TANGAZO
WANANCHI katika Halmashauri ya mji wa Masasi
mkoani Mtwara wametakiwa kutumia kwa malengo yaliyokusudiwa fedha inayotolewa kupitia
mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na mfuko wa maendeleo ya jamii nchini
TASAF.
Rai hiyo imetolewa jana na mkurugenzi wa halmashauri
ya mji wa Masasi Fortunatus Kagoro wakati anazungumza na baadhi ya wanufaika wa
mpango huo katika vijiji vya Maendeleo, Mkarakate pamoja na Sululu vyote vikiwa
ni vya Halmashauri ya mji wa Masasi.
Kagoro alifanya ziara fupi la kukagua utaratibu
mzima unaotumika wakati wa kugawa fedha hizo ndani ya Halmashauri ya mji wa
Masasi ambapo alijionea namna baadhi ya wanufaika walivyotoa ushuhuda ni kwa
jinsi gani wemeweza kubadilisha maisha yao kupitia mpango huo wa kunusuru kaya
maskini.
Alisema serikali kupitia TASAF imedhamiria
kuondoa umaskini wa kipato unaowakabili wananchi wengi nchini na kwamba ili
kuunga mkono jitihada hizo za serikali wananchi ambao ni wanufaika wa mpango
huo wanapaswa kutumia fedha hizo kwa kile kilichokusudiwa.
Alisema kumekuwa na taarifa kuwa baadhi ya wanufaika wa mpango wa kunusuru
kaya maskini wamekuwa wakitumia fedha hizo vibaya kinyume na malengo yaliyopo
huku wengine wakitumia fedha hizo kuongeza wanawake kwa upande wa wanaume na
wengine wakitumia kwa ajili ya ulevi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo alisema mpango
huo wenye lengo la kupunguza umaskini unatoa fedha hizo kwa ajili ya matumizi
ya elimu, afya lakini cha ajabu wananchi wengi mara baada ya kupata fedha hizo
wamekuwa wakibadilisha matumizi mazingira ambayo kila siku wamekuwa
wakilalamika kuwa fedha hizo hazitoshi.
“Wananchi ni kweli kuwa pesa hazitoshi lakini
kwa hiki kidogo mnachokipata ni vyema mkakitumia kwa malengo mazuri
mliyojiwekea…haipendezi kuona mtu umepewa pesa ili umpeleke mtoto wako shuleni
lakini hufanyi hivyo na badala yake unaenda kutumia kwa ajili ya
ulevi,nawahakikishia kuwa ofisi yangu itafanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhusu
fedha hizi”.alisema Kagoro.
Alisema kushindwa kwa baadhi ya wanufaika
kuzitumia fedha hizo kwa usahihi ndiko kunakopelekea wananchi kuendelea
kuibebesha lawama kila siku serikali kuwa imekuwa haifanyi kitu chochote cha
maana katika kubadilisha pamoja na kuboresha maisha ya watanzania.
Kagoro alisisitiza kuwa kutoka sasa kaya ambayo
itabainika kutumia fedha wanazopewa kinyume na utaratibu basi upo uwezekano wa
kuiondoa ili wapewe wale wenye shida ya pesa hiyo ambayo endapo ikitumika
vizuri inaweza kubadilisha maisha ya wanufaika.
Mwisho.
BAADHI ya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji cha Sululu Halmashauri ya mji wa Masasi wakisubiri kulipwa fedha zinazotolewa na TASAF.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD