Jeshi la Polisi wilaya ya Masasi Azaria Makubi akizungumza na wafanyabishara eneo la soko kuu la Mkuti ambalo limeteketea kwa moto.

Mussa Mnalala ni katibu wa soko kuu la bidhaa la Mkuti ambalo limeteketea lote kwa moto ambaye kwa upande wake alisema hadi sasa hawajuia chanzo cha moto huo ni nini na kwamba hata walipowauliza walinzi wanaolinda sokoni hapo nao pia waneshindwa kuwapa majibu kuhusu chanzo cha moto huo.
Alisema kwa sasa wanachofanya ni kumalizia suala la uokoaji wa vifaa vya ujenzi zikiwemo baadhi ya bati na matofali ambapo baadae jioni hii ya leo watafanya kikao cha uongozi ili kuangalia ni kiasi gani cha hasara kimepatikana kutokana na moto huo.
Alisema mabanda yote ya biashara za mama lishe,mbogamboga,dagaa,matunda,viungo,vyakula pamoja na mabanda ya samaki yote kwa sasa yaneteketea kabisa kwa moto na hakuna kitu chochote kilichopatikana kama mabaki kutoka kwenye soko hilo.

Kwa mujibu wa Mnalala aliiomba serikali kufanya haraka tathimini ya hasara ya soko hilo ili nao waweze kufahamu hatima ya maisha yao baada ya uharibifu huo ambao amekiri kuwa vijana weng wako katika wakati mgumu kutokana na mikopo ya biashara waliyoikopa kutoka benki na taasisi zingine za fedha.



Nao baadhi ya wafanyabiashara ambao mabanda yao ya biashara yameteketea kwa moto na kwa wale ambao wamekuta mabanda yao yamevunjwa na watu wasiofahamika walisema hali ni mbaya kwao kwa sasa na hawajui cha kufanya ambapo wameiomba serikali kuwasaidia kwa kile itakachoweza.
Kwa sasa moto katika soko hilo la Mkuti umetulia ila kilichobaki ni kwa wafanyabishara wa madukaa ambao walifanikiwa kuokoa baadhi ya bidhaa kuzirudisha majumbani mwao huku jeshi la polisi likiwaamuru wananchi waondoke kwenye eneo hilo ili wafanyabishara waweze kufanya kikao cha tathimini.
Hadi sasa tayari viongozi mbalimbali wa serikali na chama wameshatembelea kwenye eneo hilo la tukio kwa kuwapa pole wafanyabiashara hao na wananchi kwa ujumla.

Mwisho.


TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top