TANGAZO
Mkurugenzi wa MacDonald Donald Masunga |
Na
Clarence Chilumba,Masasi.
Jumla ya shilingi milioni 900 zimetumika katika ujenzi wa mradi
wa shule ya MacDonald English medium iliyoko eneo la Mtandi halmashauri ya mji
wa Masasi lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha
sekta ya elimu nchini.
Shule hiyo iliyoleta changamoto kubwa wilayani Masasi kutokana
na ubora wake inamilikiwa na mtu binafsi ambaye amekuwa akifanya jitihada
kadhaa katika kuboresha miundo mbinu ya shule hiyo ikiwemo
barabara,usafiri,umeme pamoja na maji.
Mradi huo wa ujenzi wa shule hiyo ya mchepuo wa kiingereza
ulianza mwaka 2010 ambapo hadi sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 249 wa
darasa la awali hadi darasa la sita huku ikiwa na walimu 14 pamoja na watumishi
sita.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na "Blog ya Mtazamo Mpya" jana mkurugenzi wa shule hiyo Donald Masunga alisema dhumuni kubwa la kuanzisha shule
hiyo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kutoa elimu bora kwa wananchi
wake.
Alisema kama ilivyo katika ilani ya uchaguzi ya chama cha
Mapinduzi ya mwaka 2010 na katiba ya nchi ambayo inahimiza sekta binafsi
ikiwemo mashirika ya dini pamoja na watu binafsi kujenga vituo mbalimbali vya
kutolea elimu ili mradi viwe vimekidhi vigezo.
Alisema shule yake imesajiliwa kwa namba MT.03/7/EA kwa shule ya
awali ambapo kwa shule ya msingi namba ya usajili ni MT.03/7/002 huku akikiri
kuwa wananchi wa wilaya ya Masasi wamekuwa wakileta watoto wao shuleni hapo
kutokana na huduma bora za elimu zitolewazo.
Kwa mujibu wa Masunga alisema mradi huo umegharimu kiasi cha
shilingi milioni 900 na kwamba kati ya hizo milioni 400 sawa na asilimia 44
zimetokana na michango ya ada kutoka kwa
wazazi huku milioni 500 ambazo ni sawa
na asilimia 56 ni mkopo kutoka benki.
“Nilipata wazo la kubuni mradi huu mwanzoni mwa mwaka 2009 baada
ya kuona mji wa Masasi bado unahitaji kupata shule ya awali pamoja na msingi itakayofundisha
kwa kutumia mchepuo wa kiingereza…nakiri wazi kuwa wananchi wameniunga mkono
katika jitihada zangu za kuboresha sekta ya elimu wilayani Masasi”.alisema
Masunga.
Aidha mkurugenzi huyo alisema kuwa licha ya watoto wa wilaya ya
Masasi kupata elimu bora inayoendana na karne ya 21 ya sayansi na teknolojia
lakini bado kuwepo kwa shule hiyo kumesaidia kupunguza gharama kwa wazazi
waliokuwa wakitumia fedha nyingi kuwapeleka watoto wao shule zilizo kwenye
mikoa ya mbali nchini.
Alisema pia shule yake imesaidia kutoa ajira kwa watanzania kwa
maana ya walimu pamoja na watumishi wasio walimu sambamba na kuchangia pato la
Taifa kwa kulipa kodi.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wilayani hapa wameoneshwa
kufurahishwa kwao kwa kuwepo kwa shule hiyo ambayo imesaidia kupunguza gharama
walizokuwa wanakumbana nazo hapo awali kabla ya kuanzishwa kwa shule hiyo.
Mradi huo wa ujenzi wa shule ya MacDonald English medium
umezinduliwa rasmi hivi karibuni wakati wa mbio za mwenge wilayani Masasi na
kiongozi wa kitaifa wa mbizo za mwenge wa uhuru Juma Chumu.
Mwisho.
MKURUGENZI wa MacDonald English Medium School Donald Masunga akipokea cheti kutoka kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka huu Juma Chumu ikiwa ni uzinduzi rasmi wa shule hiyo iliyoko katika eneo la Mtandi Halmashauri ya mji wa Masasi.
MMOJA wa walimu wa shule hiyo akisoma taarifa fupi kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa aliyetembelea shuoeni hapo hivi karibuni kwa ajili ya uzinduzi wa shule hiyo.
WANAFUNZI wa shule ya Mc Donald English Medium School wakicheza wimbo maalumu kabla ya uzinduzi rasmi wa shule yao hivi karibuni mwenye sare ni mmoja wa wakimbiza mwenge wa uhuru mwaka huu.
ILIKUWA ni shangwe na vigelegele kwa wanafunzi wa shule ya McDonald Kwa kuzinduliwa kwa shule yao hivi karibuni na kiongozi wa mbio za mwenge.
WAKIWA wameshika Bango lililokuwa na ujumbe wa mwenge wa uhuru mwaka huu 2015 shuleni hapo.
MKE wa Mkurugenzi wa McDonald English Medium School akicheza kwa furaha pamoja na wanafunzi wake wakati wa uzinduzi wa shule hiyo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD