TANGAZO
Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi (Mbunge) Dkt.shukuru Kawambwa (picha ya maktaba).
Lengo la mradi ni kufikia
wasichana 10,200 kwa mikoa ya Lindi na Mtwara
Tatizo la watoto wa kike mkoani Mtwara
kukatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali limepungua kwa kiasi kikubwa,
baada ya uwapo wa mradi wa `Hakuna wasichoweza’ unaoendeshwa na T-Marc kwa
ufadhili wa Vodacom Foundation.
Mradi huo umeonyesha mwelekeo wa kutatua matatizo
yanayowakabili watoto wa kike kutotimiza wajibu wao wa masomo shuleni ikiwa ni
pamoja na kutotimiza ndoto zao sambamba na kupunguza utoro.
Akizungumza wakati wa mrejesho wa mwenendo wa mradi huo kwa wadau
wa elimu wa Mkoa wa Mtwara, Meneja wa mradi huo, Doris Chalambo, alisema mradi
huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2013 mkoani humu, ulilenga kufikia wanafunzi
10,200 wa shule za msingi kuwapatia elimu ya afya, namna ya kujisitiri wakati
wa siku zao na kupatiwa vifaa vya kujisitiri.
Alisema katika thamini yake iliyotolewa chini ya utekelezaji
wake kwa mkoani Mtwara, umeonyesha kuwa na mafanikio makubwa baada ya kupunguza
tatizo la utoro.
“Lengo la mradi ni kufikia wasichana 10,200 kwa Mikoa ya Lindi
na Mtwara, lakini kwa Mkoa wa Mtwara wanafunzi wapatao 7,077 tayari wamefikiwa
na tumekuwa tukiwapatia elimu juu ya wanapokuwa kwenye siku zao itakayomsaidia
anapokuwa katika hali hiyo afanye kitu gani pamoja na elimu ya afya na madhara
ya mimba za utotoni sambamba na kumsaidia vifaa vya kujisitiri na hii ni
kutokana na kuwa suala hilo halizungumziwi kabisa katika jamii yetu hivyo mtoto
anapata changamoto na kumsababishia kukosa shule kati ya siku mbili hadi tano
ndani ya mwezi mmoja na kumrudisha nyuma kielimu,” alisema Chalambo.
Aidha, alisema changamoto wanazokumbana nazo katika kutekeleza
mradi huo ni pamoja na baadhi ya shule kukosa miundombinu kama vyoo na chumba
maalum kwa ajili ya kusaidia wasichana katika masuala ya afya na kuwa
mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili ikiwa awamu ya pili itakuwa mkoani
Lindi.
“Katika kutekeleza mradi huu, hatuwezi kufanikiwa bila ya
miundombinu, tumegundua shule nyingi vyoo siyo vizuri kwa hiyo bila kuendana na
miundombinu sahihi hatuwezi kufanikiwa,” alisema Chalambo.
Akizungumza kwa niaba ya katibu tawala Mkoa wa Mtwara, Jose
Kitenana, alisema mradi huo umeleta mabadiliko katika mkoa huo na kuwa serikali
imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha miundombinu ya shule inakuwa rafiki.
“Mpango huu ni mzuri na kwa sisi serikali hatuwezi kufanya kila
jambo, hivyo kuna wadau tunashirikiana nao kama T-Marc kutoa elimu ya afya kwa
wanafunzi kwa udhamini wa Vodacom Foundation ili kusaidia watoto wetu wa kike
na suala la miundombinu bado zipo taratibu zinazofanyika kuhakikisha
wanajengewa mazingira rafiki,” alisema Kitenana.
Naye Mkuu wa Vodacom Foudation, Renatus Rwehikiza, alisema
wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali kwenye jamii katika vipengele tofauti na
sasa wanatekeleza mradi wa `hakuna wasichoweza’ kwa lengo la kuongeza
mahudhurio ya watoto shuleni na kuwa itapunguza kasi ya magonjwa, utoro na
mimba za utotoni.
Mmoja wa wanafunzi, Doreen Mvungi, alisema mradi huo umewapa
maarifa namna ya kukabiliana na changamoto walizokuwa wakizipata pindi
wanapokuwa kwenye siku zao.
CHANZO: NIPASHE.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD