Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

LUKUVI AZITAKA HALMASHAURI NCHINI KUHARAKISHA UPIMAJI WA ARDHI NA MASHAMBA YA WANANCHI

TANGAZO
Waziri Lukuvi wakati anaongea na wananchi wa mji wa Masasi.

Na Clarence Chilumba, Masasi.
WAZIRI wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi Wiliam Lukuvi ameziagiza halmashauri zote nchini kuharakisha upimaji wa ardhi na mashamba katika maeneo ya wananchi ambao ndio wamiliki wa asili wa maeneo hayo ili kuondoa migogoro ya ardhi inayosababisha wananchi kuichukia serikali yao.
Agizo hilo amelitoa leo wilayani Masasi baada ya kupokea taarifa ya wilaya iliyosomwa na mkuu wa wilaya hiyo Bernald Nduta ambapo alisema umilikishaji pamoja na upimaji wa ardhi ndio njia pekee inayoweza kupunguza ama kuondoa kabisa migogoro huku akikiri kuwa mingi ya migogoro hiyo husababishwa na maofisa wa ardhi wa Halmashauri nchini.
Alisema halmashauri zinapaswa kupima ardhi na mashamba kwa lengo la kuongeza thamani ya maeneo hayo huku akitoa masharti kuwa wakati wa upimaji wa maeneo hayo ni lazima kuwe na makubaliano ya kisheria kati ya wamiliki na halmashauri na kwamba pia wanapaswa kulipwa fidia zao za umiliki.
Alisema tatizo kubwa lililopo katika halmashauri nyingi nchini ni pale wananchi wanaposhindwa kupewa taarifa wakati wa zoezi la upimaji wa maeneo yao mazingira ambayo husababisha migogoro ambayo imekuwa kero kubwa kwa wizara ya ardhi.
Kwa mujibu wa waziri huyo alisema kwa sasa kitu pekee ambacho halmashauri zote nchini zinapaswa kufanya ni kushirikiana na baadhi ya makampuni ya watu binafsi ambayo yamekuwa yakifanya kazi za upimaji wa ardhi na mashamba ambayo hulipa fidia au mradi shirikishi ambao kampuni hupima ardhi na kugawana viwanja kati ya wamiliki na kampuni husika.
Aidha aliziasa halmashauri hizo kufanya kazi na kampuni zilizosajiliwa na zinazotambulika na wizara ya ardhi ili kuepusha usumbufu ambao baadhi ya wilaya ikiwemo wilaya ya Lindi imezikumba ambapo kampuni ya UTT iliyopima viwanja ililipa fidia ya shilingi 400,000 kwa wamiliki kwa ekari moja huku kampuni hiyo ikiuza ekari moja kwa shilingi milioni 16.
Akizungumzia kuhusu tatizo la uhaba wa watumishi wa idara ya ardhi nchini alisema kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016 serikali imeajiri maofisa wa ardhi, wapimaji na wathamini wapatao 60 nchi nzima ambao hawatoshi na kwamba ili kurahisha huduma za ardhi wizara yake imepanga kuleta maofisa hao kwa kila kanda pamoja na kununua vifaa mbalimbali vya upimaji ambavyo vingi vina gharama kubwa.
Awali akisoma taarifa ya wilaya kwa waziri huyo mkuu wa wilaya ya Masasi Bernald Nduta alisema halmashauri ya mji wa Masasi imeweza kuandaa mchoro wa mipango miji wa eneo la ujenzi wa nyumba za gharama nafuu za shirika la nyumba la Taifa pamoja na viwanja vya wananchi 30 waliopisha ujenzi wa nyumba hizo.
Alisema kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Masasi imefanikiwa kwenye mpango wa urasimishaji wa ardhi ulioanza mwaka 2010 chini ya ufadhili wa Mkurabita na shirika lisilo la kiserikali la Concern  World wide ambapo hadi sasa jumla ya vijiji 14 vimefanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Mwisho.
WAZIRI wa Ardhi Wiliam Lukuvi akimsikiliza mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi Kazumari Malilo alipotembelea ofisi ya Ardhi ambayo ilichomwa moto.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top