Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

NIMEKUWEKEA HAPA STORY TANO (05) KUBWA KWENYE MAGAZETI YA LEO TANZANIA NA HABARI KIBAO

TANGAZO




MWANANCHI
CCM imesema kuwa itahakikisha inarudi Ikulu hata “kwa bao la mkono” wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya Nyehunge wilayani hapa.
Neno “bao la mkono” hutumiwa kama goli lililofungwa kwa kuupiga mpira kwa mkono kinyume cha taratibu za mpira, lakini hukubaliwa kwa kuwa mwamuzi anakuwa hajaona kitendo hicho.
“Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono... bao ni bao tu ili mradi refa hajaona,” alisema Nape.
Nape, aliye kwenye ziara ya katibu mkuu wa CCM, aliwataka wananchi wa Sengerema kusubiri ushindi wa chama hicho na kuwakumbusha kuwa wanapaswa kuiweka CCM kuanzia udiwani mpaka ubunge kwa nafasi ya urais tayari kuna uhakika.
Katika mkutano huo, Nape alisema ana uhakika CCM itashinda baada ya kushuhudia mwitikio wa Watanzania tangu alipoanza kuongozana na Kinana katika ziara zake za kuizunguka nchi na kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero zao.
Amebainisha kuwa amejifunza na kujiridhisha kuwa chama chake bado kinapendwa miongoni mwa wapigakura waliofikiwa tofauti na vyama vya upinzani.
“Tumefika maeneo mengi ambayo upinzani haujafika. Huko tuna hazina kubwa ya wanachama. Hakuna namna Ukawa wanaweza kuingia Ikulu mwaka huu,” alisisitiza.
Wapinzani waja juu
Kauli hiyo ya Nape ilipingwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani waliosema kuwa mtendaji huyo anamaanisha kuwa CCM itaiba kura.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa hakutaka kabisa kuzungumzia kauli ya Nape zaidi ya kusema watakutana Oktoba.
“Kwa bahati mbaya kauli za Nape siwezi kuzijibu. Kauli za Nape zichukue kama zilivyo, ingekuwa ni (katibu mkuu wa CCM, Abdulraham) Kinana, ningemjibu lakini ajue kuwa tutakutana Oktoba,” alisema Dk Slaa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo.

MAJIRA
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, amesema kama CCM kitamteua kuwa mgombea urais na kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao, atahakikisha Ikulu na nyumba za wizara zote zinahamia Dodoma.

Bw. Membe ambaye ni miongoni mwa wagombea urais ndani ya CCM, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa mkoa huo na wana CCM waliojitokeza kumdhamini.

"Hili jambo nimelifikiria muda mrefu, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alitumia nguvu na fedha nyingi kujenga Ikulu ya Chamwino hivyo nikiwa rais, nitahamia Dodoma.

"Siwezi kukaa hapa peke yangu, lazima Mawaziri wangu wote nao waishi jirani na mimi," alisema Bw. Membe na kuongeza;
"Kama kuna mtu miongoni mwenu anategemea kuteuliwa katika baraza nitakalounda, ajiandae kuishi Dodoma maana nitaishi katika Ikulu aliyojenga na Mwalimu," alisema.

Aliwahakikishia wana CCM waliojitokeza kumdhamini kuwa, hawatajutia uamuzi huo; bali atatii kiu yao, kuwaletea uongozi bora na makini unaochukia rushwa na ufisadi kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.

Alitoa wito kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu, kuhakikisha wanamchagua yeye ambapo sera yake ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda unaobebwa na kilimo iko palepale.

Bw. Membe anaendelea kutafuta wadhamini mkoani Morogoro.

HABARI LEO
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limemtangaza Shehe Abubakar Zuberi Ally kuwa Kaimu Shehe Mkuu na Mufti wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Mufti Shehe Shaaban Issa bin Simba kufariki dunia wiki moja iliyopita.
Shehe Zuberi, atashika wadhifa huo kwa siku 90 ili kupisha uchaguzi utakaofanyika kumpata kiongozi huyo mkuu wa Waislamu nchini kwa mujibu wa taratibu za Kiislamu.
Uteuzi huo ulifanyika na kutangazwa jana asubuhi Bagamoyo, Pwani mara baada ya Baraza la Ulamaa lenye wajumbe 7 kukaa na kumteua Shehe Zuberi kushika wadhifa huo.
Akitangaza uteuzi huo katika ofisi za makao makuu ya Bakwata jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Bakwata, Shehe Suleiman Lolila alisema Baraza la Ulamaa lilikaa likiwa na wajumbe nane ili kumteua Kaimu Mufti.
Uteuzi huo ulifanyika kwa kupiga kura ya siri ambapo kati ya wajumbe wote waliohudhuria, Shehe Ally alipata kura zote nane na hivyo kuteuliwa na kushika wadhifa huu kwa siku 90.
“Kwa mujibu wa Katiba yetu ya Bakwata, Mufti akifariki dunia Baraza la Ulamaa linatakiwa likae na kumteua Naibu Shehe Mkuu na Mufti ambaye anatakiwa kudumu kwa kipindi cha miezi mitatu,“ alisema Lolila.
Akizungumza mara baada ya uteuzi huo, Shehe Zuberi alisema amefurahi kuteuliwa kushika wadhifa huo na yupo tayari kuitumikia Jumuiya ya Waislamu na kuendeleza yale yote mema aliyoacha Mufti Simba na kusimamia vyema mchakato wa kumpata Mufti mpya.
“Nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuhakikisha kuwa kwa kipindi hiki cha miezi mitatu tunampata Mufti atakayetuongoza baada ya kufiwa na mpendwa wetu, Mufti Simba, “ alisema Shehe Zuberi.
Alisema ataendeleza umoja na mshikamano uliopo baina ya Waislamu pamoja na kuifanyia marekebisho Katiba iliyopo ili iweze kukidhi mahitaji yaliyopo na kuwaunganisha Waislamu kwa pamoja.
JAMBO LEO
WAMILIKI wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), wamesema endapo Serikali itapitisha Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari watasitisha huduma ya utoaji wa habari katika vyombo binafsi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Dk. Reginald Mengi alisema kama Serikali itavinyima uhuru wa kukusanya habari na kusambaza ni kuwanyima haki Watanzania.
Alisema mfumo na utaratibu kama huo ni hatari na haelewi Serikali inataka kufanya nini, kwani uhuru wa demokrasia ni nguzo muhimu katika kujenga amani na ushirikiano.
“Katika hali ya sasa ni muhimu kufahamu vitu vinavyotokea kwa undani, kwa nini kuwe na haraka wa kupitisha muswada huo usiokuwa na tija kwa jamii kutokana na kunyimwa uhuru wa kupata habari,” alisema.
Mengi alihoji ni nini Serikali inataka kukificha ambacho wananchi hawatakiwi kukijua huku wakiwaacha wachache walio serikalini kukijua na kwamba kufanya hivyo ni kuwanyima Watanzania uhuru wa kupata habari na hicho ni chanzo cha kuleta matatizo katika nchi.
Alisema azimio la Moat ni kuomba Serikali kuondoa muswada huo bungeni kwa sababu unamgusa kila Mtanzania, huku akibainisha kuwa Serikali ikigusa vyombo vya habari ni sawa na kuigusa Watanzania wote.
Kwa upande wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, alisema Watanzania wanaelekea kwenye mchakato huo, lakini hatuwezi kuwa na uchaguzi huru ikiwa vyombo vya habari havina uhuru wa kupokea na kuandika habari ili wananchi waweze kuelewa, hivyo Serikali inatakiwa kujadili kwa makini ili kunusuru machafuko yanayoweza kujitokeza.
“Hatuwezi kuficha vitu wakati mambo yanatakiwa yawe wazi na kama tungekuwa tunataka uwazi tusingeruhusu vyombo vya habari kuwa wazi, hivyo muswada huo utatupa matatizo kwenye uchaguzi na hauwezi kuwa huru pasipo wananchi kujua nini kinaendelea kupitia vyombo hivyo,” alisema Mengi.
Kwa upande wake, Rostam Azizi ambaye ni mmiliki wa vyombo vya habari, alisema muswada huo ni mbaya hauna haja ya kuwa na majadiliano bungeni kuhusu vifungu vilivyomo.
Alisema anaiomba Serikali isitishe kuupeleka bungeni kwa sababu utaleta matatizo katika nchi ambayo inajivunia upendo na amani huku akisema muswada pia alisema unaua dhana ya uwazi.
HABARI LEO
IDADI ya wagombea wanaochukua fomu kwa ajili ya kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana walifikia 39 baada ya mwanachama wake, Ritha Ngowi kuchukua fomu.
Ngowi, mkazi wa Dar es Salaam, anakuwa mwanamke wa tano kuchukua fomu, ambapo waliochukua fomu wa awali ni Balozi Amina Salum Ally, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Asha-Rose Migiro, Dk Mwele Malecela na Monica Mbega.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema yeye ni msomi ambaye ana shahada ya Maendeleo ya Jamii na pia amepitia kozi mbalimbali katika ngazi za diploma na cheti. Alisema vipaumbele vyake vitakuwa ni kwenye sekta ya elimu na uchumi.
“Nimeguswa sana na kuamua kugombea nafasi ya Urais lengo langu kubwa ni kutaka kuboresha elimu na Uchumi” alisema.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha kila Mtanzania anapata elimu ya msingi na asiwepo Mtanzania asiye na uwezo wa kupata kipato na atahakikisha Watanzania wanawezeshwa ili kuwe na uzalishaji.
Kwa upande wa uchumi alisema atamairisha vivuko kwa ajili ya kupunguza foleni, na wakulima watapatiwa pembejeo na mazao yao yatatafutiwa masoko.
Hata wafanyabiashara kazi zao katika mazingira mazuri na wafanyakazi wa serikali watapata mishahara mizuri itakayowezesha wananchi kuishi maisha yenye viwango. Alisema atarekebisha mishahara kuanzia ngazi ya chini.
“Unaweza kuona mtu anapokea mshahara wa Sh 350,000 hadi 450,000 anapanga nyumba na analipa ada, maslahi yao lazima yarekebishwe,” alisema.
Alipohojiwa kama ana sifa 13 za mgombea wa CCM anavyo alisema anazo sifa hizo zote ndio maana amejitokeza. Pia alipohojiwa atatanuaje tatizo la rushwa iwapo ataingia madarakani, alisema ili kuondoa tatizo la rushwa jambo la kwanza ni kudhibiti vyanzo hivyo.
Alisema kutakuwepo na mikakati ili fedha zote zinazokusanywa zifike kwenye vyanzo husika na huduma zifike mahali panapostahili.
Katika historia yake alisema amewahi kufanya kazi Shirika la Uchumi na Maendeleo ya Wanawake Tanzania (Suwata) pia aliwahi kufanya kazi Chama cha Wasioona Tanzania, pia mmiliki wa shule ya sekondari ya Jostihego iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Mawaziri 2 warudisha fomu Wakati huo huo, mawaziri wawili wanaowania kuteuliwa na CCM, kuwa wagombea wa nafasi ya Urais jana walirudisha fomu. Waliorudisha fomu ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri wa Kilimo na Ushirika Steven Wassira.
Balozi Karume Mgombea mwingine, Balozi Ally Karume alirejesha fomu yake saa 10.35 jioni. Alichukua fomu hiyo Juni 4, mwaka huu na kwenda kutafuta wadhamini katika mikoa mbalimbali ya Bara na Visiwani, mwenyewe akisema amepata wadhamini wa kutosha na wengine wa ziada.


TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top