TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
IMEELEZWA Kwamba wilaya ya Masasi mkoani Mtwara ni miongoni mwa wilaya nchini zenye matukio mengi na makubwa ya wananchi kushambuliwa na hata kuuawa na wanyama wakali.
Aidha wanyama hao ambao wengi wao ni waharibifu husababisha uharibifu mkubwa wa mali,kujeruhi na hata kusababisha vifo vya watu wilayani humo kusini mwa Tanzania.
Wanyama wanaotajwa kuwa ni adui mkubwa kwa wananchi waishio kwenye maeneo yaliyopo kandokando ya Mito na maziwa ni pamoja na Mamba,Tembo,Fisi na Boko.
Hayo yalisemwa jana na mkuu wa wilaya ya Masasi Bernald Nduta wakati anawasilisha taarifa ya wilaya ya Masasi kwa waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu kwenye ukumbi wa ikulu ndogo mjini hapa.
Alisema maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa ni maeneo yaliyo karibu na hifadhi ya Msanjesi na maeneo yaliyo kandokando ya mto Ruvuma ambapo zaidi ya asilimia 90 ya matukio hayo husababishwa na Mamba waishio mto Ruvuma.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya ya Masasi alisema katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2014 jumla ya watu 48 walipoteza maisha huku 54 wakijeruhiwa na uharibifu wa mazao mbalimbali ukifanywa na wanyama wakali na waharibifu.
Aidha watu 34 kati ya 104 wamelipwa fidia na kwamba watu 68 waliobakia malipo yao yanaendelea kushughulikiwa na wizara ambapo malipo hayo yanategemewa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha 2014/2015.
Nduta alisema jitihada za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu zinafanywa kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhifadhi na namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya wanyama hao kwa njia ya mikutano na matangazo mbalimbali.
Alisema wizara ya maliasili na utalii iliamua kufanya sensa ya Mamba katika mto Ruvuma na kuvuna baadhi ili kupunguza tatizo la wanyamapori hao ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakiathiri maisha ya watu wilayani humo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD