TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Wazazi 19 wa wanafunzi walioshindwa
kuripoti kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2014/2015 wamehukumiwa
kifungo cha nje cha miezi mitatu kila mmoja kutokana na kosa la kushindwa
kuwapeleka watoto wao shuleni.
Wazazi waliohukumiwa kifungo hiko ni
wale wa kata za Mpindimbi pamoja na Lukuledi zote zikiwa ni za Halmashauri ya
wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Aidha wametakiwa kuripoti kwenye
mahakama ya mwanzo ya Lisekese Wilayani Masasi kila baada ya wiki mbili wakati
wote watakapokuwa wanatumikia kifungo hiko.
Mbele ya hakimu wa
mahakama ya mwanzo ya Lisekese wilayani Masasi Gloria Mkwera karani wa mahakama
hiyo alidai washtakiwa hao walitenda kosa hilo mwanzoni mwa mwaka huu pale
waliposhindwa kutimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto wao shuleni huku wakijua
ni wajibu wao.
Karani huyo alieleza kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo
umekamilika washtakiwa hao wana
kosa la kujibu na kuiomba mahakama
iwatie hatiani kwa kuwapa adhabu kali
ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotenda vitendo hivyo vinavyowanyima
watoto haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Washtakiwa hao kwa
pamoja walikubali kosa na waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa kuwa wengi
wao ni mara yao ya kwanza kutenda makosa hayo.
Baada ya kusikiliza
maelezo ya pande zote mbili hakimu wa mahakama ya mwanzo ya lisekese Gloria
Mkwera aliridhika na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka na kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa kuwapa adhabu ya
kifungo cha nje cha miezi mitatu kila mmoja .
Katika hatua nyingine
hii leo wazazi watatu wamefikishwa mahakamani kujibu shitaka la kushindwa
kuwapeleka watoto wao shuleni.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD