TANGAZO
Dar es Salaam.
Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kila
mwanachama anapaswa kuwaunga mkono wagombea watakaopitishwa na chama hicho
katika nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwani kinyume chake ni
kukisaliti na adhabu yake ni kufukuzwa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira
alisema mwishoni mwa juma kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi
Mkuu, chama hicho kinahitaji nguvu za pamoja.
“Sisi bado hatujajiunga na Ukawa, hivyo
wanachama wetu wanapaswa kulitambua hilo na kuepuka kushiriki kwenye ushawishi
wa kufanya kampeni za wagombea wa vyama vingine. Hata kwenye katiba yetu
tunasema sasa tunalenga zaidi katika kujiimarisha ili kutoa ushindani mzuri wa
kisiasa katika uchaguzi huu,” alisema.
Katiba ya ACT, imeeleza wazi kuwa pamoja
na sababu nyingine na kwa mujibu wa kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu,
mwanachama yeyote ambaye atasaidia kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la kuunga
mkono chama kingine au mgombea wakati chama kimeweka mgombea wake kwa mujibu wa
sheria za nchi, atakuwa amepoteza uanachama wake.
ACT- Wazalendo tayari imetoa ilani yake
ya uchaguzi ikionyesha kwamba iwapo itaingia madarakani, itawajibika kwa
wananchi kwa kuweka kipaumbele katika maeneo manne ambayo ni hifadhi ya jamii,
uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, afya na elimu.
Kauli hiyo ya ACT linakuja huku kambi
ya vyama kadhaa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
ikiwa kwenye mchakato wa kuunganisha nguvu ili kusimamisha mgombea mmoja wa
urais na kuachiana majimbo katika baadhi ya maeneo.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James
Mbatia amewahi kunukuliwa akisema kuwa umoja huo unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD umehamishia nguvu zake kwenye Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Mbatia alisema tayari umoja huo umeunda
kamati maalumu kutafuta namna ya kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na
kuachiana majimbo.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, alisema tayari kamati zimeundwa na zinaendelea na kazi ya
kuratibu mpango huo mahsusi, unaolenga kuiondoa CCM madarakani.
“Lengo letu ni kuhakikisha Ukawa ina
nguvu ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na katika mpango huo, vyama
vitaachiana majimbo na viti vya udiwani kulingana na nguvu ya chama katika
sehemu husika,” alisema.
Mkakati huo uliopangwa na Ukawa, unaelezwa
na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni kombora kwa CCM, kwani endapo
utafanikiwa, utakiweka chama hicho tawala katika wakati mgumu katika Uchaguzi
Mkuu uliopangawa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Chanzo:Mwananchi.........
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD