Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

WANANCHI 83,798 WA MJI WA MASASI WANATARAJIWA KUANDIKISHWA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Wananchi katika Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara wameaswa kuendelea kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa uandikishaji kwa njia ya kielektroniki BVR.
Zoezi hilo kwa Halmashauri ya Mji wa Masasi lilianza jumatatu April 24 mwaka huu katika kata za Mtandi, Jida, Chanikanguo pamoja na Mkuti na ambalo litadumu kwa muda wa siku saba ili kuwezesha wananchi wote wa kata hizo kuweza kujiandikisha kwa wingi waweze kupata sifa za kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao pamoja na zoezi la kuipigia kura ya ndio au hapana katiba inayopendekezwa.
Halmashauri ya Mji wa Masasi ni miongoni mwa Halmashauri saba zilizopo mkoani Mtwara yenye jumla ya kata 14 ambapo jumla ya wananchi 83,798 wanatarajiwa kuandikishwa kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Akizungumza na Blog ya Mtazamo mpya hii leo Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi Mzenga Twalibu alisema halmashauri yake imeweka utaratibu maalumu katika utekelezaji wa zoezi hilo nyeti na kwamba wameamua kuanza kuandikisha wakazi wa kata nne za Chanikanguo, Jida, Mtandi na Mkuti.
Alisema jumla ya vituo 28 vilivyopo kwenye kata hizo nne za awali viko kwenye zoezi la uandikishaji na kwamba hadi sasa zoezi hilo linaendelea vizuri huku akikiri kuwa ziko baadhi ya changamoto chache zilizojitokeza ambazo ambazo zimekuwa zikipatiwa ufumbuzi wa haraka kutoka kwa wataalamu wa mifumo kwa ngazi ya halmashauri ya mji wa Masasi kwa ushirikiano na wale wa kutoka tume ya Taifa ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Mzenga alisema zoezi hilo kwa kata hizo linatarajia kukamilika april 30 na kwamba kata za Nyasa,Napupa,Marika pamoja na Mumbaka zitafuata na kwamba baada ya kata hizo zoezi hilo litahamia kwa wananchi wa kata za Mkomaindo,Migongo na Temeke.
Kata zingine alizozitaja ambazo zitafuata ili kuhakikisha wananchi wote wa Halmashauri ya mji wa Masasi wanaandikishwa ni pamoja na kata za Sululu, Mwenge Mtapika na Matawale ambako zoezi hilo litafikia mwisho.
“Nitoe wito kwa wananchi wa mji wa Masasi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi hili muhimu kwao na kwa Taifa…wawahi kufika kwenye vituo vyao ambavyo kila mtaa kipo kituo kimoja ambacho wananchi wa eneo husika wanapaswa kwenda kujiandikisha,pia nitoe rai kuwa wananchi wasisubiri hadi siku za mwisho”.alisema Mzenga.
 Kwa upande wake Chatoni  Chatoni ambaye ni mwananchi wa kwanza kuandikishwa katika kituo cha JIDA kata ya Jida halmashauri ya mji wa Masasi alisema vitambulisho hivyo vipya viko tofauti na vile vya awali na kwamba ameipongeza tume ya Taifa ya uchaguzi kwa uamuzi wa kuleta mfumo mpya wa kupata vitambulisho vya wapiga kura.

Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top