TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
WANANCHI wilayani Masasi wametakiwa kutambua mchango walioutoa
waasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar April 26, 1964 na kwamba amani
iliyopo nchini ni matokeo ya muungano huo.
Muungano ni kitendo cha msingi ambapo watanzania wanapaswa
kujifunza kupitia nchi jirani ambazo kwa siku za hivi karibuni zimekumbwa na
machafuko na kwamba hao wanaoukashifu muungano huo wanapaswa kulaaniwa kwa
kutojua thamani ya tendo hilo lililofanywa na waasisi wa n chi ya Tanzania.
Hayo yalisemwa jana na katibu tawala wa wilaya ya Masasi mkoani
Mtwara Danford Peter wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza
kumsikiliza wakati wa maadhimisho ya
kumbukumbu ya sherehe za muuungano ambapo kwa halmashauri ya mji wa Masasi
sherehe hizo zilifanyika kwenye kijiji cha Marika.
Alisema watanzania waliteswa sana kabla uhuru kwa wengine kuuzwa
kama bidhaa sokoni mazingira yaliyopelekea viongozi wetu wa wakati huo akiwemo
mwalimu Nyerere kudai uhuru wa nchi yetu.
Alisema watanzania wengi hasa vijana wanaojiita wa kidijitali
wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu muungano huku wakidai kuwa wakati umefika
wa Zanzibar na Tanganyika kujitenga kitu ambacho amekiri kuwa ni ujinga wa
kufikiri kufanya matendo hayo yasiyo na tija.
Aidha katibu tawala huyo aliwaasa wanafunzi wa shule ya sekondari
ya kutwa ya Marika halmashauri ya mji wa Masasi kutumia vizuri fursa hiyo ya
kusoma waliyoipata katika maisha yao na kwamba endapo wasipofuata maadili na
nidhamu wanaweza kupata matatizo yakiwemo magonjwa ya UKIMWI.
Alisema pia wanapaswa kuzingatia maadili ya dini zao kwa kufuata
maagizo waliyopewa na kwamba wakitaka kutimiza malengo yao ni lazima wazingatie
maelekezo kutoka kwa viongozi wa dini huku akiwakumbusha kutenga muda wao
kusoma vitabu vya dini.
“ Matendo maovu hayakubaliki hata kwa mungu na ndio maana mji wa
Sodoma na Gomora uliangamia kutokana na matendo mabaya waliyoyatenda wanadamu
wa wakati ule ikiwemo zinaa…kumbukumbu ya torati sura ya 28 inazungumzia agizo
alilopewa Musa mtakapokataa kutii amri
ninazowapa leo magonjwa mbalimbali yatawapata ikiwemo ugonjwa wa “ukaufu” ambao
kwa sasa ni sawa na ugonjwa wa
UKIMWI”alisema.
Alisema wakati wa
mbio za mwenge mwanzoni mwa mwezi mei mwaka huu wanatarajia kuzindua mwongozo wa kupambana na mimba za
utotoni na utoro shuleni na kwamba klabu hiyo ni ya wanafunzi wote kwa lengo la kuwafanya
wanafunzi hao kujenga mahusiano ya kuwa
wao ni ndugu moja wanapokuwa shuleni ambapo wanapaswa kusaidiana katika masomo yao
na si kuishi kama wapenzi.
Akizungumzia
kuhusu zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura
linaloendelea wilayani Masasi alisema wananchi w aache kusikiliza na kushabikia mawazo mbalimbali
ya baadhi ya watu wanaofadhiliwa na mashirika ambayo kwa sasa yameamua
kuiharibu dunia watu ambao ni kama vile wamekata tamaa ya maisha.
Alisema katiba inayopendekezwa imeandaliwa na watu makini wenye
mawazo na kwamba wanapaswa kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete kwa kuipigia kura
ya ndio katiba inayopendekezwa kwani imekidhi mahitaji kwa makundi yote.
Aidha alisema kwa sasa kuna wimbi la vijana wengi ambao wamekuwa
wakikutwa kwenye baadhi ya taasisi za dini bila sababu za msingi ambao wengi
wao wamekuwa wakitoka katika maeneo mbalimbali na kwamba amewaasa wazazi
kutokubali kurubuniwa na watu hao wanaokuja na mbinu za kutoa misaada.
“Msidanganyike na msikubali kuingia kwenye huo mtandao mfano ni
nchi jirani ya Kenya ambao kwa siku za karibuni wameingia kwenye hayo matatizo
kutokana na kuruhusu vijana wengi kukaa kwenye kambi mbalimbali zikiwemo
taasisi za dini zisizojulikana…tafadhali msithubutu kushiriki kwenye kambi
hizo”.alisema Peter.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD