Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

RUANGWA KUMEKUCHA!! UJENZI WA MGODI WA MADINI YA BUNYU (GRAPHITE) MBIONI KUJENGWA

TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Ruangwa.
MRADI wa madini ya Kinywe wa Nachu  (Nachu Graphite product) kupitia kampuni ya Uranex iko mbioni kujenga mgodi wa madini ya  Bunyu katika eneo la kitongoji cha Liwale-Namkongo wilayani Ruangwa mkoani Lindi ifikapo Desemba 2016.
Akizungumza jana wakati wa anatoa mada ya mradi huo kwenye kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkurugenzi wa kampuni ya MTL Consulting iliyopewa kazi ya ushauri wa mradi huo John Tindyebwa alisema viongozi wa wananchi wakiwemo madiwani wana wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya mradi huo ili kuwajengea uelewa.
Alisema tayari kampuni ya MTL Consultants imeanza tathimini pamoja na utambuzi wa mazingira ya eneo ambapo mgodi utajengwa na unatarajia kukamilika mwishoni mwa june mwaka huu ambapo kazi  ya upembuzi yakinifu wa mradi itakamilika Septemba na mwezi  Novemba kampuni inatarajia kupokea hati ya mazingira kutoka wizara ya mazingira baada ya kazi hiyo kukamilika.
Alisema tayari utambuzi wa eneo litakalojengwa mgodi huo tayari imekamilika katika kitongoji cha Liwale-Namkongo huku bwawa la kuhifadhia mabaki ya madini hayo litajengwa kaskazini mwa mgodi huo karibu na mto Mbwemkuru.
Alisema kuwa shughuli za usanifu wa awali wa mradi huo Zinatarajia kukamilika ifikapo Novemba mwaka huu huku ujenzi rasmi wa mgodi utaanza mwezi januari 2016 na kwamba uzalishaji unatarajia kuanza rasmi ifikapo Desemba 2016.
Kwa mujibu wa Tindyebwa alisema Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ni miongoni mwa wilaya nchini zilizobainika kuwa na kiasi kikubwa cha madini hayo ya Bunyu jina ambalo linatokana na lugha ya asili ya wenyeji wa wilaya hiyo (Wamwera) madini ambayo hapo awali yalikuwa yanatumika kwa ajili ya shughuli za kufinyanga vyungu.
Alisema kampuni ya Magnis Resources ya nchini Australia ndiyo iliyopewa kibali na serikali cha kuwekeza kwenye mgodi huo ikiwa ni pamoja na ujenzi inayotarajia kutumia kiasi cha fedha zaidi ya dola za kimarekani milioni 150 huku akikiri kuwa ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa kuwahi kutokea nchini.
Alisema baada ya upembuzi yakinifu wa eneo ambapo mgodi utajengwa wanatarajia kufanya mkutano wa hadhara na baadhi ya wananchi wapatao 600 ambao wanategemea kuwa watakuwa ni miongoni mwa watu watakaoathirika na mradi huo ili waone namna watakavyoweza kupanga utaratbu wa kulipa fidia za mali zao zitakazoharibiwa wakati wa ujenzi wa mradi huo.
Akizungumzia kuhusu namna ya wananchi wa wilaya hiyo wanakavyonufaika na ujenzi wa mgodi huo alisema jumla ya wafanyakazi 400 wanatarajiwa kuajiriwa na kampuni hiyo ya uwekezaji huku kwa upande wa Halmashauri inatarajia kupata kiasi cha fedha shilingi Bilioni 2 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 0.3 ya mapato yote.
Alisema mwekezaji yuko tayari kufanya mazungumzo na serikali ya wilaya kuona ni namna kampuni yake itakavyosaidia katika kuboresha miundo mbinu mbalimbali ikiwemo elimu,afya,maji pamoja na barabara ili wananchi wa wilaya ya Ruangwa waweze kunufaika na ujenzi wa mradi huo.
Kwa upende wake mkuu wa wilaya ya Ruangwa Mariamu Mtima alisema wananchi wa wilaya hiyo hasa wale wa eneo husika ambapo mgodi utajengwa wanapaswa kuunga mkono jitihada za serikali kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika kuboresha maisha ya watanzania.
Alisema madiwani nao kwa nafasi zao waendelee kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo hayo ili waweze kufahamu hatua kwa hatua katika mchakato mzima wa ujenzi wa mradi huo kwa lengo la kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza wakati na baada ya ujenzi wa mgodi huo.

Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top