TANGAZO
Dkt.Jabiri Bakari,Mtendaji Mkuu wa eGA. |
Na Clarence Chilumba, Dar es salaam.
Taasisi za serikali nchini
zimetakiwa kufanya mabadiliko katika mfumo wa barua pepe za serikali ili
kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo kwa sasa ulimwenguni
huku wito ukitolewa kwa taasisi hizo kuhakikisha zinatoa taarifa zake kwa wananchi
kwa wakati kupitia tovuti.
Hayo yamesemwa leo na mtendaji mkuu
wa wakala ya serikali mtandao Tanzania (e-Government Agency Ega) Dkt. Jabiri
Bakari wakati anafungua mafunzo ya siku
mbili ya uboreshaji wa barua pepe za serikali (GMS) yanayofanyika katika ukumbi
wa eGa jijini Dar es salaam.
Mafunzo hayo yanatolewa kwa maofisa
mawasiliano serikalini wa Halmashauri zote za mkoa wa Mtwara pamoja na
wachambuzi wa mifumo wa Halmashauri hizo yenye lengo la kuwajengea uwezo
wataalamu hao katika uboreshaji wa taarifa muhimu za serikali kupitia tovuti na
barua pepe mpya za serikali.
“Kwa sasa watumishi wengi wa
serikali wamekuwa wakitumia barua pepe zao binafsi katika kutuma taarifa
mbalimbali za serikali kitu ambacho kiusalama si kizuri kuachwa kikiendelea…hivyo
serikali kupitia Ega wameamua kubadilisha na kuboresha mfumo wa barua pepe hizo”.alisema
Dkt.Bakari.
Alisema wananchi wengi kwa sasa
wanahitaji taarifa muhimu kutoka kwa serikali na kwamba endapo taasisi hizo
zikibaki kuwa kimya ama kuchelewa katika utoaji wa taarifa muhimu za serikali
ziko athari ambazo zinaweza kutokea hasa kwa wakati ambapo wananchi wengi
wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii katika kupata taarifa mbalimbali.
Alisema wakati umefika kwa mikoa na
Halmashauri zote nchini kuwa na tovuti ambazo zitasaidia kutoa taarifa kwa
wakati kwa wananchi ikwemo namna ya ukusanyaji wa kodi wa kila Halmashauri
unavyofanyika,matangazo mbalimbali ya halmashauri pamoja na shughuli za
utekelezaji wa miradi ambazo wananchi wanapaswa kufahamu.
Kwa mujibu wa mtandaji huyo alisema
ni lazima wananchi wajue ni nini serikali inafanya katika taasisi zake zote
zilizopo nchini kwa lengo la kuondoa malalamiko mbalimbali yasiyo na msingi
ambayo kila siku yamekuwa yakielekekezwa kwa serikali kuwa haifanyi kazi kitu
ambacho si kweli.
Akizungumzia kuhusu ugunduzi wa gesi
asilia mkoani Mtwara alisema taarifa hizo ni muhimu kuwafikia wananchi kwa
wakati ili kutangaza fursa hiyo adimu mkoani humo kwa lengo la kuvutia
wawekezaji mbalimbali duniani kuja kuwekeza mkoani humo.
Alisema wengi hawafahamu uwepo wa
gesi kwa mikoa ya kusini ikiwemo Lindi na Mtwara lakini kupitia tovuti za
Halmashauri za wilaya na ile ya Mkoa wananchi wengi walio ndani na nje ya
Tanzania watafahamu namna hali ilivyo kwa sasa kwa mikoa hiyo mara baada ya
ugunduzi wa gesi asilia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma
za TEHAMA wa Ega Benedikt Ndomba alisema wakala ya serikali mtandao Tanzania
waliona umuhimu wa kuwa na mafunzo ya Barua pepe za serikali (GMS) kwa maofisa
hao kwa ngazi ya Halmashauri ili kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi
wa kila siku kupitia mifumo mbalimbali ya kiteknolojia.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD