Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

SABA KIZIMBANI KWA KUVAMIA NA KUPORA MAGARI MADOGO ENEO LA MDENGA-NANGOO WILAYANI MASASI

TANGAZO
Clarence Chilumba,Masasi
WATUHUMIWA saba  wakazi wa kitongoji cha Mdenga  kijiji cha Nangoo  Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka sita  yanayowakabili ikiwemo kula njama pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha kijijini hapo.
Khatibu Buju (35), Ramadhani Dunga (25), Kazumari Mwema (21), Makasi Benedict (35), Mabruck Nurudini (22),Steven Salvatory (18) pamoja na mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 17 (Jina linahifadhiwa) walifikishwa mahakamani hapo jana  mbele ya Hakimu  wa mahakama ya wilaya ya Masasi Halfani Ulaya na kusomewa shitaka na mwendesha mashtaka Iddi Nassoro.
Nassoro alidai kuwa mnamo May 29 mwaka huu  majira ya saa 6:00 usiku hadi saa 10: 00 alfajiri katika eneo la kitongoji cha Mdenga-Nangoo watuhumiwa hao walipanga mawe pamoja na magogo makubwa ya miti katikati ya barabara kuu itokayo mkoani Mtwara kuelekea wilayani Masasi kwa lengo la kufanya uvamizi na uporaji kwenye magari.
Alidai jumla ya magari madogo sita yalivamiwa  na waporaji hao huku wamiliki na madereva wakipigwa na wengine kuumizwa vibaya ambapo pia majambazi hayo yakifanikiwa kupora baadhi ya vitu vikiwemo simu,kadi za benki,nyaraka mbalimbali pamoja na fedha taslimu huku wakijua kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Nassoro aliieleza mahakama kuwa baada ya waporaji hao kukamilisha hazma yao waliyaruhusu magari hayo kuendelea na safari na wao kutokomea kusikojulikana lakini kutokana na jitihada za wasamaria wema kwa kushirikiana na jeshi la polisi watuhumiwa hao walifanikiwa kutiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani.
Kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kuhairisha kesi hiyo kupisha upelelezi kwa kuwa bado wako baadhi ya watu wengine wanahusika na tukio hilo.
Hakimu  Halfani Ulaya alikubaliana na ombi la mwendesha mashtaka na alihairisha kesi hiyo hadi Juni 16 mwaka huu itakapotajwa tena ambapo Watuhumiwa hao walirudishwa rumande kwa kuwa dhamana haikuwa wazi.
Mwisho.





TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top