TANGAZO
DIWANI wa kata ya Mangaka Halima Mchoma akikabidhi vitabu kwa mmoja wa walimu wakuu wa shule za msingi nne za kata ya Mangaka hii leo kwenye viwanja vya shule ya msingi Mangaka.
Na Clarence Chilumba, Masasi
DIWANI wa kata ya Mangaka
jimbo la Nanyumbu mkoani Mtwara, Halima Mchoma amenunua vitabu 488 vya masomo
ya sayansi na stadi za kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 1,157,000/= kwa
wanafunzi wa darasa la nne wa shule za msingi za kata hiyo.
Shule zilizonufaika na msaada
huo ni pamoja na shule ya msingi Mangaka,Nahawara,Ndwika 2 na Mtokora ambazo
zote ni kutoka katika kata ya Mangaka Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani
Mtwara.
Vitabu alivyovinunua diwani
huyo ni pamoja na vitabu 388 vya somo la
sayansi,vitabu 100 vya somo la stadi za kazi pamoja na boksi nne za peni zenye
peni 400 ambazo watapewa walimu wa shule za msingi katani humo.
Diwani huyo ameamua kununua
vitabu hivyo pamoja na peni kwa walimu
wote wa kata hiyo kwa fedha zake za mfukoni kwa lengo la kuunga mkono jitihada
za serikali ya awamu ya tano ya kutoa elimu bila malipo.
Akizungumza leo wakati wa
kukabidhi msaada huo kwa walimu wakuu wa shule hizo katika viwanja vya shule ya
msingi Mangaka alisema ameamua kununua vitabu vingi vya sayansi kutokana na
ugunduzi wa gesi mkoani humo ambao wengi wa wataalamu wanaohitajika ni wale
waliosoma masomo ya sayansi.
Alisema kutokana na kero ya upungufu
wa vitabu kwenye kata hiyo waliyokuwa wanailalamikia walimu ndicho
kilichomsukuma kuamua kununua vitabu hivyo ambapo kwa sasa kila mtoto wa darasa
la nne atatumia kitabu kimoja kama inavyotakiwa kitaalamu.
Mchoma alisema kwa vitabu vya awamu ya kwanza alivyonunua vina thamani
ya sh.1.2 milioni na kwamba lengo lake kwa sasa ni kutatua changamoto zilizopo
kwenye shule hizo ikiwemo upungufu wa madawati,matundu ya vyoo,vyumba vya madarasa
pamoja na nyumba za walimu.
“Nimeguswa na tatizo la
wanafunzi wa kata yangu kutumia kitabu
kimoja zaidi ya wanafunzi wawili…ndio maana nimeamua kununua vitabu hivi
ambavyo kwa sasa naamini kila mwanafunzi anayesoma darasa la nne kwenye kata
hii atatumia kitabu chake na nitafanya
hivi kwa kipindi chote cha uongozi wangu ndani ya miaka mitano,”alisema Mchoma.
Alisema pia amefanya uamuzi
huo baada ya kuguswa na namna walimu wa kata hiyo wanavyojituma katika
kufundisha kunakopelekea shule za kata hiyo kufanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani
mbalimbali ikiwemo yale ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2015.
Kwa upande wake ofisa elimu taaluma wa shule
za msingi wilayani Nanyumbu Stephen Urassa alimpongeza diwani huyo kwa namna
alivyoonesha njia na kwamba msaada huo umekuja wakati muafaka ambao wanafunzi wa
darasa la nne wanajiandaa kufanya mitihani ya majaribio.
“Nimekuwa Halmashauri ya
wilaya ya Nanyumbu tangu mwaka 2008…lakini sijawahi kuona kiongozi yeyote wa
kisiasa akitoa msaada wa vitabu kwa wanafunzi wa shule za msingi hivyo hii
inaonesha ni kwa namna gani wananchi wa kata ya Mangaka hawakufanya makosa
kukuchagua”.alisema Urassa.
Naye mratibu elimu kata wa
kata ya Mangaka Fidelis Hokororo alisema kata hiyo ina jumla ya wanafunzi 253
wa darasa la nne ambapo kutokana na msaada huo kwa sasa kila mwanafunzi wa darasa
la nne atakuwa anatumia kitabu kimoja cha sayansi huku vitabu 135 vikiwa
zidifu.
Alisema kwa upande wa vitabu
vya stadi za kazi ambavyo ni 100 kwa wastani kila wanafunzi watatu watakuwa
wanatumia kitabu kimoja na kwamba watatumia baadhi ya vitabu vilivyopo kwenye
shule hizo ili kufikia lengo la kila mwanafunzi kutumia kitabu kimoja.
BAADHI ya wanafunzi wa darasa la nne wa shule ya msingi Mangaka wakifurahia msaada huo wa vitabu kutoka kwa diwani wa kata hiyo.
MWENYEKITI wa kijiji cha Nahawara kata ya Mangaka Rukia Ismail Makarani akizungumza wakati akitoa shukrani zake baada ya diwani wa wa kata ya Mangaka kutoa msaada wa vitabu kwa wanafunzi wa darasa la nne.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD