TANGAZO
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa K. Majaliwa.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema
shule za sekondari za Kata zina fursa ya kufanya vizuri kama zilivyo shule
nyingine, licha ya kuwa watu wengi wanazidharau. Alitoa kauli hiyo juzi wakati
akikabidhi zawadi ya kompyuta mpakato kwa mwanafunzi aliyeshinda shindano la
kuandika insha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kompyuta hiyo ina thamani ya Sh milioni
1.9. Mwanafunzi huyo, Jabir Mandando, amehitimu kidato cha nne katika shule ya
sekondari ya Mbekenyera iliyoko wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Alipata ufaulu
wa daraja la pili na sasa anasubiri matokeo ya kujiunga na kidato cha tano.
Mandando aliandika insha hiyo wakati akiwa kidato cha nne mwaka jana.
“Huyu ni mtoto wa kijijini tu. Anatoka
kijiji cha Namilema wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi. Shule ya Mbekenyera
aliyosoma ni shule ya Kata. Ameweza kushinda tuzo na kushika nafasi ya tatu
katika shindano lililoshirikisha shule nyingi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki,”alisema.
Alieleza kuwa mwanafunzi huyo licha ya
kutoka katika shule ya Kata aliweza kuchomoza kitaifa katika shindano la
kimataifa. “Nimeamua kumpa zawadi hii aweze kujisomea zaidi na kupata elimu ya
masuala mbalimbali kwa kutumia kompyuta hii. Pia nataka iwe chachu kwa vijana
wengine kushiriki mashindano kama haya,” Waziri Mkuu alisema.
Aidha, alimkabidhi Mwalimu Mkuu wa shule
hiyo, Shanael Nchimbi fedha taslimu Sh 500,000 zikiwa ni zawadi kwa ajili ya
shule hiyo. Mwalimu Nchimbi alimsindikiza mwanafunzi huyo Arusha kupokea zawadi
hizo katika mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
uliomalizika jijini humo wiki iliyopita.
Kwa upande wake, Mandando alimshukuru
Waziri Mkuu kwa zawadi na kuahidi kuongeza bidii katika masomo yake ya kidato
cha tano na cha sita, ili ndoto yake ya kuwa daktari itimie. Alipoulizwa
alipataje taarifa ya uwepo wa shindano hilo, alisema: “Walimu walipata taarifa
wakazileta darasani na kutuambia tushiriki kuandika. Walizikusanya na kuchagua
tatu bora, ndipo yangu ikashinda.”
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD