TANGAZO
RAIS Dk John Magufuli
amewataka Watanzania wa dini zote na viongozi wa dini kutoka madhehebu
mbalimbali, kuendelea kumuombea ili atekeleze ahadi alizozitoa pamoja na kuinua
maisha ya Watanzania.
Dk
Magufuli aliyasema hayo kwenye Ibada ya Mavuno iliyofanyika katika Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam jana.
Aliwashukuru pia wananchi wote waliomuombea na kufanikisha kuchaguliwa kuwa
Rais wa Tanzania wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika
siku ya nne akiwa ofisini na Jumapili yake ya kwanza tangu alivyoapishwa kuwa
Rais wa Tanzania, aliwasili kanisani hapo saa 12.50 asubuhi akiambatana na
mkewe, Janet. “Natoa shukurani kwa Watanzania wote wenye imani za kidini tofauti
kwa sala zao.
Nawaomba
waendelee kuniombea ili niweze kutekeleza ahadi nilizotoa, lakini pia niinue
maisha ya Watanzania,” alisema Dk Magufuli alipopewa nafasi ya kuzungumza.
Alisema anaamini kuwa ana deni kubwa kwa Watanzania hivyo aliahidi kufanya kazi
kwa bidii na kuboresha utoaji wa huduma kama njia ya kutimiza wajibu wake kwao.
“Sala
zenu ni muhimu sana, zitaniwezesha kufikisha nchi yetu katika hatua nyingine
bora zaidi,” alisisitiza. Awali, wakati akimkaribisha kanisani hapo, Mwenyekiti
wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Dk Adelhelm Meru, alisema kwa kawaida Watanzania
na Waafrika kwa ujumla wana utamaduni wa kutoa shukurani pale wanapopata
mafanikio.
“Huu
ni utamaduni tuliorithi tangu vizazi na vizazi ndio maana nakuomba leo
mheshimiwa Rais, uje usalimie katika mkutano huu,” alisema Dk Meru ambaye pia
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Dk Magufuli ni mmoja wa
waumini katika parokia hiyo ya Mtakatifu Petro kama ilivyokuwa kwa Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD