TANGAZO
Na Fatuma Maumba,Mtwara.
SHIRIKA la Umeme Tanzania Tanesco
wamekamilisha mpango wa kupanua uwezo wa kituo cha kuzalisha umeme cha
mkoani Mtwara, kwa kuongeza mtambo mpya wa gesi wenye uwezo wa kuzalisha
megawati 20 unaotarajia kukamilika mwishoni
mwa julai mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba, wakati wa sherehe
fupi ya kukabidhi magari madogo aina ya Double cabin 132 ambayo yamesambazwa kwa
wilaya zote nchini nia ikiwa ni kuziwezesha wilaya hizo kufanya kazi kwa ufanisi
zaidi.
Alisema sambamba na hilo wamepanua mfumo wa
usambazaji katika mikoa ya Mtwara na Lindi kutoka Volti 33 hadi Volt 132 na kujenga substation mbili kubwa
Mtwara pamoja na Mnazi mmoja.
Hata hivyo, alisema Tanesco kwa kushirikiana na Symbioni
imekamilisha upembuzi yakinifu wa mtambo mkubwa wa umeme wa megawati 400
utakaojengwa Mkoani Mtwara pamoja na njia kubwa ya umeme ya kutoka Mtwara
kwenda Songea ya kilovolti 400.
“Pamoja na kuleta magari haya madogo,
Tanesco imeagiza magari makubwa (malori yenye crane) kwa idadi hiyo ambayo pia
yatasambazwa wilayani…Nia ya shirika ni kuhakikisha kwamba huduma zinaboreshwa,
umeme unapatikana kwa uhakika zaidi, miradi inatekelezwa kwa ubora na kwa
wakati, wananchi wanahudumiwa kwa wakati pasipo ubabaishaji wowote, kazi
zinafanywa kwa kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa.
Alisema pamoja
na magari hayo ya kufanyia kazi, shirika limeagiza vifaa vya kisasa vya
kuchimba mashimo, kusimamisha nguzo na kuvuta nyaya ambavyo zitafanya kazi zao
zifanyike kitaalamu na kwa ufanisi wa hali wa juu tofauti na ilivyo sasa.
Mramba alisema Mikoa ya Lindi na Mtwara ina jumla ya
wafanyakazi 215, aidha mikoa hii inawafanyakazi wa mkataba 32 na katika
kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme mikoa hii hutumia wafanyakazi wa kazi
maalumu (vibarua) wastani wa 159 kwa mwezi hivyo kuchangia katika kutoa ajira
katika mikoa hiyo.
Miradi ya kupeleka umeme vijijini
yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 32.5 inaendelea kutekelezwa katika
mikoa ya Lindi na Mtwara na inatarajiwa kukamilika mwezi juni mwaka huu na
sambamba na hilo miradi ya kupeleka umeme katika maeneo yanayopitiwa na bomba
la gesi inaendelea kutekelezwa kwa pamoja kati ya REA, TANESCO na TPDC
Alisema katika kushirikiana na jamii
inayopitiwa na miundombinu, shirika huingia mikataba na wana vijiji katika
kusafisha njia za umeme kila mwaka, mfano maeneo ya Mtawanya, Ziwani,
Mtendachi, Madimba, Mbwala chini, Nanguruwe, Ndumbwe na Mpapura.
Mwisho.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba, akizindua na
kukabidhi magari 132 ambayo yatasambazwa nchi mzima (picha na Fatuma Maumba)
Aliyesimama ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba, kutoka kushoto wa
kwanza waliokaa ni Mhandisi John Bandiye,Meneja Tanesco mkoa wa Lindi, wa
pili ni Mhandisi Azizi Salumu, Meneja Tanesco mkoa
wa Mtwara, kutoka kulia wa kwanza waliokaa pia ni Meneja wa Kituo cha kuzalisha
Umeme power plant Mtwara, Mkulungwa Chinumba na wa pili ni Mhandisi
Mahenge Mugaya,Meneja Mwandamizi wa Tanesco Kanda ya Dar es Salaam na
Pwani.(picha na Fatuma Maumba)
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD