TANGAZO
Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi Renatha Mzinga |
Na Clarence Chilumba,Masasi.
KAMANDA wa polisi mkoa wa Lindi Renatha Mzinga amewataka
askari wa kike nchini wahakikishe wanatimiza majukumu yao kikamilifu ikiwa ni
pamoja na kufanya kazi kwa weledi na nidhamu katika kitengo cha dawati la jinsia chenye waathirika
wengi wa matukio ya unyanyasaji nchini.
Wito huo
ameutoa leo wilayani Masasi wakati wa uzinduzi wa mtandao wa polisi wanawake
Tanzania (TPF-NET) pamoja na dawati la jinsia ambapo alisema mtandao huo ni chombo pekee cha
ukombozi kwa askari wa kike ambao kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wakikabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na unyanyasaji kutoka kwa baadhi wa
askari wa kiume.
Alisema TPF-NET iliundwa kwa lengo la kupambana
na vitendo vyote vya unyanyasaji wanavyovipata askari wa kike kutoka kwa raia
pamoja na baadhi ya askari wa kiume na kwamba uwepo wa mtandao huo ambao kwa
sasa umeenea kila kituo cha polisi nchini umesaidia kuondoa changamoto hizo.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Lindi
alisema licha ya kutetea haki za askari wa kike TPF-NET pia husimamia nidhamu
pamoja na maadili kwa wanachama wake wote ambao ni askari wote wa kike wa jeshi
hilo.
“Ndugu zangu askari wa kike leo tunafanya
uzinduzi wa mtandao huu…mtambue kwamba chombo hiki ni muhimu kwetu kwa maslahi
yetu hivyo kila alipo askari wa kike nchni anapaswa kutimiza majukumu yake kwa
kufuata kanuni na sheria za jeshi la polisi Tanzania”.alisema Mzinga.
Alisema askari wa kike wanapaswa kutumia fursa
mbalimbali zilizopo kwenye jeshi hilo ikiwemo elimu kwa kujiendeleza ili nao
waweze kufikia nafasi za juu za uongozi wa jeshi la polisi kama wao walivyoweza
ambao kwa sasa wako kwenye nafasi za juu za uongozi.
Awali akisoma risala fupi mmoja wa wanachama wa
mtandao huo Pendo Pakacha alisema wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali
katika uetekelezaji wao wa majukumu ya kila siku ikiwemo ukosefu wa nyenzo za
kutendea kazi, ukosefu wa rasilimali fedha pamoja na ofisi ya mtandao kwani kwa
sasa mtandao hauna ofisi.
Alizitaja changamoto zingine kuwa ni ukosefu wa
mtaji wa kuanzisha mradi hivyo kushindwa kufikia moja ya malengo ya mtandao huo
ya kuinua vipato vya askari wa kike ambapo walimuomba kamanda wa polisi mkoa wa
Lindi kuwafikishia kilio chao kwa uongozi wa juu wa jeshi hilo nchini.
Mtandao wa polisi wanawake Tanzania (TPF-NET)
ulianzishwa rasmi wilayani Masasi mwaka 2009 ambapo kwa sasa una jumla ya
wanachama 41.
KAMANDA wa polisi mkoa wa Lindi Renatha Mzinga akiwa na Afisa Mnadhimu wa jeshi la polisi mkoa wa Mtwara George Salala wakipiga makofi wakati wakipokea maandamano ya askari wa kike wa wilaya ya Masasi hii leo wakati wa uzinduzi wa Mtandao wa polisi wa kike wilayani humo.
BAADHI ya askari wa kike wa jeshi la polisi wilaya ya Masasi wakiwasili kwenye ukumbi wa miduleni mara baada ya kumaliza kwa maandamano yao yaliyoanzia viwanja vya polisi Masasi na kupita kwenye Barabara kuu iendayo Mkoani Mtwara na hatimaye kwenye Barabara ya Mkapa.
Askari wa kike ambao ni wanachama wa Mtandao wa Polisi wa kike Tanzania (TPF-NET) wilaya ya Masasi wakiwa kwenye ukumbi wa Miduleni wilayani Masasi wakati wa uzinduzi wa Mtandao wao hii leo.
MAANDAMANO ya askari wa kike wa jeshi la polisi wilaya ya Masasi yakipita kwenye Barabara ya Mkapa hii leo wakiwa na wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Masasi pamoja na wanafunzi wa sekondari ya kutwa ya Masasi.
ASKARI wa kike wa wilaya ya Masasi pamoja na wanafunzi wa sekondari ya wasichana Masasi wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi ambaye ni kamanda wa polisi mkoa wa Lindi Renatha Mzinga wakati wa uzinduzi wa TPF-NET.
MAANDAMANO ya askari wa kike wa jeshi la polisi wilaya ya Masasi yakiwasili kwenye ukumbi wa Miduleni wilayani Masasi hii leo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD