TANGAZO
Ofisa Utamaduni Wa Halmashauri ya wilaya ya Raungwa Boppe Kyungu. |
Na Bashiru Kauchumbe,Ruangwa.
MANGARIBA wapatao 50 kutoka kwenye kata 22 wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi wameaswa kuzingatia
kanuni za afya ili waweze kujiepusha na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi pindi
wanapofanya kazi zao.
Maghariba hao ni wale wanaojihusisha na tohara kwa watoto wa kiume wilayani humo huku wakipewa
onyo kali kwa wale watakaoshindwa kufuata kanuni za afya kwao na kwa watoto hao
hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Rai hiyo imetolewa jana na ofisa utamaduni wa Halmashauri ya wilaya ya
Ruangwa Bope Kyungu wakati wa kikao cha
pamoja na Mangariba hao kwa ajili ya maandalizi ya kuanza kwa shughuli
za jando na unyago ambazo zinatarajia kuanza mapema juni mwaka huu.
Kila mwaka inapofika mwezi juni
baada ya shule za msingi kufungwa katika wilaya ya Ruangwa yenye wenyeji wa
asili wa kabila la Wamwera kunakuwa na mila na desturi ya jando kwa watoto wa
kiume na unyago kwa watoto wa kike ingawa kwa miaka ya hivi karibuni utaratibu
huo wa kufanya shughuli hizo kila mwaka umevurugika na hii ni kutokana na
mabadiliko ya hali ya hewa yanayoambatanana na ukame unaosababisha njaa.
Kwa mujibu wa Ofisa utamaduni wa
wilaya hiyo alisema kuwa wamelazimika kutoa tahadhari hiyo mapema mara baada ya
kugundua kuwa Mangariba wengi wamekuwa wakifanya kazi zao bila kuchukua
tahadhari yoyote ambapo alisema
mangariba wengi hutumia kifaa kimoja (Kisu) ambacho hutumika kwa watoto
zaidi ya mmoja wakati wa kutahiri watoto hao.
Suala hili kwa maghariba wilayani humo ni la kawaida
ambao wengi wao hutahiri watoto hadi kumi kwenye uwanja mmoja huku wakitumia
kisu kimoja ambacho pia huwa hakichemshwi zaidi ya kusafishwa kwa maji kuondoa
damu zinazobaki kwenye kifaa hiko baada ya kumaliza kumtahiri mtoto mmoja mazingira
ambayo huhatarisha afya za watoto na hata maghariba wenyewe.
Lakini Mbaya zaidi ni pale maghariba hao
wanapolazimika kufuga kucha ndefu mikononi mwao ambazo husaidia kuchuna ngozi
za watoto hao wakati wanafanya tohara hizo kitu ambacho ni wazi kuwa hakifai
kuachwa kikiendelea.
Aidha maghariba hao wamekuwa wakitahiri pasipo kuvaa
mipira ya mikono (Gloves) kama kinga jambo ambalo ni hatari kwa afya za
watoto hao ambao hata namna ya utaratibu wenyewe unakwenda kinyume na haki za
mtoto kwani hupelekwa porini na hutahiriwa wakiwa wamelazwa chini kwenye
mavumbi.
Akiongea na gazeti hili Abdallah Bonge mmoja wa
mangariba maarufu wilayani Ruangwa alisema ni kweli kuwa wamekuwa wakifanya
kazi zao bila ya kufuata kanuni za afya huku akikiri kuwa ni kitendo cha
kifahari kwa ngariba mmoja kutahiri watoto zaidi ya mmoja kwenye uwanja mmoja
wa shughuli hiyo ya jando.
Alisema inafikia hatua kwa maghariba hao kutumia hata
imani za kishirikina ili waweze kutahiri watoto wengi kwa siku kwa kutumia kisu kimoja bila kujali kuwa ni
hatari kwa watoto wanaofanyiwa tohara hiyo na hata kwa wao wenyewe.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa
ghariba mmoja wilayani humo ana uwezo wa kutahiri watoto hadi 15 kwa siku kwa
kutumia kisu kimoja na ghariba huyo ndiye anayependwa na wazazi kwa kigezo kuwa
anaweza kufanya kazi kwa haraka na vizuri.
Pia ipo imani kuwa watoto wanaofanyiwa tendo hilo la
kutahiriwa na ghariba kama huyo wanakuwa na uwezo mkubwa wa kushiriki tendo la
ndoa pale wanapofikia umri wa kuoa huku wazazi wengine wakikataa kuwapeleka
watoto wao hospitalini kwa madai kuwa ganzi wanayowekwa watoto hao kabla ya
kutahiriwa husababisha watoto hao kushindwa kushiriki kikamilifu tendo la ndoa
wanapofikia umri wa kuoa.
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya
ya Ruangwa Dkt. Joseph Anga alisema idara ya Afya wilayani humo itasimamia kikamilifu suala hilo kwa kuhakikisha
kuwa tohara iliyo salama inafanyika na
Mangariba hao huku akidai kuwa wako tayari kutoa vifaa salama vya kufanyia
tohara kama vile nyembe maalumu, dawa pamoja na mipira (Gloves).
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD