TANGAZO
Katibu Tawala (W) Masasi Danford Peter. |
Wakulima wilayani Masasi mkoa wa Mtwara, wamehimizwa
kutumia simu za mkononi na mitandao ya kompyuta kwa kutafuta ushauri wa
kitaalamu wa kilimo na masoko ili kujikwamua na tatizo la ubora na soko la
mazao wanayolima.
Wito huo ulitolewa jana na Katibu Tawala wa wilaya ya Masasi, Danford Peter, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano wa kampuni ya
simu Tanzania (TTCL), katika kata ya Lupaso wilayani Masasi, ambapo
alimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo Bernald Nduta.
Alisema baadhi ya watu wamekuwa
wakitumia vibaya mitandao ya mawasiliano ya kompyuta na simu za mkononi kwa
kueneza ujumbe wa uchochezi na lugha chafu ikiwemo matusi jambo ambalo halileti tija kwao, lakini
alisema kama mitandao hiyo itatumika vizuri inaweza kuwa nyenzo muhimu kwa
maendeleo hasa wakulima.
Aidha, Peter aliwataka wakulima kutumia
simu na mitandao mingine kwa kutafuta masoko ya mazao wanayoyapata kutokana na
kilimo ndani na nje ya maeneo yao wanayoishi kwa ajili ya kupanua wigo wa soko
na kukuza kipato.
Alisema mitandao ni njia mojawapo
ya kutangaza kiasi cha mazao yaliyopatikana hasa mazao ya ufuta, alizeti,
choroko na korosho ambalo ndio zao kuu la biashara kwa mkoa wa Mtwara, na kwa
kufanya hivyo wanunuzi watapa kufahamu wastani wa uzalishaji wa mazao katika
maeneo husika.
“Tunafahamu kwamba korosho ndio zao pekee linalowapatia wananchi
wetu kipato..sasa mitandao hii ni njia mojawapo ya kutangaza kwamba tunakorosho
kiasi gani sisi tuliopo hapa Lupaso, tuna ufuta kiasi gani tuliozalisha, tuna
alizeti kiasi gani tuchozalisha tunahitaji
soko..sasa njia pekee ya kuwasiliana na kutangaza hivyo vitu ni kupitia
mitandao.” Alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa TTCL mkoa wa Lindi
ambae alimwakilisha mkurugenzi wa kanda ya Zanzibar na kusini, Nicodemus Mngulu, alisema kupitia mfuko wa kusimamia utoaji
wa huduma ya mawasiliano kwa wote nchini (UCSAF), kampuni hiyo
ilipewa jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 20 katika awamu
ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa mawasiliano vijijini.
“Katika kata hizo za mwanzo, Lupaso na Lipumbulu ni mojawapo ya
kata zilizonufaika na mradi huo. Hii ni sehemu ya juhudi za serikali
kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano kwa urahisi zaidi na pia kuchangia
ukuaji wa maendeleo katika maeneo ya vijijini.” Alisema Mngulu.
Mnara huo uliozinduliwa unakuwa ni
mnara wa tano wa kampuni hiyo kwa mkoa wa Mtwara, na kwamba unatoa huduma
katika vijiji vitatu vya Lupaso, Mchoti na
Lipumbulu vyenye wakazi
zaidi ya 2,000, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Mwisho.
KAIMU mkurugenzi wa kanda ya
Zanzibar na kusini ambaye pia ni meneja wa TTCL mkoa wa lindi Nicodemus Mngulu,
akimkaribisha mgeni rasimi kuongea na wakazi wa Lupaso muda mfupi kabla ya
kuzindua mnara wa TTCL uliopo kijijini hapo.
Uzinduzi rasmi wa mnara ambapo mwakilishi wa
mkurugenzi wa kanda ya zanzibar na kusini Nicodemus Mungulu na katibu tawala
wa wilaya ya masasi Danford Peter wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi
huo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD