TANGAZO
Na Clarence
Chilumba, Masasi.
Sakata la watoto 11 kukutwa
wakiwa nyumbani kwa Alhaj Maulana Shirazi (71) wa
Jumuiya za Wi’yatu LiQadria iliyoko Katika
Kijiji cha Chikundi Halmashauri ya wilaya ya Masasi limechukua sura mpya baada
ya wazazi wa watoto hao kukiri kuwapeleka watoto wao kwa ushawishi walioupata
kutoka kwa Yusuph Hashimu Nakanje mkazi wa kijiji cha Mkululu.
Thawabu Hashimu (43) mama mzazi wa watoto Murji Muhidini (12) pamoja na Marick Muhidini (10) Mkazi wa kijiji cha Mkululu wilaya ya Masasi akiwa nje ya Nyumba yake wakati anaongea na Blog ya Mtazamo Mpya iliyotembelea kijijini hapo kwa lengo la kupata ukweli juu ya sakata la watoto hao.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti na Blog ya Mtazamo Mpya iliyotembelea kijiji cha Mkululu
kilichoko Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wazazi wa watoto hao akiwemo
Thawabu Hashimu (43) ambaye ni mama mzazi wa Murji Muhidini (12) pamoja na
Marick Muhidini (10) alisema watoto hao walipelekwa kwa Alhaj Maulana kwa
shinikizo kutoka kwa kaka yake Yusuph Hashimu Nakanje aliyefahamiana na mzee
huyo.
Alisema watoto wake
waliondoka nyumbani kwake tangu januari mwaka huu na kwamba kwa sasa anachofahamu ni kuwa watoto wake wako
kwa huyo Sheikh Maulana licha ya kukiri kuwa hamjui na hajawahi kumuona na hata
watoto wake wanaendelea vipi hajui zaidi ya kupewa taarifa mara chache kutoka
kwa mjomba yao.
Kwa mujibu wa
Thawabu Hashimu alisema kaka yake Yusuph Hashimu alimweleza kuwa ni vyema
wawapeleke watoto hao kwa mzee Maulana kwa madai ya kuwa anafahamiana nae kwa
kipindi kirefu na kwamba alimwagiza amtafutie watoto 20 yatima ili aweze
kuwalea kwa kuwapa elimu ya Quran.
Alisema mtoto wake
Marick aliacha shule mara baada ya kukataa kurudia darasa la pili baada ya
kufeli mtihani huku mtoto wake Murji alifukuzwa shule kutokana na utoro wa muda
mrefu aliokuwa nao sambamba na kutojua kusoma na kuandika hivyo alipoambiwa
aende shuleni alikataa.
Bibi Mwanahawa Swalehe (62) Bibi wa watoto Mwajuma Selemani (10) na Gadafi Hamis (13) wakati anatoa maelezo kuhusiana na wajukuu zake kuishi kwa mtu ambaye amekiri kuwa hamfahamu.
Kwa upande wake
Mwanahawa Swalehe (62) ambaye ni Bibi wa watoto Mwajuma Selemani (10) na Gadafi
Hamisi (13) alisema wajukuu zake hao walipelekwa kwa mzee huyo kutokana na
shinikizo la mtoto wake kike ambaye ndie mzazi wa watoto hao Asha Hussein
anayeishi Zanzibar kwa sasa.
Alisema chanzo cha
mtoto wake huyo kufahamu taarifa za Alhaj Maulana ni pale alipompeleka mtoto
wake wa kwanza wa kike aitwaye Zainabu Swalehe aliyekuwa anasumbuliwa na tatizo
la akili ambapo baadhi ya watu kijijini hapo walimshauri ampeleke kwa Alhaj
Maulana kwa ajili ya kupata matibabu na ndipo alipopewa taarifa za kuanzishwa
kwa chuo cha watoto hao yatima.
Kwa mujibu wa Bibi
huyo mwenye jina maarufu la “AKU- SOKONI” alisema alimkatalia mtoto wake
asiwapeleke watoto hao lakini mtoto wake alikataa kwa madai ya kuwa mawazo ya
Bibi huyo yamepitwa na wakati na badala yake aendelee kufanya mambo yake
binafsi.
Alisema baada ya
yeye kushindwa kumshawishi mtoto wake alibaki kimya huku akisubiri
kitakachoendelea ambapo mwezi januari mwaka huu wajukuu zake hao walipelekwa
kwa Alhaj Maulana mtu ambaye bibi huyo amekiri kutomfahamu kabisa.
Mama Mdogo wa watoto Mwajuma Selemani pamoja na Gadafi Hamisi Fatuma Jafari akitoa maelezo kwa Blog ya Mtazamo Mpya iliyotembelea kijiji cha Mkululu wilayani Masasi.
Naye Fatuma Jafari
mama mdogo wa watoto hao ambaye ndie aliyewapeleka katika kijiji cha Chikundi
kwa Alhaj Maulana alisema mara kadhaa alimshauri dada yake kusitisha mpango huo
lakini ilishindikana na ndipo alipopewa jukumu la kuwapeleka watoto hao kwa
mzee huyo.
Alisema alipofika
nyumbani kwa Alhaj Maulana aliwakuta watoto wengine aliowafahamu kutoka
kijijini hapo kwenye kitongoji cha Mbalichila anakoishi wakala wa mzee huyo
Yusuph na alipofika alipewa fedha ya nauli kiasi cha shilingi 10000/=.
Alisema ni kweli
hawana mawasiliano na watoto hao huku akikiri kuwa walipanga mwezi huu mwishoni
afanye safari ya kwenda Chikundi kwa ajili ya kuona watoto hao ambao kwa mujibu
wa Fatuma ni kama wamewatelekeza watoto hao kutokana na ubishi wa dada yake.
Hapa ni Nyumbani kwa Bibi yao watoto Mwajuma Selemani na Gadafi Hamisi katika kijiji cha Mkululu wilayani Masasi .
Nyumba hii ni Nyumbani kwa Mama mzazi wa watoto Murji Muhidini na Mariki Muhidini huko katika kitongoji cha Mbalichila katika kijiji cha Mkululu wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Kwa upande wake
mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkululu wilayani Masasi Abdul Chilamula shule
ambayo watoto hao walikuwa wanasoma alikiri kuwa majina ya wanafunzi hao yapo
kwenye kitabu cha usajili licha ya mahudhurio yao ya darasani kuwa duni
kutokana na utoro wa kudumu walionao watoto hao ambapo wao kama shule walikuwa
hawajui ni wapi wanafunzi hao walipo.
Ni Baadhi ya Majengo ya Madarasa ya shule ya Msingi Mkululu, shule ambayo watoto waliokutwa kwa Alhaj Maulana walikuwa wanasoma kabla ya kutoroshwa na wazazi wao na kupelekwa katika Kijiji cha Chikundi-Masasi.
Ikumbukwe kuwa Watoto
waliokutwa jana katika kituo hicho ambao wanatoka ni pamoja na Selemani Juma (12) mkazi wa
kijiji cha Mandawa wilaya ya Ruangwa Jamali Abbasi (12) mkazi wa Mwena Masasi, Karimu Abbasi (17) mkazi wa wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Marick Muhidini mkazi
wa kijiji cha Mkululu wilayani Masasi, Nurudini Ausi (11) kutoka kijiji cha
Mpanyani Masasi pamoja na Ally Bakari (12) mkazi wa kijiji cha Milola mkoani
Lindi.
Wengine ni Gadafi Hamisi (13) kutoka katika kijiji cha
Mkululu Masasi, Bakari Nang’ani (12) mkazi wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Haji
Juma (18) wa kijiji cha Mkululu wilayani Masasi, Mwajuma Selemani (10) wa
kijiji cha Mwena Masasi, Murji Muhidini (12) mkazi wa Mkululu wilaya ya Masasi
pamoja na Hamis Seif (05) mkazi wa kijiji cha Kanyimbi wilayani Masasi katika
mkoa wa Mtwara.
Watoto waliokutwa jana nyumbani kwa Alhaj Maulana huko Chikundi.
Jeshi la polisi wilayani Masasi bado linamshikilia Alhaj Maulana kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tuhuma hizo za kukutwa na watoto kinyume na kanuni na sheria za nchi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD