TANGAZO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kijiji cha Namahema-Ruangwa.
Na Mwandishi Wetu,Ruangwa.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali
inatarajia kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Nanganga, Ruangwa
hadi Nachingwea. Hatua hiyo itawezesha kutatuliwa kwa kero ya barabara
inayowakabili wananchi wa wilaya za Ruangwa na Nachingwea kwa muda mrefu.
Majaliwa amesema barabara hiyo ambayo kwa sasa haipo
katika hali nzuri itajengwa kwa kiwango cha lami. Serikali inatarajia kuanza
kuifanyia upembuzi yakinifu katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Aliyasema hayo juzi alipozungumza kwa nyakati tofauti
na wananchi wa vijiji vya Likunja, Nkowe na Namahema katika mikutano ya hadhara
aliyoifanya wilayani Ruangwa wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi.
Alisema serikali imejipanga katika kuboresha miundombinu
ya barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwamba mara baada ya kumalizika
kwa upembuzi yakinifu, ujenzi wa barabara hiyo utaanza, hivyo amewataka
wananchi kuwa na subira.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amewataka wananchi wa
vijiji hivyo kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuweka kando itikadi
zao za kisiasa kwa sababu uchaguzi ulishamalizika tangu Oktoba 25 mwaka jana.
“Mimi nitaendelea kuwaheshimu, kuwasikiliza na
kuwahudumia, nawaomba tushirikiane na tuweke kando masuala ya itikadi za vyama,
sasa ni wakati wa kazi, hivyo ni bora tukashirikiana kufanya kazi kwa maendeleo
ya Ruangwa jambo ambalo linawezekana.
Hata kama wewe ambaye najua ulinichukia, mimi
nimekusamehe kutoka moyoni, wewe ni wangu hata kama hukunichagua nitakuhudumia
na kukutumikia kwa sababu mimi ndiye mbunge wako hivyo naomba tushirikiane,”
alisema Majaliwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya
Ruangwa, Rashid Nakumbya aliomba wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana kwa pamoja
kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya wilaya yao iweze kupiga hatua.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea Soko Kuu la Wilaya ya Ruangwa kukagua hali ya upatikanaji na bei za vyakula akiwa katika ziara ya jimbo hilo mkoa wa Lindi jana. (Picha na Ofisi ya waziri mkuu)
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD