TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
WAZIRI wa Maliasili
na utalii Lazaro Nyalandu amesema chama cha mapinduzi (CCM) ni chama pekee
nchini ambacho kimefanikiwa na kinaendelea kupanua wigo wa
demokrasia,kinachopendwa na chenye dira na mwelekeo huku akiwataka wana CCM
kote nchini kuwa tayari kwa ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu oktoba mwaka
huu.
Waziri Nyalandu ni
miongoni mwa wanachama wa chama hicho nchini waliotia nia ya kugombea nafasi ya
urais katika uchaguzi ujao,aliyasema hayo leo wakati anazungumza na viongozi
pamoja na wanachama wa chama cha mapinduzi wilayani Masasi waliojitokeza
kumdhamini.
Alisema hakuna tunu
bora nchini zaidi ya kuendeleza umoja,amani na mshikamano uliopo hivi sasa ndani ya chama
hicho huku akitoa wito kwa wagombea wenzake ndani ya chama kuacha kukitia madoa
chama na hata wao wenyewe kwani kwa sasa CCM inahitaji umoja.
Alisema wana CCM
nchini waondoe tofauti zao kwa kuwa ndio silaha pekee itakayoirudisha
madarakani ambapo pia aliwaasa watanzania kupinga vitendo vyote vya
kibaguzi,udini,ukabila na hata tofauti za rangi na kwamba endapo CCM kitampa
ridhaa ya kuwa mgombea wa urais atahakikisha vitendo hivyo vinabaki kuwa
historia.
Kwa mujibu wa
Nyalandu alisema amekuwa ndani ya chama cha mapinduzi kwa muda mrefu sasa na
kwamba kwa sasa mungu ameruhusu kizazi kingine kipate fursa ya kuongoza nchi
lengo likiwa ni kujenga uchumi imara kwa kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo
gesi,mafuta,milima pamoja na hifadhi za Taifa.
“Mimi na CCM
hatukukutana njiani kama ilivyo kwa wengine…nilizaliwa nikiwa mwana CCM tayari kwani
Baba yangu alikuwa ni mwenyekiti wa chama cha mapinduzi pale
kijijini kwetu kwa muda mrefu hivyo nakijua chama vizuri na ndio maana nimeamua
kujitokeza kuwania kuchaguliwa ndani ya chama changu ili niwe mgombea wa nafasi
ya urais”.alisema Nyalandu.
Kwa upande wake
mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Masasi Kazumari Malilo (Simba wa
Yuda) alisema watia nia wote wa chama hicho wapatao 38 hadi sasa wanapaswa
kuiga mfano wa Nyalandu ambaye amezungumzia mambo ya msingi ikiwemo umoja na
mshikamano ndani ya chama kitu ambacho ni tofauti na watia nia wengine.
Alisema wanachama wa
CCM si watu wanaopenda migogoro isiyo na maana ndani ya chama hicho na kwamba
ni vyema sasa wanapopita kutafuta wadhamini wasitoe ahadi nyingi ambazo wakati
mwingine hazitekelezeki ili kuondoa malumbano kwa wananchi ambao wengi wamekuwa
wakiamini sera za chama cha Mapinduzi.
Malilo alisema
Nyalandu anafaa kuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa namna
anavyozungumza masuala nyeti na ya msingi kwenye ziara zake za kutafuta
wadhamini kwani mara nyingi kauli zake ni za kukijenga chama tofauti na
wagombea wengine ambao wanaonekana kuwa na misimamo tofauti.
Kwa mujibu wa
mwenyekiti huyo wa CCM wilaya ya Masasi alisema wakati sasa umefika kwa
wanachama wa chama hicho kubadilika na kuwa kitu kimoja hasa katika kipindi
hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu baadae mwezi oktoba mwaka huu ili waweze
kuendelea kubaki madarakani waendeleea kuwaletea maendeleo watanzania.
“Nimekuwa nikifuatilia
sana hotuba zako kote unakopita kutafuta wadhamini… sjasikia ukiwasema vibaya
watia nia wenzako ndani ya chama au ukitoa ahadi nyingi na kuwa na makundi
mengi ya watu,hakika wewe ni mfano wa kuigwa ndani ya chama chetu binafsi na
wanachama wa CCM wilaya ya Masasi tunakuombea ushinde ili uipeperushe bendera
ya chama chetu”.alisema malilo huku akishangiliwa.
Alisema wilaya ya
Masasi ni miongoni mwa wilaya nchini ambazo zimetoa viongozi wengi wa ngazi za
juu kwenye serikali hii ya chama cha mapinduzi huku akimuhakikishia kuwa kwa
kufika kwake kuja kutafuta kudhaminiwa ni ishara tosha na yeye atakuwa ni
miongoni mwa wana CCM watakaochaguliwa kugombea nafasi ya urais.
Naye mjumbe wa
Halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi wilaya ya Masasi Ramadhani Pole alisema
anawashangaa watia nia wengine kutoka kwenye chama hicho ambao kila siku
wamekuwa wakikusanya watu ambao wengine si wana chama wa chama hicho huku
wengine wakienda mbali kwa kusema kuwa endapo hawatachaguliwa watajiondoa
uanachama.
Alisema Nyalandu si
mtia nia mwenye “Mbwembwe” kama wengine wanavyofanya ndani ya chama hicho
mazingira ambayo yanampa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro
hiko ndani ya chama na kwamba anaamini mungu atasikiliza ombi la wana CCM wa
wilaya ya Masasi.
Alisema kwa sasa
chama kinahitaji mtu mwenye uwezo wa kukipeleka mbele chama na si kukirudisha
nyuma kwani watanzania bado wanakiamini kutokana na sera zake ambazo nyingi
zimewaletea maendeleo wananachi hivyo ni vyema akapewa nafasi hiyo mwanachama
mwenye mapenzi mema na chama kama alivyo Nyalandu.
“Mimi nakuombea
uchaguliwe kuwa mgombea urais kupitia chama cha Mapinduzi…na endelea kutoa rai
kwa viongozi wenzako wakilinde chama hiki waache malumbano yasiyo na tija na
kwa yule mwanachama anayesema asipochaguliwa ataondoka CCM basi huyo hatufai”.alisema
Pole.
Kwa mujibu wa Pole
alisema wanachama waliojitokeza kumdhamini ni kutoka kwenye kata za Nyasa,Mkuti
pamoja na Jida na kwamba huo ni utaratibu waliouweka ndani ya chama wilayani
humo ili kila mtia nia anapokuja aweze
kupata wadhamini na kwamba wao kama mkutano mkuu watafanya maamuzi ya busara.
Nyalandu anaendelea
kutafuta wadhamini mkoani Lindi na baadae hii leo ataelekea mkoani Ruvuma
katika wilaya ya Songea.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD