TANGAZO
Na Bashiru Kuchumbe,Ruangwa.
Wakazi wapatao 2517 wa kijiji cha Chingumbwa kilichoko kata ya Mbekenyera Wilayani Ruangwa afya zao
zipo hatarini kwa kukosa huduma ya maji safi na salama kwa takribani miaka 60
sasa tangu kijiji hiko kianzishwe.
Hayo yalisemwa na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakati wanaongea na Mwandishi wa habari wa Blog ya mtazamo mpya aliyetembelea kijijini hapo mapema wiki hii.
Hadija Hamisi na Amina Mkango ni baadhi ya wananchi wa kijiji
hiko ambao walisema kijiji cha
Chingumbwa hakina kisima hata kimoja cha maji jambo ambalo limesababisha wakazi
wa kijiji hicho kuishi kwa kunywa maji ya bwawa ambayo sio safi na salama kwa
kuwa maji hayo yanatumika kwa shughuli mbalimbali ikiwamo shughuli ya kusafishia
madini ambayo yamekuwa na kemikali ambazo ni hatari kwa afya za binadamu.
Walisema kwa nyakati za
kiangazi maji huwa yanapatikana kwa shida kutokana na
bwawa hilo kukauka mazingira
yanayopelekea kusafiri umbali mrefu kufuata maji.
Kwa upande wake Ramadhani Hamisi alisema kwa mwaka huu hali ya upatikanaji wa maji kijijini
hapo itakuwa shida kutokana na hali ya
ukame ulioikumba wilaya ya Ruangwa na kwamba tayari bwawa ambalo wanalitegemea kupata maji japo sio
safi na salama limeanza kupungua maji na hakuna sehemu nyingine wanayoitegema
kupata maji zaidi ya bwawa
hilo.
Mtazamo mpya ilipiga hatua mpaka Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji ili
kujua kama kuna mipango yoyote ya kupata huduma ya maji katika kijiji
hicho,lakini alikiri kuwa hadi sasa kijiji hakijaibua mpango wowote wa kupata
mradi wa maji safi na salama .
Nae mwenyekiti wa kijiji hiko
Abdala Manjakali ameiomba Halmashauri ya Wilaya Ruangwa kukipatia huduma
ya maji kijiji cha Chingumbwa ili kuzinusuru afya za wakazi wa kijiji hiko kutokana na kunywa maji yasiyo safi na salama.
MWISHO
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD