TANGAZO
BAADHI ya walimu wakiwa kwenye mafunzo |
Na Clarence Chilumba,Masasi.
JUMLA ya walimu 99 kutoka kwenye
shule 33 za Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara wanapatiwa mafunzo ya
masomo ya Sayansi,Hisabati na Kiswahili kutoka kwa Mamlaka ya elimu Tanzania
(TEA) yanayofanyika katika ukumbi wa shule ya msingi Mkomaindo mjini hapa.
Mafunzo hayo ya siku tano
ambayo yanalenga kuwapa mbinu mpya za
ufundishaji walimu hao zitakazosaidia kuinua kiwango cha ufaulu katika masomo
hayo ambayo yamekuwa changamoto kubwa katika ufaulu wa wanafunzi nchini.
Akizungumza na Blog ya Mtazamo Mpya
hii leo Ofisa kutoka idara ya utawala ya Mamlaka ya elimu Tanzania Azana Lujina
alisema mafunzo hayo yameandaliwa na TAMISEMI kwa kushirikiana na wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kwamba lengo ni kuwajengea uwezo walimu wa shule za
msingi nchini ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na serikali ya matokeo
makubwa sasa (BRN) katika sekta ya elimu.
Alisema Mamlaka ya elimu nchini
imekuwa ikiendesha mafunzo hayo kwa awamu katika mikoa mbalimbali nchini
ikiwemo Kilimanjaro,Tanga,Mwanza na Mtwara ambapo walimu wengi waliohudhuria
mafunzo hayo wamekuwa wakikiri kuwa bado tatizo ni kubwa katika Masomo hayo.
Alisema katika tafiti mbalimbali
ilibainika kuwa kuna baadhi ya mada katika masomo ya hisabati,Kiswahili na
kiingereza ni ngumu na ambazo wanafunzi wengi wamekuwa wakifanya vibaya
mazingira yanayopelekea masomo hayo kuonekana magumu kitu ambacho hakina ukweli
wowote.
Kwa mujibu wa Lujina alisema TEA
imeyapa kipaombele maeneo yote ambayo yamekuwa na utata katika masomo hayo
nchini ikiwemo mkoa wa Mtwara ambao kwa sasa mafunzo yanaendela katika halmashauri ya mji wa Masasi.
Kwa upande wake mwalimu Upendo Nkane
ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo alisema ni vyema serikali kupitia
wizara ya elimu wakaweka utaratibu maalumu wa mara kwa mara ili kuweza kuwapa
elimu walimu hao wa shule za msingi.
Alisema pia iko tofauti ya namna ya
ufundishaji kwa walimu wenyewe wanaofundisha masomo hayo huku akitolea mfano
kuwa mwaka 2005 akiwa chuoni alifundidhwa kuwa MSAMIATI ni moja ya mada kuu katika somo la kiswahili lakini
cha kushangaza alipofika shuleni kwa mara ya kwanza kuja kuanza kazi alikuta
walimu wanaofundisha somo la kiswahili wakidai kuwa Msamiati ni mada ndogo.
Nae
mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo mwalimu Buruhani Makotha alisema katika
mafunzo hayo jumla ya mada tisa kwa kila somo zimechaguliwa zikiwemo Mada ya
Aljebra na Jometri kwa somo la hisabati,mada ya Sarufi kwa somo la kiswahili pamoja
na mada ya aina za maneno kwa somo la kiingereza
Alisema
lengo la kufundisha mada hizo ni kuwajengea uwezo walimu katika ufundishaji
pamoja na kuwapa stadi mbalimbali wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika
mitihani yao.
WALIMU kutoka kwenye shule 33 za Halmashauri ya Mji wa Masasi wakiwa kwenye mafunzo hayo ya siku tano kwenye ukumbi wa shule ya msingi Mkomaindo Mjini Masasi hii leo. |
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD