TANGAZO
Mwalimu Mustapha Swalehe akitangaza nia hii leo mjini Masasi. |
Na Mwandishi
wetu,Masasi.
MWALIMU Mustafa
Swalehe (41) ambaye kwa sasa anasoma shahada ya usimamizi wa biashara (Business
Administration) mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha Stella Maris tawi la Mtwara
ametangaza rasmi nia yake ya kugombea
nafasi ya ubunge jimbo la Masasi kwa tiketi ya UKAWA.
Akitangaza nia yake
hii leo katika viwanja vya mti Mwiba mjini Masasi alisema ameamua kugombea
nafasi hiyo ya ubunge kupitia umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) kwa lengo la
kupigania maisha ya wakulima hasa wa zao la korosho ambao kwa muda mrefu sasa
wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kushuka kwa bei ya
zao hilo.
Alisema kwa sasa
nchini kumekuwa na ongezeko kubwa la bei ya pembejeo huku bei ya zao la korosho
ikiendelea kushuka mazingira ambayo hupelekea maisha ya wakulima kubaki kuwa
duni ambapo alisema endapo UKAWA utampitisha kuwa mgombea wa nafasi hiyo basi
kero hizo zitabaki kuwa historia.
Alisema ubunge wa
sasa ni wa kisayansi unaojengwa kwa hoja za msingi ambazo zinapaswa kutekelezwa
kwa uhakika na kwa ufanisi wa hali ya juu utakaowaletea maendeleo wananchi wa
jimbo la Masasi huku akiwaomba vijana kufanya maamuzi magumu katika uchaguzi
mkuu ujao kwa nafasi ya ubunge.
Kwa mujibu wa mtia
nia huyo ambaye ni mwanachama wa chama
cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) alisema jimbo la Masasi kwa sasa
linahitaji mbunge mwenye elimu kama yeye ambapo alisema miswada inayojadiliwa
na kupitishwa na wabunge bungeni huandikwa kwa lugha ya kigeni ya kiingereza
hivyo ni vyema wakachagua mgombea mwenye nguvu na uwezo mkubwa atakayeendana na kasi iliyopo kwa
sasa.
“Ndugu zangu wana
Masasi hivi ni kweli bungeni hakuhitaji elimu?...mnachopaswa kutambua kuwa suala hilo
si kweli na tunadanganyana kuwa eti kuwa mbunge si lazima uwe na elimu binafsi sikubaliani na hilo kwani
miswada mingi iko kwenye lugha ya kiingereza,je hivi leo tukichagua mbunge
ambaye hana elimu hataweza kutuletea maendeleo? Alihoji Swalehe huku
akishangiliwa.
Akizungumzia kuhusu
sera ya vijana Swalehe alisema kwa sasa hakuna kijana hata mmoja wilayani
Masasi ambaye yuko kwenye baraza la vijana la Chama hivyo ni vyema wakaungana
katika kuhakikisha wanafanya mabadiliko makubwa ya uongozi ambapo aliwahimiza
vijana kuthubutu kuhusu masuala ya kisiasa.
Aidha alisisitiza
msimamo wake kuwa yeye atakuwa mbunge mwenye huruma kwa wananchi wake na kwamba
kwa hali ilivyo hivi sasa jimbo la Masasi linahitaji mbunge kama yeye mwenye
uwezo wa kufanya kazi kwa uhakika atakayelinda rasilimali za mafuta na gesi.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliokuwepo kwenye mkutano huo wa hadhara
walisema mwalimu Mustapha Swalehe ndio tegemeo lao katika uchaguzi mkuu ujao
kwa nafasi hiyo ya ubunge huku wakiweka wazi hisia zao kuwa atakuwa mkombozi wa
wakulima,watumishi,wazee,akinamama pamoja na vijana.
Mwalimu Mustapha
Swalehe alizaliwa Machi 3, 1974 katika wilaya ya Newala mkoani Mtwara alipata
elimu yake ya msingi mwaka 1983-1989 katika
shule ya msingi Karume wilayani Newala,mwaka 1990 hadi 1993 alipata elimu ya
sekondari Newala na baadae alichaguliwa kujiunga na chuo cha ualimu Mtwara
ambako alihitimu astashahada yake mwaka 1996.
Aidha mnamo mwaka
2002 alipata stashahada ya ualimu ambapo mwaka 2010 alihitimu astashahada
nyingine ya uongozi na utawala wa elimu katika chuo cha uongozi cha Bagamoyo
(ADEM) na kwamba kwa sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha
Stella Maris mkoani Mtwara ambapo wiki tatu zijazo anatarajia kumaliza.
Mwisho.
BAADHI ya wananchi wakiwa na mabango kwenye mkutano huo maeneo ya mti Mwiba mjini Masasi wakionesha hisia zao kwa mtia nia huyo wa CHADEMA anayeomba kuteuliwa na UKAWA kuwa mgombea ubunge jimbo la Masasi.
MWALIMU Mustapha Swalehe akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Masasi waliojitokeza kumsikiliza wakati anatangaza nia yake ya kugombea nafasi ya ubunge kupitia UKAWA.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD