TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Jeshi la polisi wilayani masasi limejipanga kuimarisha
ulinzi dhidi ya uhalifu katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye sikukuu ya
Pasaka kwenye maeneo yote ya mikusanyiko ya watu ikiwemo kwenye nyumba za ibada,kumbi
za starehe pamoja na barabarani.
Aidha taarifa ya jeshi hilo ilisema kwamba uzoefu unaonesha
kuwa wakati wa sikukuu kumekuwa na matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwa ni
pamoja na uporaji unaotokana na wahalifu hao kutumia mwanya huo pindi waumini
wanapokuwa kwenye nyumba za ibada wakati wa usiku.
Akitoa taarifa hiyo leo kaimu mkuu wa jeshi la polisi wilaya ya Masasi
mkoani Mtwara ambaye pia ni mkuu wa upelelezi wilaya ya Masasi Nathaniel Kyando
alisema vikosi vyake vimejipanga kusimamia amani na usalama wa raia na mali zao
katika kuhakikisha kuwa kipindi hicho chote kinamalizika kwa amani na usalama.
Alisema wananchi pia wana wajibu wa kushirikiana na jeshi la
polisi kufichua wahalifu wote mazingira yatakayopelekea kusherehekea sikukuu
hizo kwa amani.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa polisi alisema kuwa madereva
bodaboda pamoja na magari ya watu binafsi na abiria wazingatie sheria za
usalama barabarani kwa kuwa kipindi hicho watoto wengi huachwa na wazazi wao
kwenye maeneo ya burudani.
Aidha alitoa wito kwa wazazi wilayani humo kutowaacha watoto
wao ovyo wakizurura mitaani,kwenye kumbi za burudani pamoja na michezo mingine
na badala yake wawe na utaratibu maalumu dhidi ya watoto wao ili kuepusha
athari zinazoweza kujitokeza.
Alisema waumini wa madhehebu yote nao pia watumie muda huo
kuiombea amani wilaya ya Masasi na Taifa kwa ujumla katika kipindi hiki cha
sikukukuu ya ufufuko wa yesu kristo.
Katika hatua nyingne Kyando amewaasa wananchi wa mji wa
Masasi mkoani Mtwara kuchukua tahadhari ya watu wenye tabia za kitapeli ambao
wamekuwa wakiwadanganya watu kwa njia ya mtandao kuwa watawapa fedha kutoka
kupitia bahati nasibu mbalimbali.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD