TANGAZO
Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
WAZIRI Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa
amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu watambue jukumu walilonalo la
kuwahudumia wananchi kutokana na majukumu ya ofisi hiyo yanayogusa maisha ya
kila siku ya Watanzania.
“Ofisi ya Waziri Mkuu
ni kubwa na pana sana na inahusika na shughuli za kila siku za Watanzania. Kwa
hiyo tuna kazi kubwa ya kukidhi matarajio yao,” alisema Majaliwa. Alitoa kauli
hiyo jana mchana wakati akizungumza na wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi
wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye mkutano uliofanyika ofisini kwake, Magogoni,
jijini Dar es Salaam.
Jana ndiyo aliripoti
kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa Ijumaa iliyopita kwenye Ikulu ya Chamwino
mkoani Dodoma. “Pamoja na kazi nyingine, tunayo majukumu makubwa ambayo ni
udhibiti, usimamizi na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali humu serikalini.
Ninatarajia kupata
mpango kazi kutoka kwa Mkuu wa kila idara na kila taasisi zilizo chini ya Ofisi
ya Waziri Mkuu. Nitakwenda pia ofisi za Tamisemi ili kuweka vipaumbele vyetu
sawa,” alisema.
Aliwataka watumishi hao
wawe tayari kutekeleza kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo imekuwa ikisisitizwa
na Rais John Magufuli ili kumudu kasi ya utendaji kazi Serikalini ambayo
anahimiza hivi sasa. Alisema ana imani kuwa watumishi hao watampa ushirikiano
kama ambavyo walikuwa wakiutoa kwa mtangulizi wake, Mizengo Pinda ambaye
amestaafu hivi karibuni.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD