TANGAZO
Na Haika Kimaro,Mtwara.
TAASISI ya utafiti wa kilimo Naliendele iliyopo mkoani Mtwara
imefanikiwa kugundua mbegu bora chotara 24 za zao la korosho kwa mwaka wa fedha
2014/2015 na kuifanya taasisi hiyo kuwa ya kwanza barani afrika kwa ugunduzi wa
idadi kubwa ya mbegu za zao hilo.
Hayo yameelezwa na mtafiti kiongozi wa zao la korosho nchini Dkt.
Peter Massawe alipokuwa akiongea na wajumbe wa mkutano wa mapitio ya shughuli
za utafiti wa zao hilo na kuwa tayari mbegu hizo zilisajiliwa mapema Februari
mwaka huu zikiwa na sifa za ukinzani wa magonjwa na wadudu waharibifu kutoa
mavuno mengi na ukubwa wa korosho hizo.
“Utafiti wa korosho umefanikiwa kutoa mbegu chotara 24 ambazo zilisajiliwa
Februari mwaka huu na hii imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika
na kama sio duniani katika kutoa mbegu chotara iliyopitia katika mfumo wa
utafiti ya kuweza kufanya majaribio katika mazingira matatu tofauti na kutumia
data hizo na imeweka rekodi za kidunia,’alisema Massawe na kuongeza
“Na kwa upande wa Tanzania wizara ya kilimo idadi ya mbegu za
kilimo walizokusudia kutoa imepanda kutokana na mchango unaotoka katika mbegu
hizi 24 za zao la korosho,”alisema.
Akizungumza kaimu mkurugenzi wa taasisi hiyo Dkt. Omary Mponda alisema mafanikio hayo ni ya kujivunia kwa taasisi
yake na wadau wa zao la korosho nchini na wakulima sasa kuanza kutumia mbegu
hizo.
“Kubwa zaidi ni kwamba baada ya ugunduzi wa mbegu hizi wakulima
ama maafisa ugani wakishafahamu wakatengeneze vitalu ili ikapandwe na uweze
kusambazwa kwa wakulima walio wengi na mategemeo yetu ni kuwa mbegu hizi zitachangia
uzalishaji kwa wingi hapa nchini,”alisema Dkt. Mponda
Akizungumza Afisa ugani toka Mkuranga mkoa wa Pwani Julitha Bulali
alisema mkutano kikao hicho kimewawezesha kupata taarifa mpya
za kiutafiti na hivyo kuwawezesha kuwapelekea wakulima taarifa nzuri na zilizo
sahihi.
Kwa mujibu wa bodi ya korosho Tanzania uzalishaji wa zao hilo
umeongezeka kufikia tani laki moja tisini na sita elfu katika msimu uliopita
huku matumizi ya mbegu bora na teknolojia sahihi za uzalishaji wa zao hilo zikielezwa
kuwa na mchango kubwa katika kukuza kiwango cha uzalishaji na ubora wa korosho
nchini.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD