TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Nachingwea.
BAADHI ya wananchi
wilayani Nachingwea katika mkoa wa Lindi wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu ni
Rais gani wanamuhitaji katika serikali ya awamu ya tano inayotarajiwa kupatikana
baada ya uchaguzi mkuu ujao oktoba mwaka huu.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti na Blog ya Mtazamo Mpya wananchi hao wameelezea wazi kuwa Rais
ajaye anapaswa kusikiliza kero mbalimbali zinazotolewa na wananchi hasa katika
kipindi hiki ambacho vyama vya siasa vinaomba kura kutoka kwa wananchi ili
watakapochaguliwa watekeleze ahadi zao.
Akizungumza na Blog
ya Mtazamo Mpya jana kijijini hapo Ahmad Yasin Chibwana (60) mkazi wa kijiji cha
Kilimarondo,kata ya Kilimarondo wilaya ya Nachingwea ambaye pia ni mjumbe wa
mkutano mkuu wa mkoa (CCM) alisema Rais ajaye aimarishe amani iliyopo kwa sasa
nchini.
Alisema uchaguzi wa
mwaka huu ni wenye ushindani mkubwa kutokana na kila chama cha siasa kujiandaa
vyema kwa sera na mikakati yake endapo kitapewa ridhaa kutoka kwa watanzania na
kwamba ni kazi ya wananchi kupima na kuchagua ni chama kipi ama mgombea yupi
anafaa kuongoza.
Alisema Rais ajaye
anapaswa kutilia mkazo suala la kilimo ambalo kwa siku za hivi karibuni
halijapewa kipaombele kwa kuwa watanzania walio wengi ni wakulima ambao hadi
sasa wanategemea kilimo cha mkono ambacho hakina tija.
“Serikali inaweza
kabisa kukifanya kilimo kuwa chenye tija…mfano mimi nakumbuka katika miaka ya
1970 marehemu mzee Rashid Mfaume Kawawa alipokuwa mbunge wa jimbo la Nachingwea
alitoa agizo la wananchi kuondoa miti na visiki kwenye mashamba yao na yeye
akaleta matrekta na wananchi tulipata mavuno mengi viongozi wa sasa wananshindwa
nini? Alisema Chibwana.
Kwa mujibu wa
Chibwana alisema wagombea na vyama vyote wamekuwa wakitoa ahadi luluki kwa wananchi kwa lengo la kuwashawishi
wawapigie kura ambapo ukweli ni kwamba ahadi zingine ni hewa na hazitekelezeki
hivyo wananchi wapime kwa kina kila ahadi inayotolewa na chama au mgombea kama
inatekelezeka au la.
Alisema kwa sasa nchi
inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo maji,afya,elimu,barabara huku
akiweka wazi kuwa serikali imekuwa na nia thabiti ya kuleta maendeleo kwa
wananchi wake lakini anadhani kuna baadhi ya watendaji wa serikali hasa wa
ngazi za chini wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu kuhusu utendaji wao.
“Baadhi ya wizara
zimekuwa zikisuasua katika utendaji wake…lakini si kweli kwamba Rais atoi
kipaombele kwa wizara hizo shida hapa ni baadhi ya watendaji wa wizara hizo
kukwamisha baadhi ya shughuli mbona wizara ya ujenzi inafanya kazi zake vizuri
na wananchi tunaona? alihoji Chibwana.
Kwa upande wake Biena
Mohamedi (30) mkazi wa kijiji cha Kilimarondo Wilayani Nachingwea alisema Rais
wanayemtaka ni yule atakayeondoa kero mbalimbali zinazowakabili wanawake nchini
ikiwemo suala la afya ambalo wanawake ndio waathirika wakubwa.
Alisema kwa sasa baadhi
ya zahanati,vituo vya afya na hospitali nchini zimekuwa hazitoi huduma
kikamilifu hasa pindi akinamama hao wanapokwenda kujifungua kwani wengi wao
wamekuwa wakilazimika kulipia gharama kubwa licha ya serikali kutangaza kuwa
baadhi ya gharama kwa akinamama na watoto kuondolewa.
Nae mwalimu Magreth
Charles (29) anayefundisha shule ya msingi Kiegei Halmashauri ya wilaya ya
Nachingwea mkoani Lindi alisema Rais ajaye awe mkombozi wa matatizo ya
kihistoria ya walimu ambayo hadi sasa inaonekana utatuzi wake kutopatiwa
ufumbuzi licha ya serikali mara kadhaa kutoa matamko ya kumaliza kero zinazowakabili
walimu nchini.
Alisema walimu
wamekuwa wakinyanyaswa kwa kutopewa stahiki zao kwa wakati na hata mara
nyingine kutopewa kabisa mazingira yanayosababisha baadhi ya walimu hao
kujiingiza kwenye madeni na hivyo kushindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi
mkubwa.
Aisha Rajabu (30) ni
mkulima wa kijiji cha Kilimarondo ambaye alisema sekta ya kilimo inapaswa
kutizamwa upya ili kuwafanya wakulima nao kujiona ni sehemu ya watanzania ambao
wanapaswa kufaidi matunda ya nchi yao.
Alisema serikali
imekuwa ikileta mifumo kadhaa kwa wakulima akitolea mfano mfumo wa ununuzi wa
mazao kwa utaratibu wa stakabadhi ghalani ambao kwake yeye hauna shida bali
tatizo ni namna ya uendeshaji wake ambao umeonekana kumkandamiza mkulima na
kuiomba serikali ijayo kuboresha mfumo huo.
Alisema wakulima
wamekuwa wakijitahidi kulima mazao mbalimbali ili kujiletea maendeleo lakini
wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi hasa masoko ya bidhaa zao,pembejeo za
kilimo na elimu kutoka kwa maofisa ugani ambao kwa sasa hukaa maofisini badala
ya kuwafuata wakulima vijijini kusikiliza kero na matatizo yao.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD