TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
ZAIDI ya shilingi Bilioni3 zimebainika kuwa ni
hasara waliyoipata wafanyabiashara wa soko kuu la Mkuti Halmashauri ya Mji wa
Masasi mkoani Mtwara ambalo usiku wa julai 24 liliteketea kwa moto kutokana na
hitilafu ya umeme iliyotokea kwenye duka moja la vinywaji baada ya Tanesco kuzima
na kuwasha kwa ghafla umeme.
Akitoa taarifa hiyo
ya awali ya tathimini ya soko la Mkuti baada ya kuungua kwa moto mkuu wa wilaya
ya Masasi Bernald Nduta alisema kamati ya uchunguzi iliyoundwa ilipata maelezo
kutoka kwa uongozi wa soko hilo kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu katika
mfumo wa umeme sokoni hapo.
Alisema taarifa ya awali
inaonesha kuwa soko hilo la Mkuti lilikuwa na wafanyabiashara 700 huku mabanda
ya kudumu yakiwa 200 na kwamba kati ya hayo yaliyoathirika ni mabanda 90 ambapo
mabanda ya muda mfupi maarufu vizimba yapatayo 330 yote yameteketea kabisa kwa
moto huo.
Alisema kwa mujibu wa
taarifa kutoka kwa kamati ya uchunguzi,viongozi wa soko hilo pamoja na
wafanyabiashara walioathirika wamepata hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni
3,270,000,000 ambapo thamani halisi ya banda moja la kudumu ni shilingi
7,000,000.
Aidha meza za
biashara au vizimba kila kimoja ni shilingi 3,000,000 huku upotevu wa nafaka au bidhaa ikiwemo mbogamboga
na nyinginezo kwenye kila kizimba kimoja ni shilingi 5,000,000 na kufanya jumla
kuu ya zaidi ya bilioni 3.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya alisema shughuli za
kiuchumi zilizokuwa zinafanyika katika soko hilo ni biashara za bidhaa
mbalimbai ikiwemo mcheleunga,maharage,mahindi,choroko,vitunguu,samaki,matunda,mbogamboga pamoja na bidhaa zingine za madukani ambazo
kiujumla wake zote zimeteketea kwa moto.
Alisema kwa sasa
shughuli za kiuchumi sokoni hapo zimesimama baada ya wafanyabiashara hao kukosa
aneo la kufanyia biashara zao kwa kuwa eneo lote limeteketea kwa moto huku
akitoa matumaini kwa wakazi wa mji wa Masasi kuwa hali ya chakula sio mbaya
kwani baadhi ya wafanyabiashara wana maghala ya kuhifadhia chakula nje ya soko
hilo.
“Ingawa upo uwezekano
wa kuwepo upungufu wa chakula endapo wafanyabiashara hawataingiza chakula
mapema…na hiyo itatokana na ukweli kwamba kwa sasa wafanyabiashara hao watakosa
sehemu ya kuhifadhia chakula hicho kutokana na soko hili kuteketea kwa moto
hivyo natoa wito kwa wafanyabiashara kutosubiri mpaka soko lijengwe upya
waendelee kuleta chakula”.alisema Nduta.
Aidha amesisitiza
kuwa kamati yake ya ulinzi na usalama imeendelea kuimarisha ulinzi katika eneo
lote la soko hilo kwa kuwazuia watu wote wasio kuwa wafanyabiashara wa soko
hilo kuingia ndani licha ya kukiri kuwa baadhi ya wafanyabishara wamepoteza
mali zao kwa kuibiwa na vijana ambao wengi wao tayari wanashikiliwa na jeshi la
polisi wilaya ya Masasi.
Kwa upande wake
mwenyekiti wa soko kuu la Mkuti Abdallah Mtandama alisema kwa sasa
wafanyabiashara hao wanahitaji eneo la kufanyia biashara kwa kipindi hiki cha
mpito hasa kwa wale ambao wametunza chakula kwenye maghala yao kwani kikikaa
kwa muda mrefu kinaweza kuharibika.
Alisema kwa sasa
wanasubiri tamko la serikali juu ya hatima yao kuhusiana na ujenzi wa soko hilo
huku wakitoa mapendekezo kwa ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa
Masasi waruhusiwe kujenga mabanda ya biashara yaliyoteketea kwa gharama zao kwa
kufuata taratibu za ramani itakayotolewa au kuendelea na ramani ya awali.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD