TANGAZO
Na Fatuma Maumba,Mtwara.
Mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA inatarajia kuzima mtambo wa
kurushia matangazo ya luninga kwa njia ya analojia ifikapo May 30 mwaka huu
katika mkoa wa Lindi ili kuhakikisha mikoa yote ya hapa nchini inaingia katika
teknolojia ya kisasa ya dijitali inayotumika kurusha na kupokea matangazo ya
televisheni.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mtwara
mkurugenzi wa idara ya matangazo wa TCRA bwana Gunze Habba alisema katika mkoa
wa Lindi kulikuwa na mtambo wa analojia wa TBC ambao utazimwa na kuwashwa
mtambo wa dijitali wakati katika mkoa wa Mtwara hakukuwa na mtambo wowote wa
analojia.
Gunze alisema mamlaka inaamini kuwa ujio wa wa huduma za
matangazo kwa njia hiyo ya kisasa itaongeza fursa za uwekezaji katika sekta ya
utangazaji kwa wakazi wa mikoa ya kusini.
Alisema mamlaka ya mawasiliano imewaagiza watoa huduma za
kusambaza ving’amuzi walioko mkoani hapa kuhakikisha kunakuwa na ving’amuzi vya
kutosha na kwamba wamefanya ukaguzi katika mji wa mtwara na wamehakikisha kuwa
viko vya kutosha.
Aidha Gunze alitaka itolewe elimu ya kutosha kwa umma kupitia
njia mbalimbali kuhusu kuhamia katika teknolojia ya mfumo wa utangazaji wa
dijitali kutokana wananchi wengi hawana uelewa na maswala hayo.
Kwa mujibu wa Gunze alisema wamiliki wa ving’amuzi wana wajibu
wa kuhakikisha zile chaneli tano ambazo zinazotakiwa kuonekana
ziendelee kuwepo bila kujumuishwa na chaneli za kulipia ambapo amezitaja chaneli
hizo zisizokuwa na ankara ya malipo kuwa ni TBC, Chaneli TEN, ITV, Star TV
pamoja na East Africa Televisheni ili kuwapa uhuru wananchi wasiokuwa na uwezo
wa kulipia ving’amuzi vyao kuweza kupata taarifa mbalimbali.
Utangazaji wa televisheni kwa mfumo wa dijitali ulizinduliwa
rasmi mwaka 2010 baada ya mamlaka ya mawasiliano Tanzania kutoa leseni kwa makampuni
matatu ya kujenga miundombinu yenye kutoa huduma za matangazo ya dijitali
ambapo Desemba 3, 2012 saa sita kamili mitambo ya analojia kwa awamu ya kwanza
ilizimwa katika jiji la Dar es salaam kwa mujibu wa makubaliano ya nchi
wanachama wa jumuiya ya Afrika mashariki na kufuatia mikoa mingine nchini.
Mwisho
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD