TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Mkuu wa wilaya ya Masasi
mkoani Mtwara Bernald Nduta amewataka watendaji wa serikali kuwa na nidhamu
kazini ikiwa ni pamoja na kuwahi kazini,kutenda haki kwa wananchi
wanaowahudumia ili kuondoa malalamiko ya wananchi kwa serikali yao.
Wito huo ameutoa wakati
anafungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi
mkoani Mtwara kwenye ukumbi wa chuo cha maendeleo ya wananchi Masasi ambapo
alisema baadhi ya watendaji wa serikali waliopewa dhamana wamekuwa wakifanya
kazi kwa mazoea.
Alisema ili Taifa la
Tanzania lisonge mbele kimaendeleo ni lazima watendaji wa serikali wafanye kazi
kwa bidii kwani wao ndio dira na muongozo katika maeneo yao ya kazi lakini hali
ni tofauti na ilivyo sasa kwani watendaji wengi wamekuwa ndio kikwazo cha
maendeleo kwa kutumia muda mwingi kufanya mambo yao binafsi.
Alisema watendaji wengi wa
serikali na wananchi kwa ujumla kila uchao wamekuwa wakiilalamikia serikali
huku wao wakishindwa kutimiza wajibu wao kwa taifa ambapo alisema baadhi ya
nchi ambazo hii leo watanzania wengi wamekuwa wakidai zina maendeleo kuliko
Tanzania ukweli ni kwamba wananchi wake wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii.
“Ndugu zangu watumishi wa
umma mliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi na taifa letu…kwa mfumo huu wa
maisha tulionao watanzania wengi kamwe hatuwezi kupiga hatua kimaendeleo na
kila siku tutabaki kuilalamikia serikali kuwa haifanyi kazi wakati sisi wenyewe
ni sehemu ya serikali”alisema Nduta.
Awali akimkaribisha mkuu wa
wilaya kuzungumza na wafanyakazi hao,mkuu wa chuo cha maendeleo ya wananchi
Masasi Fred Mwakagenda alisema baraza hilo la wafanyakazi ni la aina yake
kufanyika kwa kuwa mara nyingi hufanyika kikanda ambapo ni wawakilishi wachache
huweza kuhudhuria tofauti na hivo lilivyofanyika kwa kuwa limetoa fursa kwa
wafanyakazi wote kushiriki.
Alisema lengo la baraza
hilo ni kujifunza masuala mbalimbali kutoka kwa wataalamu watoa mada,kujenga
mahusiano miongoni mwa wafanyakazi,kubadilishana uzoefu uliopo pamoja na
kuangalia kwa pamoja fursa zilizopo na changamoto zilizopo ili wafanyakazi
waweze kufanya kazi kwa moyo wa kizalendo.
Kwa mujibu wa Mwakagenda alizitaja
changamoto kadhaa zinazovikabili vyuo vya maendeleo ya wananchi mkoani Mtwara
kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha za uendeshaji (Ruzuku) kutoka
wizarani,ucheleweshaji wa kulipwa madai mbalimbali kwa watumishi wa vyuo
hivyo,ucheleweshaji wa kupanda madaraja pamoja na watumishi wapya kutopata
mafunzo maalumu pindi wanapoanza kazi.
Alisema ni vyema serikali
ikaangalia kwa undani zaidi malalamiko yao ambayo mengi ni ya muda mrefu ili
kurejesha imani kwa watumishi hao wa vyuo vya maendeleo ya wananchi ambavyo
hufundisha stadi mbalimbali kwa vijana wengi ili waweze kujiajiri kwenye sekta
binafsi na kuachana na dhana ya kuitegemea serikali katika kutoa ajira.
Mkutano huo wa baraza la
wafanyakazi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi mkoa wa Mtwara ulihudhuriwa na wafanyakazi
kutoka vyuo vya Mtawanya,Newala na Masasi huku mada mbalimbali zikiwasilishwa
kutoka kwa wataalamu wa mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo PSPF,NSSF na
NHIF,wataalamu wa tume ya usuluhishi na uamuzi wa migogoro kazini (CMA) pamoja
na maofisa wa TUGHE mkoa wa Mtwara.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD