TANGAZO
Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi
ya China Ralway Jiachang Engineering (CRJE) ambao wamepewa tenda ya kujenga
jengo la ghorofa 6 za Mfuko wa Pensheni wa Hifadhi ya Jamii (PPF),
mkoani Mtwara, wamegoma kufanyakazi hadi hapo kampuni hiyo itakapowaongezea
fedha wanayotaka walipwe.
Akizungumza na waandishi wa habari
kwa uchungu wa hali ya juu Mwenyekiti wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Innocent
Mangapi, alisema malalamiko yao yaliyopelekea hadi kugoma kufanya kazi ni
kutokana na ujira mdogo wanaolipwa na Kampuni hiyo na ukizingatia
kwa sasa gharama za maisha zimepanda tofauti na zamani.
Innocent alisema kuwa wameamua kugoma toka
wiki iliyopita kuishinikiza kampuni hiyo kuongeza kiwango cha malipo kwa
wafanyakazi hao kutoka shilingi. 8,000 hadi shilingi. 15,000 kwa fundi wa
ujenzi na wasio na ujuzi kutoka 5,000 hadi 12,000.
Alisema machi tano mwaka huu
walikutana na uongozi ambao unaowaunganisha kati yao na
kampuni ya CRJE ili kuomba wawaongezee posho na wakaahidiwa
kuwa wataongezewa lakini hadi kufikia
machi 11 mwaka huu hawajaongezewa posho.
“Baada ya kubaini kuwa hawa jamaa ni
wababaishaji tarehe hiyo hiyo tulifanya mgomo na baadae watu
wa Wizara ya Kazi na Ajira, kupitia Idara ya Usimamizi wa Kazi na Huduma za
Ukaguzi mkoa wa Mtwara, wakaja hivyo basi katika kufanya mgomo huo tulikubliana
nao tukiwa kama sisi wafanyakazi wakiwemo Idara ya Kazi pamoja na
Kampuni ya CRJE kufikia Machi 20 mwaka huu iwe mwisho wa kulipa ule mshahara
mdogo ambao serikali hautaki,” alisema Mangapi.
Kwa mujibu wa Mangapi alisema Machi
23 mwaka huu wafanyakazi wa Kampuni ya CRJE walipokea barua kutoka Idara ya
Kazi Mkoa ikiainisha mapungufu yaliyopo kwa kampuni ya CRJE ili yafanyiwe marekebisho
huku sehemu ya barua hiyo ikisema:
“ Wafanyakazi kulipwa malipo ya
mishahara chini ya kiwango ambacho kimeanishwa katika tangazo la Serikali
Na.196 la 2013, kuanzia tarehe 28/03/2015 unatakiwa uanze kuwalipa
wafanyakazi wenye ujuzi shilingi. 15,000 kwa siku na wasio na ujuzi ni shilingi,
12,000 kwa siku hivyo ni viwango vya chini na ukiwa kama muajiri
unaruhusiwa kuongeza na siyo kupunguza, ilisomeka sehemu ya barua hiyo
kutoka Wizara ya kazi na Ajira”.
Lakini katika hali isiyo ya
kawaida wafanyakazi hao walisema uongozi
wa kampuni hiyo umekataa kuwalipa kiasi kilichosemwa na Idara ya Kazi ambapo
walisema kuwa wao wanaendelea na mgomo hadi hapo kampuni hiyo itakapokubali
kuwaongezea kiasi kinachotakiwa.
Hata hivyo mwandishi wa Blog ya Mtazamo Mpya alipotaka kuongea
na Viongozi wa Kampuni ya CRJE hawakuweza kupatikana mara moja kutokana na
viongozi hao kujifungia ofisini.
Aidha wafanyakazi hao wamelalamikia kutolipwa
wanapofanya kazi muda wa ziada na walipanga leo jumatatu kwenda kuonana na Mkuu
wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego kumlalamikia kilio chao.
Mwisho.
Wafanyakazi wa Kampuni ya CRJE wakiwa nje ya jengo la kampuni
hiyo baada ya kufanya Mgomo ulioanza wiki iliyopita.
|
Ofisi ya Kampuni ya CRJE ambamo ndani yake ndimo jengo la PPF
linajengwa na Wafanyakazi hao.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD