TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Watu wawili wanaume wamefariki dunia papo hapo mara baada ya kugongwa na
gari aina ya Scania karibu na stendi kuu ya mabasi katika makutano ya barabara kuu ya
Lindi-Tunduru na Newala mkoani Mtwara.
Waliofariki kwenye ajali hiyo ni pamoja na aliyekuwa mhandisi wa maji wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara John Majura (39) pamoja na mlinzi wa Halmashauri hiyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kutokana na mwili wake kuharibika vibaya.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara
Henry Mwaibambe alisema ajali hiyo mbaya ilitokea jana majira ya saa 2:00 usiku
katika makutano ya barabara kuu itokayo wilaya za jirani za
Tunduru,Nachingwea,Newala na ile inayotoka mkoani Lindi jirani kabisa na kituo
kikuu cha mabasi mjini humo.
Aliwataja waliofariki kuwa ni pamoja na John Majura (39) aliyekuwa mhandisi wa maji wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkazi wa Musoma na mlinzi wa lango kuu la kuinglia ofisi za halmashauri hiyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata kichwani.
Alisema Majura alikuwa anatokea kazini kwa kuwa usiku huo kulikuwa na
kikao cha dharura cha kujadili mambo mbalimbali ya maenndeleo ya halmashauri
hiyo na kwamba alipakiwa kama abiria na mlinzi huyo kuelekea nyumbani kwao
maeneo ya Mtandi mjini hapa.
Alisema walipofika eneo la makutano ya barabara kuu za wilaya jirani na
mkoa wa Lindi ghafla lilitokea gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 983
ATN mali ya Iddi Kalinga mkazi wa Songea likiendeshwa na na dereva Ahmad Mkwepu
(32) mkazi wa Mfaranyaki-Songea na kuwagonga na hatimaye kufariki dunia papo
hapo.
Kamanda Mwaibambe alisema marehemu wote wawili walikuwa kwenye pikipiki
aina ya SANLG yenye namba za usajili MC 997 AHZ iliyokuwa ikiendeshwa na kijana
huyo mlinzi ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja licha ya kuwepo
taarifa kuwa ni mkazi wa mtaa wa Nyasa mjini Masasi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi alisema chanzo cha ajali hiyo bado
kinachunguzwa na kwamba watatoa taarifa baadae huku derava wa gari hiyo kwa
sasa anashikiliwa na jeshi la polisi wilaya ya Masasi kwa mahojiano zaidi.
Miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika hospitali ya Mkomaindo
Halmashauri ya mji wa Masasi na kwamba mwili wa marehemu John Majura utaagwa
hii leo mjini Masasi tayari kwa kusafirishwa baadae majira ya saa 9:00 jioni
kuelekea huko nyuumbani kwao Musoma.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD