TANGAZO
Na
Clarence Chilumba,Nanyumbu.
Jumla
ya miradi 47 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 69 inatarajiwa kupitiwa
na mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2015/16 katika mkoa wa Mtwara wenye
halmashauri sita pamoja na wilaya tano
huku wananchi mkoani humo wakiupokea mwenge wa uhuru kwa staili ya aina yake.
Akisoma
taarifa ya mkoa wa Mtwara wakati wa makabidhiano ya mwenge wa uhuru kati ya
mkoa wa Mtwara na mkoa wa Ruvuma Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego alisema
mbio za mwenge wa uhuru mkoani humo zitakimbizwa kwa umbali wa kilometa 649.3
kukiwa na miradi 47 yenye thamani ya shilingi Bilioni 69.
Makabidhiano
hayo yalifanyika jana majira ya saa 4:00 asubuhi katika kijiji cha Lumesule
kilichoko mpakani mwa wilaya ya Nanyumbu na Tunduru mkoani Ruvuma
yaliyomuhusisha kaimu mkuu wa mkoa wa Ruvuma Profesa Norman Sigala pamoja na
mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego.
Alisema
kati ya miradi hiyo 47, miradi 17 itafunguliwa, 13 itawekewa mawe ya msingi
huku miradi 17 ikikaguliwa na kwamba
kati ya pesa hizo mchango wa wananchi bilioni tatu sawa na asilimia 3.7,mchango
wa Halmashauri za wilaya ni shilingi bilioni mbili sawa na asilimia 2.4 huku
kwa upande wa serikali kuu ikichangia shilingi bilioni saba na mchango wa
wahisani ni shilingi bilioni 83 sawa na asilimia 86.6.
Kwa
mujibu wa mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa wa Mtwara wenye jumla ya wakazi halali
milioni 1.2 umetekeleza kikamilifu ujumbe wa mwenge wa mwaka huu unaosema “tumia
haki yako ya kidemokrasia” chini ya kauli mbiu isemayo “jiandikishe na kupiga
kura katika uchaguzi wa mwaka 2015” na kwamba hadi sasa asilimia 98.9 ya
wananchi mkoani humo tayari wamejiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga
kura lililoanza Aprili 30 mwaka huu mkoani humo.
Alisema
mkoa wa Mtwara umejipanga vyema katika mapambano dhidi ya rushwa,Ugonjwa wa
Ukimwi,dawa za kulevya pamoja na Malaria na kwamba uteja wa dawa za kulevya
unazuilika na kutibika huku akiwaasa vijana mkoani humo kupambana na maambukizi mapya ya Ukimwi
ugonjwa unaoathiri hasa kundi la vijana ambao ndio taifa la leo na kesho.
Awali
akikabidhi mwenge wa uhuru kwa mkuu wa
mkoa wa Mtwara ,kaimu mkuu wa mkoa wa Ruvuma Profesa Norman Sigala alisema
mwenge wa uhuru mkoani humo ulikimbizwa katika jumla ya kilometa 1163 huku
miradi 41 yenye thamani ya shilingi bilioni 10 ikipitiwa na mwenge wa uhuru.
Alisema
kati ya miradi hiyo tisa ilifunguliwa,miradi 12 ilizinduliwa,16 iliwekewa mawe
ya msingi na miradi minne ikikaguliwa ambayo amekiri kuwa kufanikiwa kwa miradi
hiyo ni kutokana na matumizi sahihi ya fedha za miradi inayotolewa na serikali
kwa halmashauri za wailaya mkoani humo.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wakati wa makabidhiano hayo kwenye viwanja vya shule ya
msingi Lumesule wilayani Nanyumbu mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma
Bakari Nalicho na mkuu wa wilaya ya Nanyumbu Sauda Mtondoo walisema mwenge wa
uhuru ni kielelezo cha uhai wa taifa letu na kwamba watanzania wanapaswa
kuuheshimu ili kudumisha amani na umoja miongoni mwa watanzania.
Kwa
upande wake kiongozi wa kitaifa wa mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka huu Juma
Chumu aliushukuru uongozi na wananchi wa mkoa wa Ruvuma kwa mapokezi mazuri
waliyowapa katika kipindi chote walichokaa mkoani humo huku akiwaasa wana
Mtwara kuiga mfano bora kutoka kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma.
Mbio
za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2015/2016 mkoani Mtwara zimeanza rasmi hii leo Mei
5,mwaka huu katika wilaya ya Nanyumbu ambapo mbio hizo zitakimbizwa kwa siku sita
zikipita kwenye wilaya zote tano za mkoa huo pamoja na halmashauri sita.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD