TANGAZO
NAIBU
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya
NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella
Manyanya amesema kuanzia mwakani serikali itawafukuza kazi walimu wakuu wa
shule zote za msingi ambazo wanafunzi wake wa Darasa la Tatu watashindwa
Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Alitoa kauli hiyo jana wilayani Bagamoyo wakati akipokea
madawati 1,000 kutoka kwa Kampuni ya mafuta ya Total yenye thamani ya Sh
milioni 78 kwa ajili ya shule 10 za msingi za Bagamoyo na Dar es Salaam.
Manyanya alisema hatua hiyo itawezesha kuboresha elimu na pia
kuongeza uwajibikaji kwa walimu katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata
elimu stahiki na kwa wakati unaotakiwa.
Alisema katika hali ya kawaida wanafunzi wanapaswa kujua kusoma,
kuandika na kuhesabu kuanzia ngazi ya chekechea na wawe mahiri katika masomo
hayo wafikapo Darasa la Tatu.
“Ni fedheha unamkuta mwanafunzi wa darasa la tatu hajui kusoma
kwa nini? Lazima kuna uzembe ma hali sasa hili ni agizo na utekelezaji wake
unaanza… tutapita huko kwenye mashule kukagua hili, tukibaini wapo wanafunzi hawajui
hizi KKK hatuna sababu ya kuendelea na huyo mwalimu mkuu.
“…Tutamwambia atupishe akafanye shughuli nyingine, lazima walimu
wawajibike,” alisema Manyanya baada ya kuwapa karatasi wasome na kuhesabu
baadhi ya watoto wa shule za msingi waliokuwepo kwenye hafla hiyo na kusema
elimu bora ni pamoja na kujua kusoma, kuandika, kuhesabu na kuelewa.
Naibu Waziri huyo pia aliipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania
(TEA), kwa kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia katika elimu hasa suala la
madawati, ujenzi wa mabweni huku akisema taifa lina upungufu wa madawati
1,349,090 ambayo gharama yake ni Sh bilioni 182.1 hivyo aliwaomba wadau wa
elimu kuchangia.
Akizungumza kabla ya kukabidhi madawati hayo, Makamu wa Rais wa
Kampuni ya Mafuta ya Total, Jean-Christian Bergeron alibainisha kwamba kwa
miaka mitatu kampuni yake imechangia madawati 3,000 yenye thamani ya Sh milioni
234 ambapo wanafunzi 9,000 wamenufaika nayo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD