TANGAZO
Na Mwandishi Wetu, Mtwara
MFUKO wa
Taifa wa Bima ya Afya katika juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma zake na
kuhakikisha wanachama wake na wananchi wanapata huduma bora imehamasisha
viongozi na wadau wa sekta ya Afya Mkoani Mtwara kuchangamkia fursa ya mikopo
ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo toka Bima ya Afya.
Akizungumza
katika warsha iliyokutanisha wadau wanaohusika na utoaji wa huduma hiyo, Afisa
wa Bima ya Afya makao Makuu, Isaya Shekifu alisema kuwa mpango huu wa mikopo ya
vifaa tiba ulianza tangu mwaka wa fedha 2007/2008 na umekuwa ukiboreshwa kila
wakati kutokana na mahitaji ya wadau na nia ya mfuko ya kuboresha huduma za
afya.
Alifafanua
kuwa tangu kuanzishwa kwa mikopo ya vifaa tiba mwaka 2008 hadi kufikia Disemba
mwaka jana kiasi cha 10.24 bilioni ziliidhinishwa kwa ajili ya vituo 194 na
kati yake vituo 146 vilikidhi masharti na kuchukua mkopo wa Sh. 5.34 bilioni.
Aidha
alieleza kuwa kwa upande wa mikopo kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya kutolea
huduma kiasi cha Sh. 6.8 bilioni ziliidhinishwa na walioweza kukidhi masharti
waliweza kuchukua kiasi cha Sh. 2.14 bilioni.
“Kwa
mkoa wa Lindi na Mtwara mwamko umekuwa mkubwa na wameupokea vizuri ,wengi wao
wameomba Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuendelea kuboresha mpango huu ”alisema
Shekifu na kuongeza
“Iko mikopo
ya aina nne wa kwanza ni wa vifaa tiba ambao marejesho yake ni kwa kipindi cha
miezi 24 mpaka 60, wa pili ni mkopo wa vifaa vya Tehama ambao nao ulipaji
wake ni miezi 24 mpaka 60,mkopo wa dawa na vitendanishi ambao marejesho
yake ni kwa kipindi cha miezi 15,”alisema Shekifu
Aidha
alieleza kuwa mkopo na marejesho yake yatategemea madai ya kila mwezi ya
mkopaji kwa huduma za matibabu zitolewazo kwa wanachama wa Mfuko na vyanzo
vingine ambavyo kituo kitabainisha kutumika kulipia mkopo na mkopaji anatakiwa
kujaza fomu ya maombi kama Mwongozo wa Serikali kwa Vituo vya Afya
unavyoainisha na fomu ya maombi itatozwa kiasi cha Sh. 20,000
Akizungumza
Meneja wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoa wa Mtwara, Joyce Sumbwe alisema
kuwa kwa mkoa wake hali si mbaya na tayari baadhi ya watoa huduma
wameweza kukopa hadi mara ya pili na kiasi cha Sh.170 milioni zimeweza kutolewa
kwaajili ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo.
“Hali si
mbaya sana kwa mkoa wa Mtwara baadhi ya watoa huduma washaanza
kukopa hadi kwa mara ya pili na kiasi cha Sh.170 milioni zishatolewa
kwaajili ya vifaa na kwa wilaya za Masasi,Tandahimba na ,Newala zimeweza kukopa
pamoja na zahanati ya Fajma,Likombe, na hospitali ya mkoa,”alisema Sumbwe
Aidha
aliendelea kubainisha kuwa kwa sasa wanaendelea kusajili maduka ili watu
watakapohitaji huduma za dawa katika vituo na kukosa basi waweze
kuzipata katika maduka ya dawa ikiwa ni sambamba na kuendelea kuwaelimisha watu
waone umuhimu wa Bima ya afya.
Afisa wa Bima ya Afya makao Makuu, Isaya Shekifu wakati
akiwasilisha mada zake kwa washiriki kushoto ni meneja wa mfuko huo mkoa wa
Mtwara, Joyce Sumbwe.
Baadhi ya wadau wanaohusika na
utoaji wa huduma za Afya wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye mkutano huo ulioandaliwa na NHIF.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD